Kupitia njia mbalimbali za upashanaji
habari, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samuel Sitta amenukuliwa leo akisema kuwa
ameunda Kamati ya Mashauriano ili kuondoa alichokiita ni mpasuko kati ya
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na Umoja ya Katiba ya Wananchi
(UKAWA) na wajumbe wengine.
Kwa mujibu wa habari hizo Sitta
amenukuliwa akisema kuwa kamati yake yenye wajumbe 27 itakutana Julai 24, mwaka
huu ambapo amesema kuwa watajadili mwenendo wa majadiliano katika Bunge hilo na
sura 15 za Rasimu ya Katiba Mpya, ili ‘eti’ kujua yapi muhimu yanayotakiwa
kupewa kipaumbele kabla ya Bunge Maalum la Katiba kuanza vikao vyake hapo
Agosti 5, mwaka huu.
Taarifa hiyo ya Sitta akiwa
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba imedhihirisha masuala kadhaa, kama
ifuatavyo;
1. Hajui anachokitafuta
Wakati katika hali ya juu inaweza
kudhaniwa kuwa Sitta anatafuta suluhu yenye kuleta maridhiano na hatimaye
mwafaka wa kitaifa kwenye suala la Katiba Mpya, taarifa hiyo ikisomwa kwa
makini na kina, inaonesha namna ambavyo ‘harakati’ zake hizo ni mwendelezo wa
hila za watawala kusaka Katiba Mpya kwa kura, badala ya maridhiano
yanayosimamia maoni, maslahi na matakwa ya wananchi.
Moja ya vyombo vya habari
vilivyoripoti taarifa hiyo ya Sitta, kimeandika;
“Pamoja
na mambo mengine, Sitta alisema upo uwezekano wa Ukawa kurudi bungeni lakini
wakasusa tena kadiri mjadala utavyoendelea. Iwapo itatokea hali hiyo, Bunge
litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili
kufanya maamuzi.”
Kauli hiyo inadhihirisha kuwa Sitta
kama Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, tena mwanasheria kwa taaluma na sasa
mwanasiasa, hajielekezi katika kuhakikisha kuwa Katiba Mpya inakidhi moja ya
vigezo muhimu sana ambavyo ni kuwa na uhalali wa kisiasa unaotokana na
maridhiano au mwafaka wa kitaifa.
Na hii ndiyo sehemu kubwa inapolalia
hila ya walioko madarakani, wakiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kupanga kutumia wingi wa kura kuamua suala nyeti la Katiba Mpya kwa sababu tu
wanapigania kuhakikisha matakwa ya CCM yanawekwa mbele kutokana na maelekezo ya
vikao vya chama hicho, vilivyotoa nyaraka zikitaka ‘mambo’ ya CCM ndiyo yawe
Katiba Mpya.
Ni mwendelezo wa hila za walioko
madarakani kutaka kutumia hila za kura badala ya maridhiano, kupitisha matakwa
na misimamo ya viongozi wa CCM huku maoni, maslahi na matakwa ya wananchi kama
walivyoyawasilisha mbele ya Tume ya Jaji Warioba yakiwekwa kando, kubezwa na
kudharauliwa.
2. Kuendeleza lugha ya dharau, kubeza
Aidha, wakati kupitia taarifa hiyo,
Sitta anataka kujipambanua kuwa msaka suluhu na maridhiano, lakini ameshindwa
kuficha uhalisia wake, ambapo ameendeleza tabia ile ile ya Wajumbe wa BMK wanaotokana
na CCM (au wanaounda Kundi la Tanzania Kwanza), kutumia lugha ya kebehi na
dharau kwenye jambo nyeti linalohitaji masikilizano, ikiwemo matumizi ya maneno
na lugha.
Hilo linadhihirika pale aliponukuliwa
akisema “kutakuwa na watu karibu 27, mimi
nikiwa mwenyekiti, atakayevimba kichwa na
kudharau, wananchi watajua nia yake ni tofauti na Katiba Mpya.” Kwa mtu yeyote makini, hawezi kuamini
kuwa maneno hayo yanaweza kutumiwa na mtu anayetaka kuonekana anasaka suluhu
kwenye jambo nyeti kama Katiba!
Lakini pia maneno hayo yanaibua
shauku zaidi ya kujua; kwa nini Sitta tayari anaonekana kuwa ‘defensive’ kwamba
kuna viongozi watadharau huo wito wake au uteuzi wake?
Sitta amefanya uteuzi huo kama
nani kuweza kupata watu 27nchi nzima?
Je Sitta ameanza kushtukia uhalali wa
uteuzi wake huo ambao haujulikani kaufanya lini, wapi, katika mazingira gani,
akimhusisha nani?
Je anajishtukia kuwa ameteua watu
ambao hawatakubalika?
Je hao viongozi wa dini ambao
amewateua ni wale wale ambao tayari tumewasikia ndani ya BMK wakisahau wajibu
wao katika jamii, (maaskofu, wachungaji na mashehe) kisha wakatoa misimamo yao
hadharani kuungana na CCM dhidi ya wananchi?
Ni watu gani hao hasa ambao Sitta
amewateua kisirisiri akitaka wasimame kuwa wasuluhisi chini ya mwamvuli wake?
Swali jingine muhimu, Je kwa kitendo
cha Sitta na wenzake kuendelea kuonesha msimamo wao kinyume cha maoni ya
wananchi wakati huo huo wanawateua viongozi wa dini kujadili suala hilo hilo kwa
mlengo wanaoutaka wao (akina Sitta) Je sasa wameamua hata kuwachonganisha
viongozi wa dini na waumini wao? Kwa sababu waumini ni hao hao Watanzania waliotoa
maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ambayo CCM wameyabeza na
kuyadharau hadharani!
3. Tayari anao upande wake
Aidha, kitendo cha Sitta kupitia
taarifa hiyo kujaribu kuonesha au kulazimisha taswira kuwa tatizo la mkwamo huu
wa Katiba Mpya ni UKAWA, kuamua kutoliangalia jambo hili katika ‘picha pana’ na
kulichukulia kwa uzito wake.
Ni matokeo ya kutopenda kuutafuta,
kuuona na kuukiri ukweli hata kama unauma. Watanzania wote ambao wanafuatilia
mchakato huu wa Katiba Mpya kama moja ya fursa adhimu za kujiumba kama taifa,
watashangaa kuona Mwenyekiti wa Katiba hajui kuwa CCM, tena kupitia maamuzi ya
vikao vya chama hicho na kauli za Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ndiyo
zimekwamisha mchakato huu nyeti.
Kwamba kupitia vikao vyao
vinavyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, chama hicho kilitoa
maelekezo kwa nyaraka za siri kikitaka wajumbe wanaotokana nacho wasimamie misimamo ya chama. Nao wakafanya hivyo kwa
dharau, kubeza na kutukana maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
Mpya kama ilivyowasilishwa na Jaji Warioba.
Wananchi wanajua kuwa kitendo cha
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kushindwa kutumia nafasi yake ya ukuu wa
nchi wakati wa uzinduzi wa Bunge Maalum la Katiba Mpya kuliongoza taifa zima
kujadili Rasimu ya Pili, kwa kuzingatia maoni ya wananchi, badala yake akatumia
wadhifa wa uenyekiti wa chama kuweka misimamo ya kichama inayotokana na vikao
vya chama alivyovisimamia, ni moja ya vigingi vilivyokwamisha na kuharibu mchakato
huu.
Tayari, kutokana na taarifa za ziada
na kina zilizopo, tunajua kauli hizo au hali hiyo ya kuwa na upande
anayoionesha Sitta si jambo la bahati mbaya. CCM kupitia taarifa yao maalum kuhusu
mwenendo wa BMK, wanakiri kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Marekebisho
ya Katiba Sura ya 83, ili Bunge Maalum
liweze kupitisha vifungu vya Katiba ni lazima zipatikane theluthi mbili za kura
kwa pande zote za Muungano, lakini kutokana na msimamo wa UKAWA kusimamia
misingi ya uandishi wa katiba, maoni, maslahi na matakwa ya wananchi, CCM
wameshindwa kutimiza malengo yao.
Sasa anachofanya Sitta kwa ghiliba na
hadaa ya kutafuta suluhu ni kuanza kufanya maandalizi ya namna ya kuharibu
mchakato kwa ‘kuchezea’ kifungu hicho cha sheria.
