MWIGULU, GHASIA WAKIMBILIA KUJISAFISHA
MLIPUKO wa bomu uliotokea wiki iliyopita katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani kwa CHADEMA mkoani Arusha na kuua watu wanne, umeiweka kwenye wakati mgumu serikali ya CCM, Jeshi la Polisi na Bunge. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema juzi bomu lililolipuliwa katika mkutano wa CHADEMA ni la kijeshi na limetengenezwa China na uzoefu unaonesha hutumiwa na wanajeshi kujihami wakiwa katika makabiliano na maadui vitani. Wakati Pinda akitoa kauli hiyo bungeni, viongozi wa CHADEMA wamelihusisha Jeshi la Polisi na tukio hilo huku wakidai wanao ushahidi unaonesha askari aliyevalia sare akilirusha kwenye mkutano huo. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijamii, wamelidokeza Tanzania Daima kuwa kukiri kwa serikali kuwa bomu hilo limetengenezwa China, inapaswa iibane nchi hiyo ieleze iliyemuuzia na alivyoliingiza nchini.
“Kwanini isiundwe tume huru nchini ili nchi ya China iulizwe baada ya kutengeneza bomu hilo ilimuuzia nani? Na kama haikuiuzia serikali, basi ni dhahiri tuiulize China kwanini inafadhili vikundi vya kigaidi nchini kwetu? “Je, kama bomu lilitengenezwa China, tuangalie kama mkataba wa majukumu ya mataifa duniani kuhusu silaha, nchi hiyo inatakiwa kutoka na kauli kuhusu bomu hilo na kwa kukaa kimya maana yake wanakubaliana na maelezo ya serikali,” alisema. Wakati maswali hayo yakionekana kuumiza vichwa vya watawala, viongozi wa CHADEMA kwa upande wao wamegoma kutoa ushahidi walionao kwa Jeshi la Polisi mpaka Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume ya kijaji itakayosikiliza ushahidi huo na kuendesha kesi hiyo.
Hali ya mambo ikiwa hivyo, viongozi wa CCM na wabunge wameanza kulitumia Bunge kukishambulia CHADEMA kuhusu mlipuko huo kwa lengo la kukinusuru chama chao, Tanzania Daima limedokezwa mbinu hiyo. Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, juzi bungeni walidai kuwa CHADEMA ndio wamekuwa wakihusika na vurugu zote zinazohusisha mauaji nchini. Kauli za viongozi hao zinakuja takriban siku tano tangu Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kudai CHADEMA kiliandaa na kuratibu shambulio hilo ambalo lilitokea kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani. Licha ya Mwigulu kujadili jambo lililokuwa nje ya mjadala wa bajeti na linaloendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimwacha aendelee kukilaumu CHADEMA ikionekana ni mkakati rasmi wa kulinasua Jeshi la Polisi na serikali ya CCM kwenye tuhuma hizo.
Katika madai yake, Mwigulu alianza kusema kuwa jambo la usalama wa nchi hii amekuwa akiliongelea kwa haraka haraka, hivyo watu wamekuwa hawamwelewi. “Leo naomba nilisema kwa utaratibu, jambo la usalama nimekuwa nikilisema na kuomba kama Elia aliyemwambia mtumishi wake kuwa anamwombea Mungu amfungue macho ya kimungu ili aone jinsi yeye anavyoona. “Jambo limetokea kama hili la Arusha, nimeyaongea sana mambo haya na sasa hivi ilipotokea mimi nitasema tena na wenzetu nikiwasema mara wanasema wataenda jimboni. Nawashauri wasiende tu jimboni, bali wajenge kabisa makao makuu ya chama chao,” alisema. Mwigulu ambaye alikuwa akishangiliwa na baadhi ya wabunge na baadhi ya mawaziri akiwemo William Lukuvi, George Mkuchika, Ghasia, Mary Nagu na wengine alisema anausema ukweli.
“Ni lazima tuwaze tuvuke mipaka, kuna mambo yanawezekana kabisa yakawa yamejificha pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu wanafikiria CCM inaweza kushiriki. “Mimi niwaambie CCM, hata bila kushiriki, moja kwa moja inawekwa kwenye lawama, jambo kama hilo likitokea. Ila CCM haina ushiriki katika jambo kama hili kwa sababu ndio watu wake kupitia serikali yake inatakiwa kuwahakikishia usalama,” alisema. Alisema kuwa ni lazima waangalie maana wengine waliojaa ushabiki linapotokea jambo wanakwenda moja kwa moja kuwa inawezekana CCM imeshiriki. Mwigulu aliongeza kuwa lazima yaangaliwe mazingira ya nchi kwa sasa, hasa kipindi hiki ambapo wanakuja wageni wakubwa wakiwamo marais wa China na Marekani, kwamba mataifa mengine ambayo yanajua ujio wa wageni ni biashara, wanaweza kuichafua Tanzania.
“Sisi tunakimbilia tu CCM ndiyo imejaa midomoni mwa watu, lakini hoja nyingine Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, hivi wale ambao hawatutakii mema hamjajua eneo wanaloweza wakagusa?” alihoji. Huku akinukuu ripoti ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhusu utekwaji wa Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda, katibu huyo alidai CHADEMA imetajwa kuwa ndiyo inahusika na matukio hayo ya utekeaji kwa kushirikiana na maofisa usalama wasio waadilifu ili kuonesha kuwa CCM imeshindwa kuongoza na sasa inaua watu wake. “Niliwahi kulisema hili kuwa kuna mambo mengine yanafanyika kwa hujuma na tumeziona hizo hujuma lakini watu wengine wanawahi kuamini haraka. “Lakini hawa wenzetu kama waliwahi kumvalisha raia sare za jeshi na alihukumiwa, wanashindwaje kila wakati wanasema polisi… polisi. Tunashindwaje kuamini kama wanaweza kumvalisha mtu nguo za polisi na akafanya yale?” alihoji.
Mwigulu alisema taarifa ya Polisi Mkoa wa Morogoro kuhusu tukio la kifo cha kijana Ali Zona, kilichotokea wakati wa maandamano ya CHADEMA, zinasema chama hicho ndicho kilihusika. “Yule kijana aliyeuawa Morogoro taarifa zilizopo hakuuawa na polisi, ni CHADEMA wao wenyewe walitoka pale wakatengeneza ile vurugu wakamfyatulia risasi ili kutengeneza kwamba serikali ya CCM inakandamiza wapinzani,” alisema. Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi aliongeza kuwa hata video ya mauaji ya Arusha iliyowekwa kwenye mtando wa You tube inaonesha wazi kuwa yalipangwa. “Yule aliyekuwa anachukua video eti hakushtushwa kabisa na lile bomu, aliendelea kufuatilia kama vile ni mkanda wa harusi. Iliwahi kutokea wapi mchukua video kwenye mkutano wa hadhara kitu ambacho hakikupangwa kimelipuka, kinaua watu, yeye anendelea kama anachukua ‘sendoff’?” alihoji.
Baada ya Mwigulu kumaliza, Hawa Ghasia ambaye ni mjumbe wa NEC alipewa nafasi ya kuchangia bajeti hiyo kwa kujibu hoja za baadhi ya wabunge, lakini naye akatumia muda mwingi kuilaumu CHADEMA kwa matukio ya vurugu nchini. Ghasia alitumia muda huo kupanda mbegu ya ubaguzi wa kimaeneo akidai kuwa CHADEMA wamechochea vurugu Mtwara, Mwanza, Mbeya, Morogoro na sasa Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo kama Mkoa wa Kilimanjaro wanakotoka baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho. Ghasia alisema wiki iliyopita alikuwa Kilimanjaro anakotokea Mbowe na Ndesamburo, hakuona vurugu za kuchoma matairi wala kupigwa kwa mabomu kama ilivyo Arusha. “Jamani tuwe macho na hawa CHADEMA hawataki wawekezaji waende mikoa mingine tofauti na Kilimanjaro ndiyo maana wanahamasisha vurugu katika mikoa ya wenzao.
“Wanafanya vurugu Arusha ili watalii wagome kwenda huko, wanataka watalii wakimbilie Kilimanjaro. Jamani tusiwakubalie hawa jamaa wataliingiza taifa letu kubaya,” alisema. Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji alisema kinachofanywa na CHADEMA mkoani Arusha na kwingineko kinaathiri uwekezaji kwani wawekezaji watakimbilia nchi jirani. Nagu alisema kutokuwapo kwa wabunge wa CHADEMA kumelifanya Bunge liwe tulivu tofauti na linavyokuwa wakiwapo wabunge hao. Katika kile kinachoonekana wabunge wa CCM walijipanga kikamilifu kukisulubu CHADEMA, kilichokosa wawakilishi, Waziri asiye na wizara maalumu, Mark Mwandosya, alitumia kauli mbalimbali za mafumbo kukinanga chama hicho cha upinzani.
Mwandosya alisema anaamini uchaguzi mkuu ujao, watu watachagua amani dhidi ya vurugu, upendo dhidi ya chuki, amani dhidi ya vita huku kwenye siasa watachagua vyama vinavyowaelekeza katika maendeleo na si vile vinavyowaelekeza katika vurugu, migogoro na machafuko. Kutokuwepo kwa wabunge wa CHADEMA pia kumeonekana kunatoa nafuu ya mijadala ambapo Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema mijadala mbalimbali iliyofanyika kwa siku nne imekwenda vizuri na Bunge limekuwa kama la zamani. Wakati hali ya mambo ikiwa si shwari ndani ya CCM, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanawasiliana na makachero wao kuangalia hatua za kisheria wanazoweza kuwachukulia viongozi wa CHADEMA waliogoma kutoa ushahidi. Alisema maelezo ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwa waandishi wa habari aliozungumza nao hivi karibuni ni tofauti na yale waliyoyatoa polisi, hivyo jeshi hilo litaangalia njia za kuuthibitishia umma kuwa tuhuma dhidi yao si za kweli.
Source: Isango J., & Kamkara E. (June 2013). Bomu lawatesa CCM, Polisi. Rtrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment