- Wakusudia kumshitaki bungeni ajiuzulu
- Yaipa maelekezo mazito Kambi ya upinzani
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kitawasilisha bungeni azimio au hoja zote ili kuhakikisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mawaziri wake wanawajibishwa kutokana na matokeo mabovu ya kidato nne mwaka jana. Itakumbukwa katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, zaidi ya asilimia 94 ya wanafunzi wote walifeli. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, nje ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA inayoendelea na vikao vyake vya kawaida, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika alisema chama hicho kitatumia kila aina ya njia inayowezekana kwa mujibu wa Katiba, kuhakikisha Waziri Mkuu na mawaziri wake wanawajibika. “Chama kimeamua kulivalia njuga zaidi suala la matokeo mabovu ya kidato cha nne, kwa kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mawaziri wake wawajibike, haiwezekani asilimia 94 ya wanafunzi wafeli, alafu tuache suala hili hivi hivi. "Kamati Kuu imepokea na kujadili kwa uzito mkubwa na imesikitishwa na matokeo haya, hali hii ni sawa na msiba kwa taifa,” alisema Mnyika.
Mbali ya uamuzi huo, chama hicho pia kimeiagiza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa kuhakikisha maelezo na vielelezo kuhusu madai ya ufisadi wa Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kutoa zabuni ya mabilioni ya fedha kwa kampuni ya CCM kinyume cha sheria, nalo linawasilishwa bungeni na wahusika wachukuliwe hatua. “Hadi jioni hii, tunaendelea kujadili hali ya kisiasa kwa uzito mkubwa, kutokana na matukio mbalimbali yanayoendelea nchini, hata ninyi ni mashahidi wa hali hii, naamini tukifika mwisho wa mkutano tutawajulisha,” alisema Mnyika. "Chama kimeagiza Kambi ya Upinzani Bungeni, kulichukua jambo hili kwa uzito mkubwa na kilipeleka bungeni ili viongozi wa ngazi za juu wa Serikali wawajibike. “Kamati Kuu, imejadili suala hili ikielewa wazi kuna tume imeundwa na Serikali kutafuta chanzo cha matokeo haya mabaya, lakini tukiwa kama chama pia tuna nafasi yetu ya kulishughulikia,” alisema Mnyika.
Alisema ajenda nyingine ambayo imefikiwa, ni kwamba chama hicho kitaitisha maandamano makubwa ya kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ajiuzulu," alisema Mnyika. “Tumejadili jambo kwa kina mno na tumebaini namna ambavyo Serikali imekuwa ikitafuta visingizio vya kutotoa majibu au kuwajibisha mawaziri wake na kuunda tume ambazo ripoti zake zimekuwa hazitoi majibu ya msingi,” alisema Mnyika.
Kuhusu taratibu za maandamano hayo, alisema mazungumzo yanaendelea kati ya chama hicho na viongozi wa jeshi la polisi.
Ufisadi
Akizungumzia kauli zilizotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye juu ya madai yaliyotolewa juzi na CHADEMA, kikimtuhumu Waziri Mwakyembe kuisaidia Kampuni ya Jitegemee Trading Company, inayomilikiwa na CCM, zabuni ya Sh bilioni 10 za kujenga maegesho ya magari makubwa, makontena na malori, kinyume cha sheria, Mnyika alisema CHADEMA wataendelea kupiga kelele kuhusu suala hilo. "Tunawashukuru kweli CCM, wameingia kichwa kichwa katika suala hili, Watanzania wanakumbuka hata wakati ule tulipotoa orodha ya mafisadi, tukawataja majina, hawakukanusha.
"Sisi tunajua tunachokisema na kukifanya, suala hili nalo kwa kuwa Bunge la Bajeti linaanza wiki ijayo, tutakamatana huko huko,” alisema. "Bungeni tutawasilisha vielelezo na maelezo yote kuhusu ufisadi uliosimamiwa na Waziri Mwakyembe kupitia wizara yake, kuipatia zabuni Kampuni ya Jitegemee kinyume cha sheria," alisema Mnyika. Alisema CHADEMA, inazungumza suala hilo kwa vielelezo si maneno pekee tu.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliunda tume ya kuchunguza matokeo ya kidato cha nne, ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Sifuni Mchome. Katika taarifa ya awali ya tume hiyo iliyoitoa, ilisema imebaini sababu zilizochangia matokeo hayo kuwa mabaya ni upungufu wa walimu na matumizi ya vitabu vilivyopitwa na wakati. Sababu nyingine, ni usimamizi dhaifu katika sekta ya elimu, pamoja na uhaba wa bajeti, sababu ambazo zimezoeleka na zilikuwa zikijulikana kabla ya tume hiyo kuundwa. Utafiti huo, ulihusu Jiji la Dar es Salaam.
Source: Mtanzania. (march 2013). CHADEMA wamvaa Pinda. Retrieved from Mtanzania

No comments:
Post a Comment