Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, May 17, 2013

Polisi wazidisha ngonjera kuumizwa kwa Kibanda


Jeshi la Polisi limekwepa kuwajibika kueleza kuhusiana na mchakato wa uchunguzi wa tukio la kutekwa, kupigwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda. Aprili mwaka huu Jeshi hilo liliahidi kwamba lingetoa taarifa kwa umma kuhusiana na uchunguzi wa timu iliyoundwa kuchunguza tukio hilo. Hata hivyo, maofisa waandamizi wameshindwa kutekeleza ahadi hiyo na kuunyima umma haki ya kujua waliotenda uhalifu huo wa kinyama na hatua zilizochukuliwa dhidi yao. Mara kadhaa, Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, wamekuwa wakikwepa kulizungumzia suala hilo na kuahidi kuwa taarifa zitatolewa baadaye.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited ambayo ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na The African, alivamiwa na watu hao, wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu. Jana NIPASHE iliwasiliana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, Kamishna Robert Manumba, ambaye alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa hakuwapo wakati kikosi kazi kilipoundwa na kuelekeza aulizwe aliyekiunda. “Tume hiyo iliundwa lini?” alihoji na kuendelea: “Aulizwe aliyeunda atakuwa na majibu sahihi, mimi siwezi kueleza lolote.” Wakati kikosi hicho kinaundwa, DCI Manumba alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu na Mngulu ndiye aliyekuwa anakainu nafasi yake.

Kabla ya kuwasiliana na Manumba, NIPASHE liliwasiliana na Mngulu, ambaye alimwelekeza mwandishi kumtafuta Manumba kwa maelezo kuwa amesharejea ofisini. Baadaye NIPASHE liliwasiliana na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ambaye ndiye aliyeunda kikosi hicho. Hata hivyo, Kova alikwepa kulizungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa liko juu ya uwezo wake na kufafanua kuwa lilishapelekwa kwa DCI. “Siwezi kueleza lolote kwenye simu ila naomba nikuelimishe kuwa suala hilo liko kwa DCI, ila uje ofisini kwangu kesho (leo) asubuhi nikueleze vizuri,” alisema Kova.

Aprili 8, mwaka huu, Mngulu alisema ripoti ya upelelezi wa timu maalum ya wapelelezi itatolewa kati ya Aprili 15, 16 au 17, mwaka huu. Alisema ripoti hiyo ndiyo itakayobainisha kama kuna watu wanaostahili kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na sakata hilo au la. Alisema miongoni mwa watu waliohojiwa katika upelelezi uliofanywa na timu hiyo, ni pamoja na Kibanda mwenyewe.  Akijibu swali kwa nini upelelezi wa sakata hilo umechukua muda mrefu, Mngulu alisema katika mahojianao na Redio One, hakuna muda maalum uliowekwa na sheria wa kupeleleza jambo.

Mngulu alisema hata katika kumsaka Osama bin Laden ilichukua zaidi ya miaka 10 ndipo akanaswa.  Aliwataka Watanzania kuwa na subira hadi upelelezi huo utakapokamilika na ripoti hiyo kutolewa. Katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kumkata kidole, kumjeruhi kwa kitu kizito kichwani na kumharibu jicho la kushoto. Hali hiyo ilisababisha Kibanda kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na baadaye katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.   Kufuatia tukio hilo, Senso alikaririwa akisema Mkuu wa Jeshi hilo nchini, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ameunda timu ya wapelelezi wazoefu kufanya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika katika uhalifu huo na kuwatia mbaroni.

Timu hiyo ya makachero wanne kutoka makao makuu ya polisi iliunganisha nguvu na makachero wa Jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Hata hivyo, ikiwa leo ni siku 73, hakuna taarifa yoyote ya maana ya polisi, siyo ya kumatwa kwa yeyote wala kuonyesha walau mwelekeo wa uchunguzi huo, jambo linalotafsiriwa kuwa ni kulipuuza. Hisia hizi zinatiwa nguvu hata na kauli za viongozi waandamizi wa serikali akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, bungeni kwamba Kibanda ni nani hadi aumizwe na vyombo vya usalama. Wasira alitoa maneno hayo yenye ukakasi alipokuwa akijibu hoja mbalimbali kuhusu mjadala wa bajeti ya ofisi ya rais na ofisi zilizo chini yake.


Source: Kitomory S. (May 2013). Polisi wazidisha ngonjera kuumizwa kwa Kibanda. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments: