HATUA ZA KINIDHAMU DHIDI YA WANACHAMA ZITTO ZUBERI
KABWE, DR. KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA
UTANGULIZI
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya
utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama
yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe,
aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba. Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar
es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati
Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi ya
CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha, Kamati
Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya kuizuia
Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua suala la
uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya Mahakama Kuu, Kamati
Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote watatu walishtakiwa jumla ya
mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama,
Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na
Maadili ya Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi
za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na
watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama ifuatavyo:
Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti
wa Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na
vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao
wa Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;
Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na
bila kupitia vikao halali vya Chama;
Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila,
udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa
jamii;
Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha
au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa
Mwongozo wa Chama;
Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania
uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au
kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa
Chama;
Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi
ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;
Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge
kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha
Kanuni za Maadili ya Wabunge.
UTETEZI WA WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya
utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito
wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele yake. Hata hivyo, siku ya utetezi
wao, ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na
kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri
kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr.
Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba – alikanusha na kukataa
tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na Mwongozo wa Chama. Kwa
maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla
wake dhidi ya[ke]”, na kwamba mashtaka hayo sio ya kweli na hakuvunja Katiba,
Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha, licha ya kukiri kwake katika kikao cha
Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni
pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia
Kamati Kuu kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa
wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na
Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana
Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba
anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi
atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA
MABADILIKO
Itakumbukwa kwamba katika kikao cha Novemba 2013,
Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto
Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko. Aidha, Zitto Zuberi
Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara
ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani
tangu avuliwe nafasi zake za uongozi. Hata hivyo, wakati wa mahojiano na
wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba yeye na waandishi
wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing juu ya Mkakati na kwamba
alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya baruapepe
iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’
tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya
Novemba iliyowavua madaraka.
Zaidi ya hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama
juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba
mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa
kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata kujadili
suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao kwa Msajili wa
Vyama vya Siasa.
Kuhusu tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu
wa fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi
wa Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya
viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha
zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na
Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo
alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee Jaffer Sabodo
na michango mingine ya watu binafsi zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake
kuwasilishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi
Kabwe.
Zaidi ya hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za
manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na
jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao
wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo
alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa
namna yoyote ile katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha
saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo. Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza
kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi
wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao
ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu
wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka
kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr. Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la
kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI YA KAMATI KUU
Baada ya kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na
baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba
Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe
kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na
malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa wananchi na
kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni
kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa
juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la
ukombozi.
Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali
mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake
wakitumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba
mkakati wa kukibomoa Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu. Mkakati
huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika
chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma
Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.
Kwa sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia
ifuatavyo:
Kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila
Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA); na
Kwamba, kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki
Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile
Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote
linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama,
wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na
nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya
nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto
Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.
--------------------------------
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment