Rais Jakaya Kikwete akiagana na Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa (wa tatu kushoto) baada ya mkutano wa vyama vya siasa vyenye wabunge mjini Dodoma jana, Wengine kutoka kushoto ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, John Cheyo wa UDP na Phillip Mangula wa CCM. Picha na Ikulu.
Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana waligoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuruhusu wajumbe wao kurejea katika Bunge Maalumu la Katiba, walipokutana katika kikao cha kusaka suluhu ya mkwamo wa mchakato wa Katiba. Mkutano wa jana ulikuwa na sehemu mbili kuu, wa kwanza ulifanyika katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma ambako viongozi hao walikutana na Rais Kikwete na mwingine katika Hoteli ya St. Gasper ambao uliwashirikisha viongozi na maofisa wa vyama vilivyoshiriki bila Rais Kikwete. Mkutano huo ni matunda ya jitihada zinazofanywa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho kiliratibu mazungumzo hayo yaliyochukua zaidi ya saa mbili na nusu, katika Ikulu ya Kilimani, wakati yale ya St. Gaspar yalichukua takriban saa moja na nusu.
Viongozi walioshiriki kikao hicho cha Ikulu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya. Wengine ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, Mwenyekiti wa UDP ambaye pia ndiye mwenye zamu ya uenyekiti wa TCD, John Cheyo na Mwenyekiti wa UPDP pamoja na mwakilishi wa vyama visivyokuwa na wabunge ndani ya TCD, Fahmi Dovutwa. Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Rais Kikwete baada ya kuanza kwa kikao hicho alitoa fursa kwa kila aliyekuwapo kuzungumza na hapo zilijitokeza hoja mbalimbali, nyingi mwelekeo wake ukiwa ni kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu ili kutoa fursa kwa nchi kuendelea na masuala mengine makubwa.
Chanzo chetu kilisema: “Rais amekuwa msikivu kweli, amewasikiliza wote lakini ugumu ulianza kuonekana pale ilipotolewa kauli ya kuwauliza wale watu wa Ukawa kama wanaonaje wakirejea halafu hoja zao zikazungumzwa ndani ya Bunge Maalumu, yaani hawataki kabisa kusikia hilo.” Kuhusu hoja ya kusitishwa kwa Bunge, habari zinasema ilijadiliwa kwa kirefu na wataalamu wa sheria wakijaribu kutoa uzoefu wao, lakini kikwazo kilichoonekana ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo haimpi Rais mamlaka ya kusitisha Bunge. “Rais alisema hoja zao ni nzuri na zina mashiko, lakini suala kubwa likawa ni kwamba tunafikaje huko wanakopendekeza? Maana sheria iko kimya kuhusu mamlaka ya Rais kusitisha Bunge Maalumu, ndiyo maana sasa tulitoka Ikulu tukaenda St. Gaspar ili kujadili, ngoja tusubiri hiyo tarehe 8 maana siyo mbali,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Kauli ya TCD
Baada ya kikao cha St. Gasper, Mwenyekiti wa TCD, Cheyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mazungumzo na Rais Kikwete yalikuwa mazuri na kwamba wamekubaliana kukutana naye tena Septemba 8, mwaka huu baada ya kuwa wamezifanyia kazi hoja ambazo zilijitokeza kwenye vikao hivyo. “Kama nilivyowaambia siku ile tulipokutana, tulikuwa na ajenda mbili tu kubwa, kwanza ni mchakato wa Katiba Mpya unavyokwenda na ajenda ya pili ni jinsi tunavyoweza kusonga mbele na kuwa na maandalizi ya uchaguzi mzuri mwakani,” alisema Cheyo lakini akikataa kujibu maswali mengine ya waandishi wa habari. Cheyo alisema baada ya kukutana na Rais Kikwete, waliendelea na kikao cha viongozi wa vyama kwa ajili ya kuona jinsi ya kuyafanyia kazi mambo yaliyojitokeza, hivyo wameamua kuunda kamati ndogo ya watu wanne itakayoongozwa na Mbatia kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Kinana, Profesa Lipumba na Dk Slaa ambao wamepewa wajibu wa kuwasilisha ripoti yao kwenye kikao cha wenyeviti wa vyama vinavyounda TCD ili ijadiliwe kabla ya kikao cha Septemba 8, ambacho hata hivyo, hakijafahamika kitafanyika wapi. Habari zinasema miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi ni pamoja na kuona kama Bunge linaweza kusitishwa bila kuleta athari zozote za kisheria na kisiasa, lakini wakizingatia uwapo wa makundi mengine ndani ya Bunge hilo hasa wabunge wa kuteuliwa kupitia kundi la 201. “Lakini hapa kuna suala moja kwamba Ukawa wako nje ya Bunge, ni vigumu kuwaamrisha wale walioko ndani ya Bunge ili watekeleze matakwa yao, kwa hiyo kuna kazi kubwa sana ya kufanya,” kilisema chanzo chetu.
Mgomo wa Ukawa
Dalili za Ukawa kukataa kurejea bungeni zilianza kuonekana mapema baada ya mazungumzo yasiyo rasmi ambayo yalifanyika katika moja ya kumbi za Hoteli ya Dodoma ambako walikwenda kupata chai baada ya kuwasili. Wakati wakitoka kwenye ukumbi huo kuelekea Ikulu Kilimani, baadhi yao walisikika wakipeana tahadhari kwamba wasikubali wazo la kurejea bungeni, ambalo ni dhahiri walikuwa wamepewa wakati wakinywa chai. Baadaye ndani ya basi dogo wakati wakielekea Ikulu, Lissu alisikika akisema: “Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi haiwezekani kabisa.”
Pia habari kutoka katika Ukumbi wa St. Gaspar zinasema hata katika kikao hicho, viongozi hao walishauriwa kurejea bungeni ili hoja za kuahirishwa kwa Bunge Maalumu zitolewe huko, lakini waligoma. Taarifa zinasema Ukawa walijenga hoja kwamba Bunge Maalumu halipaswi kuendelea kwa sababu kuna kila dalili kuwa muda uliopo hautoshi kukamilisha mchakato na ikizingatiwa kwamba nchi inakabiliwa na mambo mengi ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa 2015. “Pia kulikuwa na hoja kuhusu mambo ya Daftari la Wapigakura na mabadiliko ya sheria ambazo zinagusa taasisi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria mbalimbali zinazihusu vyama vya siasa na mambo ya matokeo ya rais kuhojiwa nadhani,” kilieleza chanzo kingine. Kushindwa kupatikana kwa suluhu ya mchakato wa Katiba, kunaendelea kuuweka mchakato huo njiapanda hasa ikizingatiwa kwamba Bunge Maalumu linaendelea kesho kupokea ripoti za kamati kuhusu uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba.
Nukuu
“Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi haiwezekani kabisa.” Lissu
Mwananchi
No comments:
Post a Comment