Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, June 22, 2013

Pinda amevunja katiba


        SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwataka polisi watembeze mkong’oto kwa watu wanaokaidi sheria na kanuni mbalimbali za nchi, wadau mbalimbali wamesema kiongozi huyo amepotoka na anapaswa kuomba radhi. Wakizungumza na Tanzania Daima, wadau hao walisema, Pinda amevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoapa kuilinda na kuitetea. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13(2) inasema: “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka sharti lolote ambalo ni la kibaguzi ama wa dhahiri au taathira yake.”

       Kifungu cha nne cha ibara hiyo hiyo kinasema: “Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi.” Pinda alitoa kauli hiyo akiwa anatekeleza kazi yake kama Kiongozi wa Serikali Bungeni. Katiba Ibara ya 13 (6) (e) inaonya kuwa: “Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha, pia Ibara ya 16 ya Katiba inasema: “Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi ya nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na pia heshima na hifadhi ya maskani na mawasiliano yake binafsi.” Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma juzi Alhamisi, Pinda alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia, kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”

     Waziri Mkuu alijibu: “Ni lile lile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu. Hakuna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria. “Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndiye jeuri zaidi, watakupiga tu. Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, maana tumechoka.” Kauli hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu nchini. Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Wakili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, Mabere Marando, alisema: “Nimeishangaa kauli ya Pinda, na ni aibu kubwa kwa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanasheria wote waliohitimu miaka ya 1970, ambapo kulikuwa na walimu wazuri, hatuna cha kusingizia kuwa hakuelewa sheria.

    “Niseme tu kwamba kauli ya Pinda ni kibali kibaya sana kwa vyombo vya dola, na ni uthibitisho kuwa mwenendo wa serikali na polisi kuua kisha kupandishwa vyeo si bahati mbaya, ila ni msimamo wa serikali,” aliongeza Marando. Alisisitiza kwamba, kauli ya Pinda kusema wamechoka, maana yake hawataki kuwasikiliza wananchi tena, na Pinda anatoa kibali kuwa wananchi wakienda kuuliza au wakiwa na jambo ambalo hawajaelewa basi wapigwe na viongozi, huu ni ushauri mbaya sana, tena kutoka kwa waziri mkuu wa nchi. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema kauli ya Pinda ni sawa na kumwaga Petroli kwenye mafuta ya taa.

     “Kauli yake imejaa jazba na yeye kama kiongozi mkubwa katika nchi hii hakupaswa kutoa kauli hiyo, bali alipaswa kutumia busara, kauli hiyo inayovipa mamlaka vyombo vya usalama kujichukulia sheria mkononi inaigawa nchi, ifahamike kwamba chombo chenye kuhukumu ni mahakama pekee na si yeye waziri mkuu au polisi,” alisema. Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo – Bisimba, alisema Pinda hakustahili kutoa kauli hiyo iliyojaa jazba bali alipaswa kuwa na busara na kuzungumza kwa kuzingatia sheria za nchi badala ya kutoa matamshi yasiyo na mwafaka kwa nchi. Hii ni mara ya pili kwa Pinda kutoa kauli inayokiuka haki za binadamu, ambapo mara ya kwanza ni alipozungumzia mauaji ya albino.

       Alikuwa akihutubia wakati wa kufungua Mkutano wa 16 wa Shirikisho la Vyama vya Kuweka na Kukopa (SCCULT) kwenye ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Januari 23, 2009. Pinda alisema iwapo wananchi wataendelea kuwahurumia wauaji hao ambao wanatafuta viungo vya albino wakitegemea mahakama itatenda haki huku nao wakiongeza kasi ya mauaji kwa Watanzania, watakuwa wanakosea. Hivyo alisema kwamba: “Kuanzia sasa mtu yeyote atakayemuona mtu amemkata shingo au mkono mweziwe, basi naye auawe papo hapo, hii itakuwa ndiyo dawa, kwani viongozi wote tumechoshwa na mauaji hayo. ”Mkimuona mtu anamkata mwingine shingo, naye muueni, kwani sasa viongozi wote tumechoka. No more, I can’t tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena).”

     Ingawa alipohojiwa bungeni katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo alilia na kutoa utetezi kuwa: “Nilionya kuwa sisi kama serikali hatuwezi kuvumilia hali hii, nilifanya hivyo nikiamini kuwa lugha hiyo ya kuwatisha itasaidia. Sasa kama Watanzania wanaona nimefanya ovu vema, lakini nia yangu ilikuwa njema kabisa. Naomba mnisaheme sana kama nimekosea,” alisema kwa huzuni Pinda huku akifuta machozi. Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema kauli hiyo ya Pinda inathibitisha kwamba matukio ya vyombo vya ulinzi na usalama kutumia nguvu kubwa kupindukia na kusababisha mauaji ya raia na uharibifu wa mali yanatokana na maagizo ya serikali.

     Mnyika alisema kauli hizo zinatoa mwelekeo kwamba ni sera ya serikali kutumia mabavu kinyume cha Katiba ya nchi, na bila kuheshimu utawala wa sheria, hivyo serikali inakiuka Katiba na utawala wa sheria na imepoteza uhalali wa kuwanyoshea vidole wananchi pale wanapojichukulia sheria mikononi, pale vyombo vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi linapoacha kuchukua hatua dhidi ya uhalifu. “Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuwajibika sasa kwa kubariki matendo ya mauaji na utesaji. Itakumbukwa ni waziri mkuu huyu huyu alitumia kauli ya, ‘Liwalo na liwe’, wakati wa mgomo wa madaktari na hatimaye Dk. Ulimboka akatekwa na kuteswa katika mazingira ambayo vyombo vya ulinzi na usalama vinatuhumiwa kuhusika,” alisema.

Source: Tanzania Daima (June 2013). Pinda amevunja katiba. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: