WAJUMBE wa baraza la katiba la mashirika yasiyo
ya kiserikali wilayani Masasi mkoa wa Mtwara, wameshauriwa kuacha itikadi za
kidini na kisiasa, wanapotoa maoni yao kuhusu maudhui yaliyomo kwenye rasimu ya
Katiba. Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Katibu
Tawala wa wilaya ya Masasi, Yohana Miwa. Alisema hayo alipokuwa akifungua
mkutano wa siku tatu wa baraza la kujadili rasimu ya Katiba. Akizungumza katika ufunguzi wa baraza hilo,
lililoandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wilayani Masasi
(Mangonet) kwa ufadhili wa taasisi ya The Foundation For Civil Society, Miwa
alisema rasimu hiyo ya Katiba ni ya kitaifa, haipaswi kuchukuliwa ya kidini.
Alisema wajumbe wakifanikiwa kuweka kando
itikadi zao za dini na za kisiasa, watafanikiwa kupata Katiba itakayokidhi
maslahi ya Watanzania wote na taifa. Miwa alisema mikutano hiyo ya utoaji wa maoni ya
rasimu ya Katiba, inapaswa kutumika kutoa maoni ya msingi yatakayo saidia
kupata katiba iliyo bora kwa taifa na kupiga hatua mzuri ya maendeleo bila
kuwepo kwa mivutano kuhusu dini ama siasa. Kwa mujibu wa Miwa, lengo la mikutano hiyo ya
mabaraza ya utoaji wa maoni ya rasimu ya Katiba ni kutoa ushirikishwaji ili
kupata katiba yenye maslahi na haki kwa ajili ya taifa na si chama cha siasa
ama tasisi ya dini. Mwenyekiti wa Mangonet, Bernadetha Jumla alisema
mkutano huo una lengo la kushirikisha jamii kuweka miundombinu na mifumo ya
utawala bora na utawala wa sheria kuwa wa kidemokrasia na shirikishi.
Alisema washiriki wa mkutano huo ni wawakilishi
wa asasi za kiraia na asasi zisizo za kiserikali wilayani Masasi na watu wenye
mahitaji maalumu wa jinsia zote na pia mkutano huo, utaongeza ufahamu wa
wananchi kuhusu haki zao za msingi na uwajibikaji. “Mkutano huu ni mwanzo wa shughuli
kubwa ya kuandika Katiba mpya shirikishi…tunategemea mchakato huu utaongeza
idadi ya wananchi ya kujua haki zao za msingi…uwajibikaji…ushiriki wa shughuli
za maendeleo hii itapunguza ama kuoandoa migogoro ya majukumu baina ya viongozi
na wananchi,”alisema Jumla.
Source: Simba H. (Sep. 2013).‘Acheni itikadi mnapotoa maoni ya Katiba’.Retrieved from HabariLeo
Source: Simba H. (Sep. 2013).‘Acheni itikadi mnapotoa maoni ya Katiba’.Retrieved from HabariLeo
No comments:
Post a Comment