TANZANIA inadaiwa kupoteza takribani Sh trilioni 3.2 kila mwaka kutokana na fedha haramu ukiwemo utoroshwaji wa fedha. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto alisema nchi za Afrika kwa ujumla zinapoteza zaidi ya Sh trilioni 1.1 kutokana na vitendo hivyo. Zitto alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Kamati za Mabunge za Hesabu za Serikali kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Alisema fedha hizo zinapotea kutokana na udanganyifu wakati wa kuuza mazao nje ya nchi pamoja na watu wasio waaminifu kuficha fedha kwenye benki zilizo nje ya Afrika.
Alifafanua kuwa fedha zinazoingia Afrika kama msaada ni zaidi ya Sh trilioni 40 na Sh zaidi ya trilioni 40 ni kwa ajili ya uwekezaji wakati zinazotoroshwa nje ni zaidi ya Sh trilioni 700. Alisema hata zikifuatiliwa kwenye benki husasan Benki Kuu ya Tanzania (BoT) si rahisi kugundulika. Alisema fedha hizo hazigunduliki mapema kwa sababu wafanyabiashara wanaosafirisha mazao nje ya nchi hutoa ripoti tofauti na mazao wanayonunua na kupeleka nje, hivyo kutokana na hali hiyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeingia mkataba na taasisi ya Norway kudhibiti upotevu wa fedha pamoja na biashara za mazao zinazopelekwa nchi za nje. Akitoa mfano wa upotevu huo Zitto alisema walifanya uchunguzi wa korosho zilizouzwa India na kugundua kuwa kabla ya kusafirishwa Tanzania korosho hizo zilikuwa ni tani 80,000 ambazo ziliuzwa nje kwa dola 80,000 ambapo Benki ya Dunia inaonesha kuwa korosho zilizouzwa India zilikuwa tani 120, 000 kwa dola 120,000 hivyo kwa zao hilo Tanzania inapoteza dola 40,000 na kwa mazao yote hupoteza zaidi ya dola bilioni mbili.
“Endapo Afrika itaweza kudhibiti nusu ya fedha hizo kutoroshwa hatutakuwa na tabia ya kuomba misaada nchi za nje na ndio maana tunakutana hapa kujadili kwa pamoja jinsi ya kudhibiti wimbi la utoroshwaji wa fedha hizo nje ya nchi pamoja na kuhakikisha fedha zinazotengwa zinafanya kazi yake na kusimamiwa kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema. Naye Mwenyekiti wa Umoja huo kwa nchi za SADC, Sipho Makama wa Afrika Kusini alisema mkutano huo wa siku sita utajumuisha kamati mbalimbali na wakaguzi wa hesabu wa nchi wanachama, nchi marafiki na wafadhili. Rais, Jakaya Kikwete ndiye atakayefungua mkutano huo utakaoanza Septemba 2 jijini hapa.
Source: Mheta V. (September 2, 2013). Fedha haramu zaipotezea Tanzania trilioni 3.2/-. Retrieved from HabariLeo
No comments:
Post a Comment