CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebaini hujuma zinazodaiwa kufanywa kwa
ubia kati ya Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka kuanzisha
vurugu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika
kesho kutwa katika kata 26 nchini. Chama hicho
kimeeleza kuwa hata matukio ya kuvamiwa, kupigwa na kisha kukamatwa kwa wafuasi
wa CHADEMA ni matokeo ya hujuma hizo. Kauli hiyo
ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Usimamizi
wa Kanda, Benson Kigaila, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuelezea
ushiriki na mkakati wa CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga,
mkoani Iringa.
Mbali na
kuelezea mkakati wa ushindi katika Jimbo la Kalenga, pia Kigaila
alielezea matukio yanayotokea katika kampeni ya uchaguzi mdogo wa
madiwani kwa kata 26 unaoendelea sasa sehemu mbalimbali nchini. Akizungumzia
ushirikiano wa Polisi na CCM katika kuihujumu CHADEMA, Kigaila alisema mkakati
huo ulianza wakati wa M4C Operesheni Pamoja Daima, ambapo wakiwa mkoani Mbeya
katika Wilaya ya Mbarali, waligundua kambi ya vijana wa CCM wapatao 300
waliopangwa kufanya vurugu kwenye mkutano wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.
Willibrod Slaa, mkoani humo. “Tulipobaini
mbinu zao niliwasiliana na RPC Mbeya, chakushangaza badala ya kushughulika na
wahalifu hao, akaamua kumuita mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo na kumueleza
wasitishe vurugu walizopanga kuzifanya na kama zingefanyika, tuliwaambia
tutamkamata mwenyekiti wa mkoa badala ya wafanya vurugu na kweli wakasitisha,”
alisema Kigaila.
Alisema
kinachosikitisha ni kuona wafuasi wa CHADEMA wakipigwa na kuumizwa, lakini
polisi inawakamata watu walioumizwa badala ya kuwatafuta waliosababisha maumivu
hayo. “Waliofanya
fujo CCM, walioumizwa CHADEMA, waliokamatwa CHADEMA, inakuwaje hali hii na haya
mambo ya CCM kwanini yanaibuka kila panapokuwa na uchaguzi?” alihoji Kigaila. Alisema
tayari malalamiko yao dhidi ya polisi wameyafikisha kwa Msajili wa Vyama
vya Siasa ambaye ndiye mlezi wa vyama nchini na kumuomba aingilie kati hali
hiyo kabla uvumilivu haujawashinda wafuasi wao.
16
wajitokeza Kalenga
Akizungumzia
maandalizi ya uchaguzi wa Jimbo la Kalenga lililoachwa wazi na marehemu William
Mgimwa, Kigaila alisema kazi ya kuchukua fomu ndani ya chama imeshaanza na hadi
jana watu 16 walishachukua fomu kuomba ridhaa ya chama. Alisema
fomu za CHADEMA zimeanza kutolewa juzi na mwisho ni Februari 9 na hadi
jana watu 16 walishachukua fomu. Aliongeza
kuwa fomu zinapatikana katika tovuti ya CHADEMA ya CHADEMA WEBSITE pia makao makuu ya
chama hicho pamoja na ofisi ya Jimbo la Kalenga. Kigaila
alisema Kamati Kuu ya CHADEMA itakutana Februari 12 kwa ajili ya uteuzi wa
mwisho wa mtu atakayepeperusha bendera ya CHADEMA. Uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Kalenga unafanyika kuziba nafasi ya marehemu William Mgimwa
aliyefariki dunia Januari Mosi nchini Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment