MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) na watu wengine 60 wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya vurugu na uchochezi. Msigwa anadaiwa kuwachochea wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) kutoondoka eneo walilozuiwa kufanya biashara. Msigwa alikamatwa jana mkoani hapa baada ya kutokea kwa vurugu za wamachinga waliokuwa wakipinga kuhamishwa katika eneo la Mashine Tatu na kupelekwa Mlandege. Mbunge huyo anadaiwa kuwahamasisha wamachinga hao kutoondoka eneo la Mashine Tatu walikokuwa wakifanyia biashara.
Vurugu hizo zilianza jana asubuhi baada ya wamachinga hao kufika eneo la tukio ambako kulikuwa na idadi kubwa ya polisi waliokuwa wakililinda baada ya kuwepo kwa taarifa za kurejea kwao. Wamachinga hao inadaiwa walihamasishwa na Mchungaji Msigwa katika mikutano yake ya hadhara kurejea kwenye eneo hilo kwa madai wasikubali kupelekwa eneo la Mlandege. Wafanyabiashara hao walianza kujikusanya kwenye vikundi vidogo vidogo kuanzia saa 12 asubuhi bila kupanga biadhaa zao wakidai wanamsubiri Msigwa aliyewaahidi kuungana nao kupinga kuhamishwa. Walidai kuwa Msigwa aliwaahidi naye atakuwa mmachinga mpya katika eneo hilo walilofanya biashara kwa kipindi kirefu kabla ya kuhamishwa na Halmashauri ya Manisapaa ya Iringa.
Msigwa alifika eneo la tukio majira ya saa tatu asubuhi akiwa na gari lilikokota tela la kuhifadhia mizigo ambapo aliwataka wamachinga kupambana kutetea haki yao. Hata hivyo, Msigwa aliondoka eneo la tukio na polisi walianza kuwatawanya wamachinga hao kwa kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha yaliyokuwa yakitoka kwenye gari maalumu. Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi baada ya wamachinga kuwarushiana mawe na kuchoma moto matairi waliyoyaweka barabarani kama vizuizi. Katika vurugu hizo mawe yaliyokuwa yakirushwa na wamachinga yalivunja vioo vya gari la Kikosi cha Zimamoto na kuharibu mali mbalimbali. Vurugu hizo zilizodumu kwa takriban saa sita ziliufanya mji wa Iringa kuzizima na watu kushindwa kufanya shughuli zao.
Msigwa alivyokamatwa
Baada ya kuondoka eneo la vurugu, Msigwa alikwenda Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa kulikokuwa na harambee ya kuchangia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa. Katika harambee hiyo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, na viongozi hao walishiriki kikamilifu shughuli hiyo. Baada ya kumalizika kwa harambee hiyo, polisi walimkamata Mchungaji Msigwa kwa madai ya kuhusika na uchochezi uliosababisha vurugu kubwa. Hata hivyo, kabla ya kukamatwa, Msigwa aliliambia Tanzania Daima kuwa haogopi kukamatwa, na ataendelea na msimamo wa kuwataka wamachinga wasihame eneo la Mashine Tatu.
Polisi wazungumza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alithibitisha kuwakamata watu zaidi ya 60 akiwemo Mchungaji Msigwa kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo. Alibainisha kuwa jeshi hilo linaendelea na jitihada za kuwasaka watu wengine waliohusika na linatarajia kuwafikisha mahakamani leo.
Source: Godwin F. (May 2013). Mbunge CHADEMA akamatwa. Iringa. Retrieved from Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment