Baraza la Habari Tanzania (MCT) limesema kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ya kuwaagiza polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri za askari hao, inatia shaka kama ina lengo jema la kulinda amani na utulivu nchini kwa kuwa vitu hivyo haviwezi kulindwa kwa kutumia nguvu za dola. Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema hayo alipokuwa akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani, kufungua kongamano la maadili ya wanahabari la mwaka 2013, lililoandaliwa na Baraza hilo kwa lengo la kujadili ‘Wajibu wa vyombo vya habari kupambana na kauli za chuki na itikadi kali’, jijini Dar es Salaam jana. Mukajanga, ambaye hakumtaja kwa jina Pinda, alisema kauli za chuki zimekuwa si kitu cha nadharia, bali hivi sasa zinasikika katika kila kona ya nchi, ikiwamo barabarani, kwenye mabaa na hata misikitini na makanisani pia.
Hivyo, akasema shaka juu ya kauli kama hiyo ya Pinda inakuja kwa kuwa polisi hawajafunzwa kuchambua jambo hilo, hivyo kuna hatari kutumiwa vibaya na kusababisha kuvuruga utulivu nchini. Jaji Bomani akifungua kongamano hilo, alisema hakuna ruhusa ya matumizi ya nguvu na silaha za moto kiholela, bali mambo hayo yana sheria zake, ambazo zinatakiwa zizingatiwe. Aliwashauri wanahabari kuwa na maadili mema akisema sifa hiyo itawafanya waaminike na kukubalika katika jamii. Katika kongamano hilo, Jaji Bomani alizindua kitabu cha ‘mwongozo wa kufundisha maadili ya habari’ kilichoandikwa na Pili Mtambalike na marehemu Alfred Mbogora wa MCT, na kuwakabidhi waandishi wa habari wa mkoani Mtwara mavazi maalum ya kuwatambulisha wanapokuwa kazini.
Kongamano hilo lilijadili mada mbili, ikiwamo ya ‘Wajibu wa vyombo vya habari kupambana na kauli za chuki’ na ‘Itakadi kali na kwanini vyombo vya habari Tanzania viepuke kuandika kauli za chuki na itikadi kali’. Mada hizo ziliwasilishwa na wanahabari nguli; Makwaia wa Kuhenga na Ndimara Tegambwage na kuchambuliwa na Mwalimu Bashiru Ally na Dk. Ayub Rioba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Source: Said M. (June 2013). Baraza la Habari laishtukia kauli ya Pinda. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment