Wazo Langu: Lyatuu Lucy
JUMAMOSI iliyopita ilikuwa siku ya mwisho ya mabaraza yote kuwasilisha maoni na mapendekezo yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ambayo yalilenga kuboresha yale yaliyotolewa na kuhakikisha Rasimu ya Katiba mpya itakidhi matakwa ya wananchi walio wengi. Katika hatua hiyo ya kuwasilisha mabaraza mbalimbali yalipeleka mapendekezo yao huku wengine wakipata fursa ya kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwepo mapungufu na hata wengine kuzungumzia mapendekezo yao ambayo yalifanikiwa kuingizwa katika rasimu hiyo. Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa masuala mbalimbali ambayo awali yalitolewa kama mapendekezo kutoka kwa wadau lakini pia wadau hao hao walikusanyika kwa nyakati tofauti na kuanza kuzungumzia mapungufu ambayo kwa awamu nyingine yaliwasilishwa ili kuboresha rasimu hiyo.
Aidha, katika mikusanyiko hiyo ya Rasimu baadhi yao walionekana wakiwakemea kwa nguvu kubwa wanasiasa kuingilia mchakato huo huku wakiwasilisha yale ambayo walifikiri yana faida kwao huku wakisahau maslahi ya wananchi walio wengi. Miongoni mwa waliokuwa wakizungumzia sana hatua ya wanasiasa kuingilia mchakato huo ni pamoja na asasi mbalimbali za kiraia ambapo zilifika mbali zaidi na kuwataka wananchi kuwa macho pindi rasimu hiyo itakapofika katika Bunge la Katiba kuhakikisha idadi ile ya wajumbe wanaotakiwa kushiriki katika Bunge hilo kutoegemea zaidi kwa wanasiasa. Aidha wadau hao walitoa mwito kwa Serikali kutazama kwa jicho la huruma kuhusu idadi hiyo ya wajumbe ambao wengi wao wanahisiwa kuwa ni wanasiasa ambao kwa namna yoyote ile lazima yale mapendekezo ambayo yatawanufaisha wao lazima yatazingatiwa zaidi ya wengine.
Katika kuliona hilo na kulikemea pia, msomi na mchambuzi mahiri wa masuala ya siasa, Profesa Mwesiga Baregu amekemea uamuzi wa baadhi ya vyama vya siasa nchini kuunda mabaraza yao ya Katiba na kutoa mapendekezo ya Rasimu kwamba hatua hiyo ni kuingilia uwakilishi wa wananchi walioteuliwa kuunda mabaraza hayo. Kadhalika Profesa Baregu alisema mabaraza hayo ya Katiba yaliundwa kwa ajili ya wananchi na si vinginevyo ambapo yatatangulia kabla ya Bunge maalumu la Katiba ambapo wananchi watatoa maoni yao kuhusu ugumu wa maisha, matakwa halisi ya wananchi huduma muhimu za nishati ya umeme, maji pia migogoro ya wakulima na wafugaji. Kulingana na umuhimu huo wa mabaraza ya Katiba yalitakiwa kutoa mapendekezo ya wananchi waliowatuma na matakwa yao ambayo yanahitaji Katiba hiyo iwe ya namna gani na ambayo hata wananchi wengi walio vijijini wataweza kuona mabadiliko.
Ikumbukwe kuwa kama wanasiasa wataingilia mchakato huo na kutoa mapendekezo ambayo yatalenga kuwanufaisha wao peke yao huku wakisahau kuwatetea wananchi basi watambue kuwa vizazi vijavyo vitawahukumu kwa hilo badala ya kuwapongeza kwa kazi nzuri watakayokuwa wamefanya. Kutokana na umuhimu wa Katiba ni vyema wanasiasa wangepisha mchakato huo si kwa sababu wao sio Watanzania la hasha wao wangejadili kwa namna ya kuwasaidia wananchi kuhakikisha ndani ya Katiba hiyo wananchi watakuwa na mfumo ambao utawawezesha kunufaika na rasilimali zilizopo nchini. Ni kwa kuzingatia umuhimu huo wa Katiba, Tume ya Mabadiliko kuhakikisha kuwa wakati wa kuchambua maoni hayo kutazama zaidi yale ambayo yanalenga kuwasaidia wananchi badala ya kuegemea yale ya wanasiasa ambayo yanaweza kuwa katika mfumo ambao utawanufaisha wao peke yao.
No comments:
Post a Comment