Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, April 7, 2013

Wabunge CCM, CHADEMA kuhoji mikataba


SAKATA la tuhuma za ufisadi zilizoibuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limeingia katika hatua mpya baada ya baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupania kutaka maelezo bungeni kuhusu mradi wa bandari kavu unaotarajiwa kufanywa kwa ubia kati ya CCM na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Baadhi ya wabunge hao waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili wamesema CCM ni chama kinachopinga ufisadi, na kwamba kuhusishwa nao kwa namna yoyote ni doa ambalo lazima lisafishwe. “Kama kweli tunataka kupata ushawishi na uungwaji mkono na umma, lazima tujisahihishe na kama kuna uchafu ndani yetu tusiufumbie macho hata kama anayehusika ana ‘mapembe’, na kwa hili utakuta kuna wachache wanaotumia CCM kujinufaisha.

“Sasa tukijifanya tunashindana na CHADEMA na kuwatetea wanaotuchafua, hatutakuwa tunakiimarisha chama bali kukiangamiza. Nadhani wenzetu hawajamuelewa mwenyekiti wetu (Rais Jakaya Kikwete) alipozungumzia kujivua gamba. Huku ndiko kujivua gamba na Mwalimu Nyerere aliwahi hata kuandika kitabu akitaka tujisahihishe,” alisema mbunge mmoja wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa. Kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu zilizo wazi, mbunge huyo akiwa na mwenzake kutoka mkoa mmojawapo wa katikati ya Tanzania, alisema: “Asili ya CCM ni chama cha wanyonge, lakini kwa sasa tunajisahau na kukigeuza kuwa chama cha matajiri wachache na viongozi.

“Lazima tujisahihishe. Kuna wanaotumia jina la chama kujinufaisha kama ilivyokuwa kwa watuhumiwa wa EPA ambao Serikali ya CCM iliwashitaki. Na hawa wachache wanaotumia Kampuni ya Jitegemee kujinufaisha, lazima tupate maelezo na kuwachukulia hatua. Tukitetea uchafu tunawapa maadui zetu nafasi ya kutamba wakati hawana mpya.” Tuhuma hizo ziliibuliwa hadharani na CHADEMA ambao walisema kuna ufisadi katika ununuzi wa kiwanja kilichokuwa kinamilikiwa na iliyokua kampuni ya CCM ya Sukita na baadaye kuwa maegesho ya malori kwa ubia na kampuni nyingine ya CCM ya Jitegemee Trading. Kauli hiyo ilipingwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alibeza na kuonyesha kwamba CHADEMA hawakuwa na hoja na hawajafanya utafiti. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika juzi aliibuka na kusema kwamba CCM haijajibu hoja za msingi, na kwamba suala hilo ni miongoni mwa mambo ambayo watayawasilisha bungeni kutaka maelezo.
“Kwanini kampuni ipewe tenda ya kujenga kwenye kiwanja chake yenyewe? Pia ni kwanini kiwanja walichotoa Wilaya ya Temeke hakijachukuliwa na Bandari matokeo yake kinachukuliwa cha mabondeni? Pia CCM haijaeleza uhusiano wa wakurugenzi wa kampuni hiyo na maslahi yao na Ikulu,” alisema Mnyika.
Tayari suala hilo limeelezwa kutaka kugeuzwa na kuwa ni vita ya kisiasa ya makundi hasimu ndani ya CCM yenye malengo ya kuwania urais wa mwaka 2015, baada ya kundi moja kutuhumiwa kuitumia CHADEMA kushambulia kundi lingine. Habari za ndani ya TPA ambao ndio waliotenga sh bil. 10 kununua eneo hilo la CCM bila kufuata sheria ya manunuzi zinaeleza kwamba baadhi ya watendaji wanataka mradi huo uchunguzwe upya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya TPA, watumishi hao wamesema kwamba mradi huo wa CCM haupo katika mpango wa miaka mitano wa mamlaka hiyo wala mpango mkuu wa hadi mwaka 2025 na kushangaa ulikoanzia. Mapema wiki hii CHADEMA walitoa tamko la kukemea ufisadi ambao unataka kufanyika kwa kuhusisha moja ya mashirika makubwa ya umma nchini, TPA na Kampuni ya Jitegemee Trading inayomilikiwa na CCM. Siku moja baada ya tuhuma hizo kutolewa, CCM kupitia kwa katibu mwenezi wake, Nape ilitoka na tamko na kukanusha kuhusika kwake, huku ikiri kumiliki Kampuni ya Jitegemee Trading. Nape alikwenda mbali zaidi na kuuambia umma kwamba walichofanya Wizara ya Uchukuzi kupitia TPA ni kupeleka "barua" ya maombi kwa CCM (Jitegemee Trading) ya kusudio la kuendeleza kwa njia ya ubia eneo hilo lililoko karibu na Mto Msimbazi lililokuwa linamilikiwa na Sukita.

Kwenye bajeti iliyopita ya TPA iliyopitishwa na bodi ya wakurugenzi katika kikao chake kilichokaa wiki mbili zilizopita chini ya Kaimu Mkurugenzi, Madeni Kipande, pamoja na mambo mengine mradi huu wa ubia uliwekwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/14 na kutengewa sh bil. 10 kama ushiriki wa TPA kwenye mradi huo. Tanzania Daima Jumapili imeiona nakala ya "Capital Budget" ya miradi yote inayotarajiwa kufanywa katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha na maelezo ya kina kuhusiana na mradi huu wa ubia kati ya TPA na CCM ukiwa mmojawapo. Taarifa za ndani ya TPA zinasema mradi huu haujafanyiwa upembuzi yakinifu ili kujua kama kuna faida au hasara mbali ya kushinikizwa na wakubwa. Zinasema kwamba hata kwenye kikao cha uongozi haukujadiliwa kwa kina kabla ya kupelekwa kwenye bodi ila Kaimu Mkurugenzi Mkuu Kipande aliwatuma watu wa Idara ya Uhandisi kwenda kukagua eneo hilo.

Source: Tanzania Daima. (March 2013). Wabunge CCM, CHADEMA kuhoji mikataba. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: