Nimetafutwa na uongozi wa JamiiForums ili
kutoa maelezo kuhusu barua iliyowekwa jukwaani inayoonyesha kuwa ndani ya chama
kuna kutoelewana kuhusiana na msimamo juu ya kesi inayomkabili mmoja wa
viongozi waandamizi wa chama Ndg. Wilfred Lwakatare, Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa chama.
Maelezo yangu ni kama ifuatavyo:
1. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa chama
mnamo tarehe 15 Machi 2013 kutaka chama kifanye uchunguzi wake wa ndani
kuhusiana na ukweli wa video iliyowekwa kwenye mitandao inayoonyesha kuwa
Kiongozi wetu mwandamizi anapanga mipango ya kumdhuru Mhariri wa moja ya
magazeti hapa nchini . Sikuamini kabisa mambo yale na hivyo kutoa
ushauri kwa chama kwamba tufanye uchunguzi wetu wa ndani ili kujiridhisha.
Uchunguzi wa ndani ungetufanya kuweka mikakati wa namna bora zaidi ya kulinda
chama dhidi ya njama zozote, za ndani au za nje ya chama.
2. Mapendekezo yangu ndani ya chama kamwe
hayakulenga kumtosa ndugu Lwakatare wakati huu anakabiliwa na changamoto hii
bali yalilenga kuhakikisha kuwa wakati tunamlinda na kumtetea ili haki
itendeke, lazima tuhakikishe kuwa chama hakitaathirika na sakata hili kwa namna
yeyote ile. Ni jukumu letu kuhakikisha sura (image) ya chama inabakia salama
maana hatujui mikakati (game plan) ya maadui zetu kisiasa hasa baada ya kauli
zao kwamba chama kitakufa kabla ya 2015 ambayo imerudiwa rudiwa sana. Ni lazima
kutilia shaka (doubt) kila linalotokea sasa kwa kulipima kwa jicho la mbele
zaidi. Ikumbukwe maneno ya Mwenyekiti wetu “Mwenyekiti Freeman Mbowe anataka
ikithibitika kuwa Lwakatare alishiriki kurekodi mkanda huo iwe kwa kurubuniwa,
‘kushikishwa’ au kuingizwa mkenge, itamlazimu kuwajibika kwa kosa la kukosa
umakini” (Gazeti la Jamhuri).
3. Barua ile ya tarehe 15 Machi 2013 ilikuwa ni
ya ndani ya chama, haikuwa ya kiofisi bali ya Zitto Kabwe kwa chama,
ilisainiwa na haikukusudiwa kuwa ‘public’. Nimeshangazwa sana kusikia na
baadaye kuona barua yenye maudhui kama yale yale ya barua yangu kwa Katibu Mkuu
imewekwa mtandaoni. Barua imewekwa masaa machache baada ya kikao cha Kamati Kuu
kwisha ambapo tuliweka msimamo wa pamoja wa chama juu ya namna bora ya
kushughulikia suala la Lwakatare kama chama. Wakati mweka barua anadai kuwa
kulikuwa na mgawanyiko katika kikao, ukweli ni kwamba ajenda hiyo haikuwa na
mjadala wenye mgawanyiko kabisa na msimamo wa chama ulipatikana kwa mwafaka
bila mgawanyiko. Ni dhahiri kuwa maadui zetu walitaraji mgawanyiko na baada ya
kushindwa sasa wanatengeneza mgawanyiko huo kwa kusambaza uwongo wenye
uzandiki.
4. Baada ya kufanya uchunguzi mdogo nimegundua
kuwa ID iliyoweka video ya Lwakatare mtandaoni na ID iliyoweka barua hii
mtandaoni ni IDs za mtu mmoja. ‘Coincidence’ ya namna hii inashangaza na
kushtusha, lakini inatuambia jambo moja kubwa ‘kwamba kuna kirusi ndani ya
chama kilicho karibu sana na viongozi wa chama chenye kazi moja tu, yani
kuonyesha kuwa CHADEMA hapako shwari, kuna migogoro na hatimaye kusambaratisha
chama’. Kirusi hiki lazima kina nafasi andamizi au kipo karibu sana na viongozi
waandamizi. Inawezekana kabisa kirusi hiki kinahusika na suala zima la
Lwakatare katika kupanga, kuendesha na kutekeleza mpango mzima. Maswali kama
‘kwanini Dennis Msacky na Zitto ndani ya Video ya ‘Lwakatare’ lazima sasa
yaanze kutafutiwa majawabu.
5. Natoa wito tena kwa viongozi na wanachama wa
CHADEMA kwamba, huu ni wakati wa kuwa na umoja na mshikamano kuliko wakati
wowote ule katika uhai wa chama chetu. Chama cha Mapinduzi kitatumia njia zote
kutugawa, kutugombanisha na kupenyeza chuki miongoni mwetu katika juhudi za wao
kubakia madarakani. Umakini wa Kiongozi huonekana wakati wa changamoto kama
hizi!
6. Msimamo wa chama umetolewa na Kamati Kuu
iliyomaliza vikao vyake jana siku ya ijumaa tarehe 5 Aprili 2013. Huo ndio
msimamo wangu pia! Kesi ya Lwakatare ipo mahakamani, chama kimeonyesha dhahiri
kumwamini Jaji aliyekabidhiwa kesi hii, sasa tuache mahakama ifanye kazi yake na
tusubiri hukumu. Msemaji wa chama kuhusu suala hili ni ndugu Tundu Lissu na
amekuwa akitoa ufafanuzi kila inapohitajika.
Asanteni

No comments:
Post a Comment