WAJUMBE wa mdahalo wa kupitia rasimu ya Katiba mpya,
wamependekeza katiba hiyo, itoe fursa kwa vyama vya watu walio na ulemavu
kuchagua wawakilishi wao bungeni, badala ya wabunge hao kuteuliwa na Rais. Mapendekezo hayo yalitolewa na wajumbe hao juzi,
katika mdahalo uliofanyika katika kijiji cha Milanzi wilayani Sumbawanga, ulioandaliwa
na asasi ya Vijana wa Kupambana na Maendeleo Rukwa (VIPAMARU), kwa ufadhili wa
The Foundation For Civil Society. Mmoja wa wajumbe hao, mwalimu Thomas Sepe, ambaye
pia ni mlemavu wa macho, alisema kutokana na majukumu mengi aliyonayo Rais, ni
vigumu kuwatambua walemavu walio na sifa stahiki ya kuwakilisha wenzao.
Sepe aliwataja walemavu waishio maeneo ya pembezoni
kuwa miongoni mwa wenye uwezo lakini ni vigumu kuteuliwa na Rais kwa kuwa ni
vigumu sifa zao kumfikia. Alisema kuvipa majukumu vyama vya walemavu kuchagua
wawakilishi kutatoa fursa kwa walemavu walioko pembezoni kushiriki kwenye
mchakato huo na kuwezesha kupatikana kwa wawakilishi walio na sifa zinazoweza
kuitetea jamii hiyo. Katika kujadili rasimu hiyo ya katiba, wajumbe wa
mdahalo huo pia walilalamikia hatua ya nakala za rasimu kutokuwa na dibaji ya
kumwezesha msomaji kujua jambo analohitaji linapatikana katika ukurasa upi.
Changamoto nyingine iliyobainishwa na wajumbe hao ni
kukosekana kwa tafsiri za misamiati iliyopo katika rasimu ya katiba. Walisema
hali hiyo inasababisha wasomaji kushindwa kupata maana halisi ya baadhi ya
vipengele vya rasimu hiyo. Mmoja wa washiriki, Willy Nsalanga alipendekeza
katiba ijayo iongeze kuwepo na siku tisini kati ya siku ya kutangazwa kwa
mshindi wa urais hadi siku ya kuapishwa ili kutoa fursa kwa wanaopinga ushindi
wake kuchukua hatua stahiki.
Source: Nyambo J. (Sept. 2013). 'Hatutaki Rais ateue wabunge wetu'. Sumbawanga. Retrieved from HabariLeo
No comments:
Post a Comment