CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO; JIMBO
LA KIGOMA KASKAZINI
TAMKO KUHUSU KUONDOKA KWA WALIOKUWA VIONGOZI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kigoma
Kaskazini tunapenda kutoa taarifa kwa umma kutokana na sintofahamu inayotaka
kulazimishwa mbele ya jamii kuhusu uimara wa chama chetu mkoani Kigoma.
Tangu jana na leo kumeenea taarifa zinazowahusu watu watatu,
Jaffari Kasisiko, Msafiri Wamarwa na Mama Malunga Masoud, ambao vyombo
mbalimbali vya habari vimeandika kuwa wamehama chama chetu cha CHADEMA na
kukimbilia wanakojua wao (maana CCM inafanya kazi zake katika sura mbalimbali).
Katika hatua ya awali, sisi CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini
tungependa kusema machache juu suala hilo la watu hao kuhama;
1. Kwanza
watu hao mbali ya kwamba walikuwa ni viongozi wa chama ngazi ya mkoa, kwa
uhakika kabisa walikuwa ni kikwazo kama si kizuizi cha muda mrefu sana kwa chama
chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika mkoa mzima wa Kigoma ili kiweze
kukimbizana na wenzetu wa maeneo mengine nchi nzima. Badala yake walikikumbatia
na kukiatamia chama. Wakati maeneo mengine wenzetu wakiongeza wabunge
majimboni, Kigoma chini ya uongozi wao ikauza majimbo.
2. Tunaweza
kusema kuwa viongozi hawa pamoja na wengine wachache ambao tunajua wako mbioni
kuondoka kati ya leo na kesho, walikuwa ni sawa na KOTI LILILOTUBANA. Kwa muda
wao wote wa uongozi hawakuwahi kufanya kazi yoyote ya kioganazesheni na
kukieneza chama mkoa mzima. Wao walikuwa watu wa mikutano ya hapa na pale
Kigoma mjini pekee au pale ambapo kunakuwa na uongozi wa kitaifa au wabunge.
3. Kwa
muda mrefu saa wamekuwa viongozi ‘waliotubana’ kwa sababu walifanya kazi kwa
kuangalia zaidi maslahi yao. Sasa kuondoka kwao, ni nafuu kwa chama. Pia ni
fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka kwa wanachama makamanda waaminifu na watiifu
waliofungiwa milango kwa muda mrefu, kusonga mbele kukijenga chama chetu kwa
imani kubwa ya kuendelea kubeba matumaini ya Watanzania wanyonge.
4. Upo
ushahidi wa wazi katika hili. Kwa muda mrefu sasa viongozi hao na wengine
wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine, wamekuwa wakilalamikiwa kufanya
kazi ya chama kingine cha siasa kwa maslahi na maelekezo ya CCM.
5. Katika
madai yao ya kuhama chama watu hao wamesema wamefikia hatua hiyo eti kutokana
na chama chetu kuwa cha kibabe eti kwa sababu tu Zitto Kabwe alivuliwa nafasi
Naibu Katibu Mkuu ndani ya chama!
6. Madai
hayo yanashangaza kwa sababu mbali ya chama kuwa na sababu nzito za kumvua
Zitto (na wenzake akina Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) cheo hicho kutokana
na tuhuma za utovu wa nidhamu, pia tunaamini hakuna mwanaCHADEMA amejiunga na
chama hiki kwa ajili ya cheo. Ndani ya chama chetu tunaamini katika kugawana
majukumu si vyeo.
7. Katika
hali ya kushangaza zaidi wanasema eti Zitto amezuiwa kugombea uenyekiti. Sasa
tunajiuliza hiyo nia ya kugombea ambayo hatujawahi kuisikia ikitangazwa kwa
kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na itifaki za chama, waliambizana wao
wenyewe na mtu wao? Lakini kwa wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma tunaelewa Jafari
Kasisiko analipa fadhila za misaada binafsi ikiwemo kupelekwa nje ya nchi.
8. Ninaomba
kutoa wito kwa viongozi wenzangu wa wilaya na majimbo ya Kasulu Mashariki,
Muhambwe, Buyungu, Kasulu Magharibi, Manyovu, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini
na Kigoma Mjini, tukutane kwa ajili ya kikao cha Baraza la Mashauriano la Mkoa
ili sasa tuchukue hatua zingine za muhimu na haraka za kuhakikisha tunasafisha
chama chetu kwa kuwaondoa vibaraka na wasaliti wote waliosalia.
9. Pia
tunaomba katika hali ya dharura Chama Makao Makuu pia kiingilie kwa kutumia
kifungu cha Katiba 6.1.3, ili kupata chombo cha kuendelea kuwaunganisha
wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua hatua hiyo kupitia Baraza la
Mashauriano.
10. Sisi wa CHADEMA Kigoma Kaskazini tunawataka
wale wengine waliosalia katika mkakati huo wa kuhamisha watu wachache lakini
kwa makundi ili eti kujenga taswira ya CHADEMA kubomoka, wakiwemo viongozi
kadhaa wa Kanda wasisubiri. Chama chetu kitajengwa na watu wenye imani
watakaoweka maslahi na matakwa ya wananchi mbele kwa kuzingatia misingi yetu
kama inavyoelezwa katika Katiba ya Chama, kanuni, maadili na miongozo.
Kwa niaba ya Wanachadema imara na makamanda watiifu na
waaminifu kwa mabadiliko yanayobeba matumaini na haki za Watanzania wanyonge,
naomba kutoa taarifa hii.
Ally Kisala
Mwenyekiti wa CHADEMA
Jimbo la Kigoma Kaskazini
Mjumbe wa Baraza la
Mashauriano la Mkoa wa Kigoma
No comments:
Post a Comment