Unaweza kusema sasa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula kusema kuwa
wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015 watachukuliwa hatua
kali za kinidhamu. Mangula alisema kama wanachama hao
wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya
kisiasa nchini; “Wapo watu wanataka waichanechane
CCM kwa sababu ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata
urais. Kuna makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe
hatuwezi kuyafumbia macho.” Akifafanua hilo Mangula alisema:
“Tutawaita wote walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwanini
wanafanya hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza katika mikutano
wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua
dhamira yao ni nini.”
Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa
imepita siku moja tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye
kusema mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda
mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea. Nape alitoa kauli hiyo baada ya
Lowassa siku mbili zilizopita, kutangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi
safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za
Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika. Lowassa ambaye amekuwa akitajwa
kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa
2015, alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli. Mangula aliwashukia vigogo wa
chama hicho wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati ya
Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa salamu za mwaka
mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.
Ataja kanuni za uongozi
Katika mkutano huo Mangula
alisaidiwa kusoma kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea
ufafanuzi mambo mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa
CCM na wanachama taifa, Masoud Mbengula. Moja ya kanuni hizo inasema “Ni
mwiko kwa kiongozi wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au
eneo analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye mwenyewe
ama mgombea anayemuunga mkono.” Mangula alisema kwa mujibu wa
kanuni za chama hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa
msaliti na hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza chama
wakati wowote. Tutawachukulia hatua kali wale
wote ambao wameanza kuonyesha dalili kama hizo za kutoa michango, misaada,
zawadi. Lengo la mwanachama huyo ni kutaka kuungwa mkono, wanaotaka madaraka
wasubiri muda ufike ndiyo wafanye hivyo.”
Aliongeza “Hivi haya mapenzi ya
kusaidia yameanza lini, fedha hizo zinatoka wapi, hawa wanaosadiwa wanatakiwa
kutambua kuwa yote hayo ni kampeni kwa kuwekeza, hatuwezi kuwa na viongozi wa
nchi wa namna hii wa uchu wa madaraka, CCM haitawafumbia macho lazima kanuni na
miongozo ifuatwe.” “Kuna watu wameanza kudhani kuwa
muda wa kampeni umeanza, muda wa kampeni haujafika na hakuna majina
yaliyotangazwa ya kugombea udiwani, ubunge hata urais,” alisema Mangula na
kuongeza; “Kuna makundi yanaifanya nchi ya
Somalia isitawalike. Makundi ya aina hiyo naona yapo hata CCM; watu wanaibua
vita ya maneno ndani ya chama, wanataka wakichanechane chama kwa sababu ya
uroho wa madaraka tu.”
Bila kuyataja makundi hayo Mangula
alisema: “Utaongozaje nchi ambayo imegawanyika katika makundi? Watu wameanza
kuvuruga chama chetu, kila mtu ana kundi lake na wakati mwingine wanayatumia
makundi kuwabomoa wenzao, hili jambo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo.” Mbali na Lowassa, wengine
wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba. Makamba hivi karibuni amekuwa
akitoa misaada kwa vikundi vya waendesha bodaboda katika mikoa mbalimbali, hali
ambayo inatafsiriwa kuwa ni kujiimarisha kisiasa.
Hata hivyo, mwaka jana Rais Jakaya
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa alinukuliwa akisema kuwa sio
vibaya kwa wanachama wa chama hicho kuonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi
ndani ya chama, lakini siyo kufanya kampeni. Mei 26 mwaka jana, Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Iringa, alisisitiza kwamba chama
kitamwadhibu bila huruma mwanachama yeyote anayejipitisha katika maeneo
mbalimbali na kufanya kampeni za kuwania urais kabla ya wakati. Akifunga mafunzo ya makatibu na
wenyeviti wa wilaya na mikoa mjini Dodoma mwaka jana, Rais Kikwete alisema kuwa
inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa
viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague
katika nafasi mbalimbali za urais ama bunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa
wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali
za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi
chama hicho. Mangula akizungumzia uchaguzi wa
serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu alisema, viongozi wote wanatakiwa
kufuata taratibu na kanuni na kujiepusha na vitendo vya rushwa. “Vitendo vya rushwa ndio
vilitufanya katika chaguzi zilizopita kufanya vibaya, watu walinunuliwa kadi,
sasa viongozi wa matawi wawe makini tusirudi tulikotoka na tukibaini mtu
hafuati kanuni tutamwajibisha,” alisema Mangula.
No comments:
Post a Comment