Pori
tengefu la Loliondo ni eneo lililopo mashariki mwa hifadhi ya Taifa ya
Serengeti. Eneo hili linajumuisha vijiji ambavyo vinatambulika kisheria tangu
wakati wa ukoloni na kulindwa kisheria na sheria ya ardhi ya vijiji Na. 5 ya
mwaka 1999 na sheria ya Serikali za Mitaa, Tawala za Wilaya namba 7 ya Mwaka
1982. Vijiji hivyo ni Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri, Olorien, Maaloni,
Arash, Malambo na Piyaya. Eneo hili pia limekuwa likijulikana kama pori
tengefu la Loliondo kulingana na sheria ya wanyama pori ya mwaka 1974 na sheria
ya wanayma pori namba 5 ya mwaka 2009 ambazo zote hazija badilisha hadhi ya
vijiji vilivyopo wala haki za ardhi za wenyeji wa vijiji husika wala
hazihamishi haki hizo kwenda kwa mamlaka nyingine yoyote ikiwemo wizara ya
malisaili na Utalii.
Itambulike kwamba hadhi ya pori tengefu haingilii hadhi ya
umiliki wa ardhi bali inatoa mamlaka kwa mkurugenzi wa wanyama pori kusimamia
wanyama pori waliopo katika eneo hilo pamoja na kutoa mamlaka ya kugawa vitalu
vya uwindaji kwa makampuni ya uwindaji bila kuingilia haki za ardhi kwa wakazi
wa maeneo husika. Aina hii ya mgawanyo, usimamizi na matumizi ya ardhi na
rasilimali zake imekuwa ndicho kiini kikubwa cha mgongano wa maslahi na
migogoro ya mara kwa mara katika eneo hili na maeneo mengine yenye sifa ya aina
yake.
Mwaka
1992 serikali ilimruhusu mwana mfalme Brigadia Mohamad Al-Ali kupitia kampuni
ya Otterlo Business Corporation (OBC) kuwinda ndani ya vijiji vya tarafa
vya Loliondo na Sale. Ruhusa hiyo haikufuta haki na uhalali wa wananchi wa
kuendelea kuwepo na kutumia ardhi yao kulingana na sheria ya Ardhi ya vijiji ya
mwaka 1999 na sheria ya serikali za mitaa, tawala za wilaya.
Tangu
wakati huo kumekuwepo na upotoshaji mkubwa kuhusu uhalali wa umiliki wa eneo la
Loliondo ambao umefanywa na serikali kwa lengo la kuilinda kampuni ya uwindaji
ya OBC. Upotoshaji huo umekuwa ukifanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii na
uongozi wa Mkoa wa Arusha na wilaya ya Ngorongoro na kupelekea wananchi
kutolewa kwa nguvu katika maeneo hayo kwa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na
madai kuwa wananchi wa Loliondo ni
Wakenya,
waharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa watu na mifugo. Upotoshaji huu
umekuwa na lengo la kuwaahadaa umma wa Watanzania na ulimwengu kwamba
eneo lote la Loliondo ni eneo la hifadhi pekee na siyo ardhi ya vijiji na
kwamba wananchi ni wavamizi wa eneo hilo jambo ambalo siyo sahihi wala halina
uhalali wowote wa kisheria.
Kutokana
na nia ya serikali kuwaondoa wananchi katika maeneo yao ya vijiji vyao
kumekuwepo na harakati mbalimbali za wizara kutumia mbinu mbalimbali za kumega
na kupokonya kilomita za mraba 1500 ya ardhi ya vijiji na kuikabidhi kampuni ya
OBC kwa kisingizio cha kwamba wanawagawia wananchi sehemu ya pori tengefu la
Loliondo. Jambo hili siyo sahihi kwani ardhi hiyo ni ardhi ya vijiji husika.
Tarehe
21 Marchi 2013 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Balozi Khamisi Khagasheki,
alitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari. Taarifa hiyo ina kichwa cha
habari "Wizara ya Maliasili kurekebisha mipaka na ukubwa wa
eneo la Pori tengefu la Loliondo kutoka Kilometa za mraba 4,000 hadi 1500".
Katika taarifa hiyo Waziri ametangazia umma kwamba serikali imeamua kupunguza
ukubwa wa eneo hilo ili kutatua migogoro iliyopo katika eneo hilo, kunusuru
ikolojia ya hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na Pori tengefu la Loliondo.
Vilevile
katika tamko lake Waziri alielezea sababu zingine kwamba ni kulinda masalia ya
wanyama pori, mapito na vyazo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi kwa
manufaa ya wananchi wenyewe na taifa kwa ujumla. Pia waziri alizungumzia kwamba
wananchi wataweza kuanzisha hifadhi za wanyama pori (WMA) katika ardhi
itakayobaki kuwa ardhi ya vijiji.
Kutokana
na tamko hili la Mh. Waziri , SISI mashirika ya kiraia
yanayojihusisha na utetezi wa Haki za Ardhi na Haki za Binandamu na ambao
tumekuwa tukifuatilia suala hili kwa karibu sana tunapenda kujulisha umma wa
watanzania kama ifuatavyo;
1.Kwamba
siyo kweli serikali inawaachia wananchi ardhi yenye ukubwa wa kilomita za mraba
2500 kwani ardhi hiyo ni ardhi ya vijiji iliyopo ndani ya mipaka ya vijiji na
kinachofanyika ni kuwapokonya wananchi ardhi iliopo ndani ya mipaka ya vijiji
vyao yenye ukubwa wa kilomita za maraba 1500 na kumpatia mwekezaji wa OBC.
2.Hakuna
eneo lolote alilopewa OBC kama waziri alivyo potosha katika ukurasa wa pili wa
taarifa yake kwa umma kwamba "serikali ipo tayari
kuangalia upya eneo kubwa alilopewa OBC na ikibidi litapunguzwa…"
Ukweli ni kwamba OBC iko katika eneo la pori tengefu la Loliondo ndani ya
vijiji husika kwa kibali cha kuwinda tu na sio umiliki wa ardhi na
hawakuwahi kupewa ardhi anayodai Mh Waziri kwamba wamepewa. Vilevile
waziri anatuaminisha kwamba mgeni amemilikishwa ardhi ya Loliondo jambo ambalo
ni kinyume cha sheria ya ardhi na sheria ya uwekezaji inyokataza wageni
kumiliki ardhi isipokuwa kwa kuwekeza tu.
3.Kwamba
uamuzi wa serikali wa kugawa eneo la vijiji na kulifanya kuwa pori tengefu
unachochea mgogoro uliopo. Kusema kuwa serikali inawagawia wananchi eneo
watakaloikalia ni upotoshaji kwani wananchi ndio wenye haki ya
kugawa eneo lolote ndani ya mipaka ya vijiji vyao kwa matumizi
watakayoamua wao. Serikali kudai kuwagawia wananchi eneo ambalo tayari ni
la kwao inatosha kuchochea mgogoro katika eneo hilo na ni dalili ya serikali
kutaka kutumia mabavu kama ilivyotokea mwaka 2009.
4.Kwamba
siyo kweli kuwa serikali ina lengo la kuinusuru ikologia ya hifadhi ya Serengeti
ila ina lengo la kumpatia mwekezaji (OBC) eneo la kuwindia bila kuzingatia
sheria na matakwa ya wananchi wa vijiji husika. Hili pia halina ukweli wowote
kwani serikali wasingeruhusu uwindaji ufanyike kama wangekuwa na uchungu wa
kuwalinda wanyama pamoja na ikolojia hiyo. Hili linadhihirishwa na wanyama
wenyewe kukimbilia karibu na maboma ya wafugaji ili kuwakimbia wawindaji
wa OBC kwani wanyama pori wanajisikia wako salama zaidi wanapokuwa karibu na
mifugo kuliko kuwa karibu na wawindaji.
5.Siyo
kweli kwamba serikali inataka kulinda vyanzo vya maji kama anavyodai Mh
Waziri. Hili linadhihirishwa na ujenzi wa kambi ya kudumu ya OBC kwenye
chanzo cha mto wa Olasae linalotegemewa na wanyamapori pamoja na wanakijiji wa
kijiji cha Soit Sambu , Arash,Ololosokwa na Kirtalo. Ujenzi huu umefanywa na
kampuni ya OBC ndani ya mita 10 kutoka chanzo cha maji kinyume cha
sheria.
6.Taarifa
ya Mh. Waziri haikuzingatia suala la utawala bora wala sheria ya wanyama pori
ya mwaka 2009 kifungu cha 16(5) ikinachomtaka kwamba hakuna ardhi ya kijiji
itakayoingizwa ndani ya pori tengefu. Kipengele hiki kinasomeka kama
ifuatavyo; 16(5) "For the Purposes of subsection (4), the
Minister shall ensure that no land faIling under the village land is included
in the game controlled areas." Kipengele cha 16(6) "Subject to
subsection (4), the Minister shall, in consultation with the relevant
authorities, make regulations prescribing the manners in which sustainable
management of game controlled areas shall be achieved."
Kutokana
na maelezo yetu hapo juu sisi mashirika ya hiari tunaitaka serikali
kutekeleza yafuatayo;
1.Serikali
iache mara moja mpango wake wa kugawa ardhi ya wananchi kwa manufaa ya
mwekezaji kwa kisingizio cha manufaa ya umma badala yake itambuwe ardhi yote ya
Loliondo kama ardhi ya vijiji na kuwaachia vijiji kujipangia matumizi yao ya
ardhi kwa njia shirikishi na mujibu wa sheria za ardhi.
2.Kuacha
mara moja kupotosha umma kwamba ardhi hiyo siyo ya vijiji na izingatie sheria
kwa kuvipa vijiji haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe kwa kutumia sheria
zilizopo za ardhi na za serikali za mitaa.
3.Serikali
iweke bayana kwa umma nia yake ya kuchukua ardhi hii kwamba ni kwa
ajili ya mwekezaji wa OBC badala ya kisingizio cha uhifadhi wa mazingira na sio
vinginevyo.
4.Serikali
iache mara moja vitisho kwa wananchi wa Loliondo na wawakilishi wao,
wanaharakati, mashirika na waandishi wa habari wanaofuatilia mgogoro huu.
Serikali kuendelea kutishia makundi haya inakiuka haki ya kikatiba ya kupata
habari na kuzuia jamii kuelimishwa juu ya haki zao za kikatiba na kisheria kwa
manufaa yao wenyewe na taifa kwa ujumla. Kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya
kupata taarifa na kutoa maoni kama inavyolindwa na katiba ya Tanzania na
mikataba ya Kimataifa ambayo serikali imeridhia.
5.Serikali
iache mara moja kudharau na kuingilia utendaji wa mhimili wa mahakama kwa
kuacha kuingilia suala la Loliondo kwa kuzingatia kuwa tayari kuna kesi ya
kikatiba (MISC CIVIL CAUSE NO 15/2010) iliyofunguliwa katika mahakama kuu ya Tanzania
Kanda ya Arusha ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii na mwekezaji wa OBC
ni miongoni mwa wa walalamikiwa.
6.Serikali
iache mara moja visingizio kwamba mgogoro wa Loliondo unasababishwa na
wanaharakati na mashirika ya nje kwani yenyewe inatambua uwepo wa mgogoro huo
unasababishwa na maamuzi ya serikali ya kugawa ardhi ya wananchi bila
kuwashirikisha kwa kuangalia upande mmoja wa manufaa kwa wawekezaji tu bila
kuangalia athari kwa wananchi.
7.Serikali
iache matumizi mabaya ya vyombo vya usalama hasa jeshi la polisi ambalo
hutumiwa kuwaondoa wananchi katika makazi yao kwa nguvu huku wakisababisha
athari kubwa kwa wasiojiweza, wanawake na watoto.
TAMKO
HILI LIMETOLEWA LEO TAREHE 4 APRILI 2013 NA MASHIRIKA AMBAYO NI;
1.PINGOs
Forum
2.Tanzania
Land Alliance- TALA
3.Haki
Ardhi
4.Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu- LHRC
5.Tanzania
Human Rights Defenders
6.Tanzania
Gender Network Program (TGNP)
7.Tanzania
Natural Resource Forum –TNRF
8.Cords
9.Ujamaa
Community Resource Team- CRT
10. Pastoralists Women Council –PWC
11. Ngorongoro NGOs Network –NGONET
12. Tanzania Pastoralists Community Forum-TPCF
13. OSEREMI
No comments:
Post a Comment