UKUAJI wa uchumi umetajwa kutokuwa na uhusiano na uondoaji wa umasikini miongoni mwa wananchi. Mkurugenzi wa Mipango wa Taasisi ya Tafiti za Uchumi na Jamii (ESRF), Dk Tausi Kida, aliwaambia wabunge juzi mjini Dodoma kwamba watu wengi wamekuwa na dhana kuwa ukuaji wa uchumi unakwenda sambamba na maendeleo ya jamii. “Ndio maana ukiangalia nchi kama yetu pato la taifa linakuwa, lakini pato la mwananchi wa kawaida na maendeleo yake halikui,” alisema. Akitolea mfano Tanzania alisema pamoja na uchumi kukua kwa asilimia saba lakini imepunguza idadi ya wananchi kuishi kimasikini kwa asilimia 34, na matarajio ni kuwa ifikapo mwaka 2015 watakaoishi kwa kipato cha chini watapungua hadi kufikia asilimia 20.
Alisema ingawa mikakati ya kupanga maendeleo ya wananchi inaonekana utekelezaji wake ni rahisi, lakini dhana kubwa ni kuwaweka walengwa katikati ya mipango itakayowaletea maendeleo kwa kuishirikisha jamii katika uchumi endelevu. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mchakato wa ripoti ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania, kwa niaba wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa, Shamsa Vuai Nahodha alisema itasaidia Serikali katika ufuatiliaji wa sera na mikakati ya taifa ya maendeleo. Alisema kwa sasa Serikali inatekeleza mikakati ya Taifa ya maendeleo hadi mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo kuanzia 2011-2015 na awamu ya pili ya Mpango wa Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta).
“Kama mnavyojua hatuwezi kutekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi bila ya kuwa na ufuatiliaji na tathmini ya uhakika,” alisema. Alisema kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi kubwa ya kuwaletea maendeleo na kupunguza umasikini kwa wananchi lakini haijaweza kuwakomboa kwa kiwango cha juu dhidi ya umasikini uliokithiri. “Tumebaini kwamba zipo kasoro hasa katika utekelezaji wa mipango hiyo ya kuwaletea maendeleo Watanzania na kwa kutambua udhaifu huo, Serikali yetu ikiwa ni pamoja ya kuanzisha jitihada zinazojulikana kama matokeo makubwa sasa,” alisema. Kwa mujibu wake mchakato wa ripoti ya binadamu ya maendeleo itakuwa nyezo muhimu kwa Serikali kufuatilia na kuimarisha maendeleo. Pia inaonesha mbadala wa kufikia malengo ya kisera pamoja na kushawishi mabadiliko katika kufikia malengo ya kisera.
Ripoti itaibua mawazo mapya ya maendeleo na kuleta chachu na msukumo mpya katika utekelezaji wa mambo ya maendeleo. Nahodha alisema miaka iliyopita Tanzania ilipiga maendeleo kutokana na vita dhidi ya ujinga, umasikini na maradhi. “Leo miaka 30 imepita, nchi yetu imerudi nyuma hasa katika suala la ujinga ambapo ripoti zinaonesha kuwa asilimia 70 ya watu wazima hawajui kusoma na kuandika ikiwa ni chini ya asilimia 80 iliyowekwa na mkukuta,” alisema. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Mambo ya Kijamii (ESRF) Dk Hossiana Lunogelo alisema utayarishaji wa mikakati ya taarifa ya maendeleo, unaotegemewa kukamilika mwaka 2014.
Alisema ripoti hiyo itakuwa na mtazamo wa kisekta kama elimu, gesi na nyinginezo kuangalia kwa namna gani zitatumika kupata maendeleo ya wananchi na kuangalia maono ya nchi kwa miaka ijayo. Alisema ripoti hiyo pia itatoa mapendekezo ya kisera kwa Serikali kujua cha kufanya kukuza maendeleo ya wananchi wake.
Source: Anyimike A. ( September 2, 2013).'Ukuaji wa uchumi hauna uhusiano na uondoaji umasikini'. Dodoma. Retrieved from HabariLeo
No comments:
Post a Comment