Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 23, 2014

Molloimet: Kukataa serikali tatu, CCM ijiandae kuwa chama cha upinzani

Arusha. Agosti 5 mwaka huu, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanatarajiwa kuanza kukutana tena mjini Dodoma kujadili rasimu ya mabadiliko ya Katiba. Kikao cha Bunge hilo, kinatarajiwa kufanyika kwa takriban siku 60 na baadaye rasimu ya katiba iliyojadiliwa itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura. Mchakato wa kupatikana Katiba Mpya kwa sasa umekumbwa na sintofahamu hasa kutokana na wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa ) ambalo linaundwa na viongozi wa upinzani kuamua kususia vikao na kurudi kwa wananchi. Hata hivyo, wanasiasa na wanataaluma mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni nini kifanyike ili kunusuru mchakato huu na pia wamekuwa wakitoa maoni mbali mbali .
Luteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), mkuu wa wilaya wa zamani na mbunge, Lepilali ole Molloimet ni mmoja wa wanasiasa wakongwe ambaye katika mahojiano na Mwananchi anazungumzia mambo mengi. Molloimet ambaye aliongoza wilaya mbalimbali nchini, ana yapi ya kusema kuhusu Katiba Mpya na hali ya kisiasa nchini? 
Swali: Tanzania ipo mchakato wa kupata Katiba Mpya na sintofahamu zimeukumba mchakato je, unadhani kuna upungufu gani katika mchakato huu mzima.
Jibu: Mimi naamini upatikanaji wa wajumbe wa Bunge hili haukuwa sahihi hasa kwa kuwashirikisha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wenzao kutoka Baraza la Wawakilishi.
Ilipaswa Bunge hili liwe na uwakilishi tofauti, wajumbe wateuliwe na wananchi kutoka kila wilayani ambao wangeweza kuingia bungeni bila misimamo ya vyama vyao na lengo lao kubwa liwe ni kusaidia kupata Katiba Mpya na siyo sasa kusababisha migongano.
Swali: Unadhani wapo wajumbe wenye upungufu na ambao hawakustahili kuwamo kwenye Bunge hilo.
Jibu: Ndiyo, wapo wabunge ambao waliiingia bungeni kwa kuzingatia vyama vyao au urafiki na viongozi ndiyo sababu unasikia kuna malalamiko mengi. Binafsi, nilidhani wabunge wote wasingekuwepo kwenye Bunge la Katiba kwani ni chanzo cha mgogoro kwa kuwa baadhi wanapigania masilahi yao badala ya taifa.
Swali: Moja ya mambo yanayokwamisha mchakato wa Katiba Mpya ni mapendekezo ya rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya muundo wa serikali tatu, nini maoni yako.
Jibu: Mimi tangu nikipokuwa mbunge wa Monduli, msimamo wangu ni serikali tatu, tena kwa mazingira ya sasa haikwepeki tena.
Wenzetu Zanzibar wamefanya mabadiliko makubwa kwenye katiba yao, ambayo kimsingi yanalazimisha serikali tatu na viongozi walikuwa kimya wakati wote sasa hakuna jinsi ni kukubaliana na maoni ya walio wengi.
Swali: Lakini, waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume walipounganisha nchi walikuwa na malengo mema ikiwamo kuimarisha ulinzi na uchumi ni nini mtazamo wako?
Jibu: Ni kweli wakati ule kulikuwa na tishio la uvamizi, hasa kwa Zanzibar kupitia baharini, lakini sasa hakuna mambo kama hayo tena dunia imepiga hatua kubwa za kiulinzi na usalama.
Pia, ni kweli kiuchumi Muungano una mafanikio lakini, ikumbukwe muungano ni wa watu siyo serikali hivyo, hata serikali tatu zikiundwa tusitegemea watu kutengana ni kuboresha tu upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Swali: Chama cha Mapinduzi (CCM) tayari kimetoa msimamo wa kutetea serikali mbili unadhani kuna athari yoyote inaweza kutokea?
Jibu: Mimi pia ni mwanaCCM, nasema msimamo huu una madhara kwani wananchi wengi wanapinga na tukibaki na msimamo huu, tujiandae kuwa chama kikuu cha upinzani hivi karibuni.
Tunapaswa kuwasikiliza wananchi na hili ni tatizo, viongozi wetu wamekuwa hawashauriki, wanawasikiliza marafiki zao tu na ndiyo hawa wanateuliwa kuwa viongozi sasa. Leo hii hata Bunge lina baadhi ya watu wa ajabu, wamepatikana bila kujali sifa, tunashinikizwa kuwa na wabunge wengi viti maalumu hili jambo lina athari kwani hatupati wabunge bora wanawake, binafsi nadhani tungewaacha wagombee majimbo kwani wapo wenye uwepo mkubwa wakigombea huko na watashinda.
Swali: Wewe ulikuwa mbunge kutoka Jimbo la Monduli, wakati huo kulikuwa na changamoto nyingi katika suala la wa wafugaji unadhani matatizo yamepungua?
Jibu: Ni kweli wakati ule kulikuwa na changamoto na baadhi zimepatiwa ufumbuzi lakini hili la wafugaji nadhani matatizo yao yameongezeka zaidi.
Hivi sasa wamekuwa kama wakimbizi kwenye nchi yao, wanafukuzwa kila mahali hata walipotoka ardhi yao imetolewa kwa wawekezaji, sasa Taifa letu wawekezaji ji bora kuliko wananchi wao ndiyo wanafaidi rasilimali za nchi hii.
Swali:Unadhani nini kifanyike kupunguza matatizo haya ya ardhi?
Jibu: Serikali lazima ipime ardhi yote, itenge maeneo ya kilimo, ufugaji, huduma za jamii na maeneo ya uwekezaji kwani kufanya hivyo kutasaidia kupinguza haya mapigano kila kona ya nchi kugombea ardhi.
Swali: Tangu ulipostaafu nafasi ya ukuu wa wilaya umekuwa kijijini kwako Longido, ina maana umestaafu siasa na je, hauna nia kugombea ubunge tena?
Jibu: Hapana, mimi ni mwanasiasa na nitaendelea kuwa mwanasiasa na wananchi wakiniomba kugombea nitakuwa tayari kwani wananijua mimi wakati wote nimekuwa mtetezi wao.
Mwananchi

No comments: