Kuhusiana na mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya, CCT inaamini kuwa
suala hili ni la MARIDHIANO na sio la ubabe wa kikundi au chama fulani
cha siasa.-Kama ambavyo ilitangazwa na Mhe. Rais Januari 2014 kuwa
Taasisi mbalimbali zipeleke mapendekezo ya wajumbe wanaoweza kuteuliwa
kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, CCT ilipeleka mapendekezo ya
wajumbe tisa na kati ya hao Mhe. Rais alimteua mjumbe mmoja tu ambaye ni
Bibi Esther Msambazi.
Mjumbe huyu aliyeteuliwa ni Mkristo wa kawaida (lay Christian) na wala
si Kiongozi wa Dhehebu lolote la Wanachama wa CCT na pia hata sio Mzee
wa Kanisa analotoka bali Mkristo mwaminifu wa kawaida. Huyu ndiye
mwakilishi wa CCT kwenye Bunge Maalum la Katiba. Viongozi wengine wa
Dini ya Kikristo (Maaskofu na Wachungaji) waliopo katika Bunge hilo
HAWAKUTUMWA NA CCT na wala CCT haina taarifa ni vipi walichaguliwa kuwa
wajumbe wa Bunge hilo Maalum.
Aidha, pia Jukwaa la Wakristo Tanzania haliwatambui Viongozi hao kwani
Jukwaa hilo linaundwa na Taasisi za TEC, CCT, PCT na SDA. Kutokana na
misingi ya imani ya taasisi hizi kwa umoja wake, Viongozi
wakishakubaliana jambo fulani kwa pamoja na kwa umoja wao wanalisimamia
na kulitekeleza. NDIYO YAO NI NDIYO NA HAPANA NI HAPANA kwa kuwa hawana
ndimi mbili na wala hawatumikii Mabwana wawili.
Kwa mantiki hiyo, CCT ikiwa mmoja wa taasisi zinazounda Jukwaa la
Kikristo Tanzania inaendelea kusisitiza kuwa msimamo wa viongozi wa dini
kama ulivyotolewa na Jukwaa la Kikristo Tanzania kuhusiana na Maoni
waliyopeleka kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi chini ya Uenyekiti
wa Mhe. Jaji Mstaafu Warioba na Matamko waliyotoa ni sahihi na
itaendelea kuyasimamia na kuyasambaza hadi yamfikie kila Mkristo ili
wananchi wa Tanzania wapate Katiba wanayoitaka.
Aidha, Viongozi hao wa Jukwaa la Wakristo Tanzania haliwezi kutafuta
maoni ya Viongozi wa Dini walioko katika Bunge Maalum la Katiba kwa
sababu hawawatambui kama wawakilishi wa taasisi zao na hivyo kukataa kwa
nguvu zote yale ambayo viongozi hao waliopo Bungeni watakuwa
wakiyasema. Mwisho kabisa tunawaomba viongozi hao wajiulize, “hivi sisi
tumetumwa na tunamwakilisha nani humu Bungeni?
Imetolewa September
05, 2014 Na JUMUIYA YA KIKRISTO
No comments:
Post a Comment