Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa
Mahakama Kuu haikuzuia kikao cha Kamati Kuu yake kujadili mambo mengine
yanayomhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe bali uanachama wake
pekee. Juzi mahakama hiyo iliweka zuio, ikitaka chama hicho kupitia
kikao hicho kutojadili ajenda zozote zinazomhusu Zitto, ambaye ni Mbunge wa
Kigoma Kaskazini. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji John Utamwa, baada ya kupokea
maombi ya Zitto kupitia wakili wake, Albert Msando kukata rufaa yake
iliyowasilishwa Baraza Kuu la Chadema kusikilizwa kwanza, kabla ya kufanyika
uamuzi mwingine. Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuanza
kwa kikao hicho cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano
na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema: “Kuna watu walipotosha amri
iliyotolewa na mahakama… Ilitoa zuio la kujadili uanachama wa Zitto, lakini
haikuzuia mambo mengine kujadiliwa.”
Mnyika alifafanua: “Baada ya wao kufungua kesi ya msingi kusema
Kamati Kuu isijadili masuala ya uanachama wake mpaka pale rufaa yake ambayo
bado hajaikata itakapojadiliwa, ameeleza tu kusudio la kutaka kuikata
itakapojadiliwa na Baraza Kuu.” Aliongeza kuwa jambo hilo liliwekewa pingamizi la awali na
mawakili wa chama hicho juzi na kwamba jana, walikuwa wakiandaa majibu ya
maswali yaliyofikishwa mahakamani na mpeleka madai (Zitto). “Suala la hatima ya uanachama wake ndiyo halitajadiliwa, lakini
jambo jingine lolote likijitokeza, Kamati Kuu ya chama ina haki ya kumjadili
mtu yeyote yule,” aliongeza Mnyika. Alisema kuwa mkutano huo utatangaza majina ya watu waliopelekwa
kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba. Aliongeza kuwa Bunge la Katiba linapaswa kuchukua maoni ya wananchi,
huku akiwalaumu baadhi ya viongozi wa CCM kwa kuanza kupinga pendekezo la
Serikali tatu.
“Tayari CCM imekwishatoa msimamo ambao baadhi yao wanauendeleza
wa Serikali mbili, wakati wananchi wameshasema Serikali tatu,” alisema. Mnyika alibainisha kuwa mkutano huo pia utajadili namna ambavyo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec), ambayo inalalamikiwa na chama hicho kupewa kazi
ya kusimamia uchaguzi na kwamba chama hicho kinawasiwasi kuwa mchakato wa kura
ya maoni utakuwa shakani. “Bungeni
tulitaka Daftari la Kudumu la Mpigakura lingeboreshwa, lakini baadaye
tulipomaliza Bunge, tume ikasema halitaboreshwa,” alisema Mnyika.
Hali ilivyokuwa eneo la mkutano
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, wajumbe walionekana wakiwa na
furaha huku wakizungumza katika makundi makundi nje ya ukumbi. Wajumbe hao walipoingia ndani waliwataka waandishi wa habari
kuingia kupiga picha, kisha kutoka nje kwa kuwa hawakuruhusiwa kusikiliza. Saa 7:27 mchana, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Samson
Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu, Dk Kitila Mkumbo waliwasili
katika eneo la mkutano, huku wakipokelewa na Mwenyekiti wa Bazara la Vijana
Chadema (Bavicha), John Heche na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama
hicho, Willfred Lwakatare na kuwaelekeza sehemu ya kukaa wakati wakisubiri
kuitwa ndani kwenda kujitetea. Zitto,
Mwigamba na Dk Kitila walivuliwa nyadhifa zao zote walizokuwa nazo ndani ya
chama hicho baada ya kubainika kuwa walikuwa wakiandaa waraka wa siri kwa ajili
ya kukihujumu chama hicho, ikiwamo kumng’oa mwenyekiti wake kinyume na
kanuni, sheria na Katiba ya Chadema.
No comments:
Post a Comment