Kushamiri kwa vitendo vya ujangili nchini kumeifanya Tanzania kutajwa kuwa moja kati ya nchi nane zinazoongoza katika biashara haramu ya pembe za ndovu huku pia nchi za Kenya na Uganda zikitajwa.Katika mkutano wa Kimataifa wa Biashara kwa Viumbe Vilivyopo Hatarini Kutoweka (CITES) uliofanyika Bangkok, Thailand, mwezi Machi mwaka huu, Tanzania ilitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi nane zilizo mstari wa mbele katika biashara ya pembe za ndovu. Nchi hizo ambazo zinatambuliwa kama kundi la wanane ‘gang of eight’ ni pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda, ambazo zimewekwa katika kundi la nchi zinazozalisha pembe hizo. Nchi zilizowekwa katika kundi la wanunuzi ni China na Thailand, Malaysia, Vietnam na Ufilipino.
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Alexander Songorwa amethibitisha kupelekwa kwa ripoti hiyo, lakini akakataa kuyataja mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti kwa madai kuwa hawezi kuzungumzia masuala hayo kwenye simu na kumtaka mwandishi kwenda ofisini kwake Jumatatu. “Ni kweli tumepeleka ripoti hiyo CITES, lakini siwezi kuizungumzia, zaidi nakuomba uje ofisini kwangu siku ya Jumatatu nitakufafanulia,” alisema Songorwa. Alipopigiwa simu Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki alimtaka mwandishi kumpigia baada ya saa moja, lakini alipopigiwa tena simu yake ya mkononi haikupokewa.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na CITES kupitia mtandao wake mwishoni mwa wiki, inaitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi nane zilizowasilisha ripoti inayoeleza namna itakavyotokomeza biashara ya pembe za ndovu. Awali kamati ya CITES ilikuwa imeweka Machi 15, mwaka huu kuwa ni siku ya mwisho kwa nchi hizo kuwasilisha mipango yake. Nchi nyingine zilizowasilisha mpango kazi ni pamoja na Uganda, Kenya, Vietnam, China, Singapore, Malaysia, Ufilipino na Thailand.
Katibu Mkuu wa CITES, John Scanlon alisema ripoti ya kila nchi itapelekwa katika kamati maalum ambayo itafuatilia mapendekezo yaliyotolewa kwa kuyafanyia kazi ikishirikiana na nchi husika. “Itakapofika Julai 2014, Sekretarieti itatoa tathmini ya mapendekezo yaliyotolewa na kila nchi na namna yalivyotekelezwa,” alisema Scanlon. Akitoa hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Utamaduni na Utalii kwa mwaka 2013/2014, Kagasheki, alisema Wizara itaendelea kutekeleza mikataba na makubaliano ya kikanda na kimataifa ukiwamo ule wa CITES.
Alisema Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kwa kufanya doria ndani na nje ya mapori ya akiba kwa siku 100,000 na kwamba vikosi vya ulinzi vitaimarishwa. “Wizara itakamilisha Kanuni ya Kikosi cha Ulinzi wa Wanyamapori na itaandaa Kanuni mpya mbili. Kanuni ya kwanza ni Usimamizi wa Maeneo ya Ushoroba, Mazalia na Mtawanyiko wa Wanyamapori na ya pili ni Kanuni za Usimamizi Wanyamapori wa Taifa,” alisema Kagasheki. Aprili 30 mwaka huu Kambi ya Upinzani Bungeni ilitoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahaman Kinana ikidai kuwa anajihusisha na mtandao wa ujangili nchini.
Akiwasilisha maoni ya upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013/14, msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mchungaji Peter Msigwa alisema vitendo vya ujangili nchini vimekuwa vikilitia aibu taifa kwenye jumuiya za kimataifa. Kauli hiyo ilileta mvutano wa maneno miongoni mwa wabunge huku baadhi yao wakihaha kumsafisha Kinana, ambaye hata hivyo baadaye alikana kuhusika na biashara ya kuuza pembe za ndovu. CITES wanasema zaidi ya ndovu 17,000 waliuawa barani Afrika mwaka 2011. Kutokana na mauaji hayo, CITES wanasema wametoa onyo la mwisho kwa nchi husika wakizitaka kusimamisha haraka biashara ya pembe za ndovu. Na iwapo hazitaachana na biashara hiyo hadi kufikia Julai mwakani, watalazimika kuweka vikwazo vya kibiashara.
Ingawa baadhi ya wanaharakati wanaotetea haki za wanyama wanaona kuwa CITES wameshindwa kuwaokoa tembo wa Afrika, Katibu Mkuu wa CITES, John Scanlon anasema: “Muda wa mwisho tuliouweka tutausimamia, nchi itakayokiuka tutaichukulia hatua kali kwa mujibu wa mkataba, tunaweza kuiwekea vikwazo vya kibiashara,” anasema Scanlon. Katika mkutano wa CITES uliofanyika Doha mwaka 2010, Taasisi ya Uchunguzi wa Mazingira (EIA), ilitoa ushahidi wake ulioonyesha namna rushwa inavyochochea ujangili nchini Tanzania. Zaidi ya ndovu 30,000 walitoweka kati ya mwaka 2006 na 2009, wengi wakidaiwa kuuzwa katika masoko barani Asia.
Pia, ripoti hiyo ilibainisha kuwa kati ya tani 12 za pembe zilizokamatwa barani Asia mwaka 2009, vipimo vya vinasaba (DNA) vilionyesha kuwa nyingi zilitoka katika pori la akiba la Selous. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa ya pembe za ndovu. Serikali iliomba kibali kutoka CITES cha kuuza tani 101 za pembe, lakini iligonga mwamba baada ya kushindwa kutimiza baadhi ya masharti. Inakadiriwa kuwa mwaka 1950 kulikuwa na ndovu milioni 5 Afrika, lakini ilipofika mwaka 1989 idadi ya wanyama hao ilipungua hadi kufikia 450,000 kutokana na shughuli za ujangili. Sababu hii ndiyo iliyoifanya CITES kumweka ndovu katika nafasi ya kwanza kwenye orodha ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani.
Source: Eliona G. (May 2013).Tanzania yatajwa kuwa hatari kwa ujangili. Dar es salaam. Retrieved from Mwananchi

No comments:
Post a Comment