4. Kuendelea kudharau msingi wa Rasimu
ya Katiba
Mwenyekiti wa BMK Sitta pia kupitia
taarifa hiyo ameendeleza kauli zile zile ambazo zimekuwa zikitolewa na wajumbe
wa bunge hilo wanaotokana na CCM, ambazo hasa ndizo zilikuwa moja ya sababu
kubwa kwa UKAWA kutoka nje kususia vikao vile.
Amenukuliwa akisema “yapo mambo muhimu zaidi katika rasimu hii
kama vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya haki za binadamu, uongozi wa
asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar nafasi nafasi zaidi katika
Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko muundo…ya nini kuyapiga
teke yote haya na kujikita katika muundo pekee.”
Huu ni mwendelezo wa dharau dhidi ya
Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi. Sitta akiwa Mwenyekiti wa
BMK na mwanasheria anajua wazi kuwa msingi wa rasimu hiyo ni uwepo wa Muundo wa
Shirikisho la Serikali, sasa msuluhishi (kama mjenzi) anawezaje kubeza umuhimu
wa msingi lakini akang’ang’ania kuendelea kujenga ukuta, kuweka madirisha,
milango, paa na vingine vyote vinavyokamilisha ujenzi wa namna hiyo? Mambo hayo
yako kwenye hadithi. Labda kama Samuel Sitta anataka kugeuza jambo hili nyeti
kuwa ni sawa na Hadithi za Abunuwas!
5. Maneno yale yale; yeye, Mangula na
vijana wao
Kama ambavyo kwa nyakati tofauti
viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa viroja (badala ya hoja) na propaganda
mbalimbali dhidi ya UKAWA wakijaribu kuhamisha mjadala kwa kuibua tuhuma
zisizokuwa na msingi, Sitta naye ametumia mtindo huo huo hali ambayo inaonesha
kuwa mambo haya yanapangwa na CCM kwa lengo lile lile; kuhakikisha Katiba Mpya
haipatikani.
Amenukuliwa akisema “Sisi tumeshapeleka barua kwa wajumbe,
tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo tutaelewana kuhusu masuala hayo
na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda
ya siri.
““kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti, atakayevimba kichwa
na kudharau, wananchi watajua nia yake
ni tofauti na Katiba Mpya.”
Mpango huo wa kuzusha tuhuma hizi
mara zile, zikitumia maneno kama hayo aliyotumia Samuel Sitta umekuwa ukitumika
na viongozi wa CCM mara kadhaa sasa. Makamu Mwenyekiti Phillip Mangula (ambaye
baadae alikanusha) na vijana wao kama Nape Nnauye na wengine wamesikika mara
kadhaa wakitoa tuhuma za uongo dhidi ya UKAWA, kuhusu hongo au kutumiwa
kuvuruga mchakato.
Propaganda na hila hizi hazitasaidia.
Wananchi wanajua aliyekwamisha mchakato huu. Mtu anayetaka kuwa msuluhisi
anapoingia akiwa na ‘sentiments’ kama hizo ambazo zinaimbwa kila siku
majukwaani na viongozi wa CCM kwa lengo la kuhadaa na kughilibu umma, anakuwa
tayari amejipungizia uhalali wa yeye kutiliwa maanani na kutoa mwanya wa
umakini wake kuhojiwa.
Tumkumbushe Sitta na wenzake
waliozoea kuendesha mambo kwa hila na propaganda, msimamo wa UKAWA ambao
haujayumba na mara kadhaa sasa umesisitizwa na viongozi waandamizi, akiwemo
Mwenyekiti Freeman Mbowe, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, James Mbatia, ni
kwamba; Rasimu ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi iheshimiwe.
Bunge Maalum la Katiba lina kazi ya
kujadili na kupitisha rasimu hiyo, mjadala unapaswa kuongozwa kwa kuzingatia
hilo bila kusahau kuwa kiini au msingi wa rasimu hiyo ni kuwepo kwa Muundo wa
Shirikisho la Serikali tatu. Hayo ndiyo maoni ya wananchi ambayo UKAWA umeamua
kuyasimamia.
Imetolewa Jumatano, Julai 9, 2014 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari-CHADEMA
No comments:
Post a Comment