Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, August 20, 2013

Wakati wa Bunge kuhoji matumizi ya fedha dhidi ya dawa za kulevya



Na Zitto Kabwe

KAMATI za Bunge za Hesabu ni asasi muhimu za Bunge katika kuhakikisha serikali inawajibika kwa wawakilishi wa wananchi. Majukumu ya kamati hizi yameainishwa na Kanuni za Bunge, nyongeza ya nane. Nyaraka muhimu na ya kwanza katika kazi za kamati za kusimamia hesabu ni ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Hivyo Kamati za Bunge za Hesabu pamoja na CAG, wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa. Ndiyo maana bajeti ya CAG inapitishwa na PAC na ikishapitishwa hakuna mamlaka ya kuhoji tena. Vile vile PAC ndio Kamati yenye mamlaka ya kuteua mkaguzi wa hesabu za ofisi ya CAG.

       Ni wajibu wa Kamati za Bunge za Hesabu kulisaidia Bunge katika kuiwajibisha serikali. Mara kadhaa kumekuwa na maelezo kwamba kazi ya Bunge ni kuishauri serikali, hapana. Katika kuisimamia serikali ndani yake kuna ushauri hivyo ushauri haupaswi kuwekewa mkazo zaidi ya usimamizi. Warasimu wa serikali wanapenda neno ushauri na kuchukia neno usimamizi. Wabunge hawapaswi kuingia katika mtego wa ‘kazi yao ni kushauri’ kwani huo ni mtego uliotegwa na warasimu ili kupunguza nguvu ya Bunge. Kazi ya Bunge ni kusimamia serikali.

     Kamati za Bunge za Hesabu ndizo zenye kubeba mzigo huo mkubwa kwa niaba ya Bunge na kwa hiyo, uadilifu ni jambo la msingi katika wajibu huu. Vile vile ndio maana ni rahisi kuona Kamati za Hesabu zikipewa kila aina ya shutuma kutoka kwa wasimamiwa na wakati mwingine kwa kuwatumia baadhi ya wabunge kwa kujua au kutokujua. Wakati mwingine Kamati za Bunge huambiwa kuangalia ‘mahesabu tu’ basi. Ni wajibu wa Kamati za Bunge kuangalia hesabu za umma na kuona kama matumizi ya fedha za umma yanafanikisha malengo yaliyotarajiwa (performance audit).

       Itakuwa ni wendawazimu kwa kamati kuridhika kwa kuangalia tu mizania ya serikali au mashirika ya umma au serikali za mitaa. Kwa mfano, ni wajibu wa kamati kuangalia kama fedha zilizotolewa kwa ujenzi wa barabara zimetumika kwa kazi hiyo. Ni wajibu zaidi wa kamati kuangalia kama gharama hiyo iliyotumika kujenga barabara husika ndio gharama halisi na sio kwamba imezidishwa ili kunufaisha watu wachache. Ni wajibu mkubwa zaidi wa kamati kuangalia kama barabara hiyo imejengwa kwa kiwango kinachotakiwa. Hii inaitwa ‘value for money’. Katika utendaji wa kazi hizi ni muhimu na lazima, Kamati za Bunge kutumia kwanza taarifa ya CAG. Hata hivyo, kamati pia zinaweza kutumia taarifa kutoka vyanzo vingine mbalimbali kama wananchi na vyombo vya habari, katika kufikia malengo ya kuchunguza.

      Kwa mfano, hivi karibuni moja ya magazeti hapa nchini yaliandika kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika mkutano wa Smart Partnership, kwamba takribani shilingi bilioni nane zimefanyiwa ufisadi. CAG amenukuliwa akisema hajapata barua yoyote inayomwomba (CAG haagizwi, anaombwa) kufanya ukaguzi maalumu wa mkutano ule. Kamati ya Bunge ya PAC inaweza kutumia mamlaka yake kumwomba CAG kufanya ukaguzi maalumu na kuwasilisha matokeo yake kwenye kamati na hatimaye bungeni. Iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilifanya wajibu huu vizuri kwenye suala la nyumba ya Gavana wa Benki Kuu na kutokana na ukaguzi huo hoja ile ilifungwa.

     Ili kutekeleza wajibu huu muhimu wa uwajibikaji, Kamati za Bunge za Hesabu ni lazima ziwezeshwe vya kutosha kwa mafunzo ya ujuzi (skills) na maarifa (knowledge). Bila ya kuwa na uelewa mpana wa mambo kamati hujikuta zikifanya uamuzi wenye madhara makubwa kwa taifa. Katika kutekeleza wajibu, ni muhimu na lazima wajumbe wa kamati kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani vitendo hivyo huzuia usimamizi na hatimaye kuendeleza rushwa kwa wanaosimamiwa. Uwajibikaji ni silaha dhidi ya rushwa na hivyo wanaosimaima uwajibikaji ni lazima wawe wasafi, wao binafsi kwanza kabla ya kusafisha walio wachafu. Uadilifu ni msingi muhimu katika kujenga uwajibikaji. Bila ya uadilifu hakuna uwajibikaji na vile vile kukosekana kwa uwajibikaji humomonyoa utamaduni wa uadilifu katika jamii.

Mambo gani ya kuzingatia?

       Tumeona wajibu wa Kamati katika kusimamia uwajibikaji wa serikali. Baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia ni katika utekelezaji wa wajibu huu ni; moja, pamoja na matumizi yote ya serikali ambayo kamati husimamia, kuna matumizi ambayo inabidi kuweka msisitizo maalumu. Kati ya matumizi hayo ni pamoja na deni la taifa. Katika ripoti ya CAG ya mwaka 2012, hoja za kuhusu deni la taifa zimeendelea kutokana na kasi ya ongezeko lake. Kamati inapaswa kufahamu kwamba mzigo mkubwa wa deni hilo ni katika kulipa kwa kutumia fedha nyingi za umma. Kila mwaka bajeti ya kuhudumia deni la taifa huwa ni moja ya bajeti kubwa zaidi ya bajeti nyingine zote. Kwa mfano mwaka 2012/13, serikali ilitenga takribani shilingi trilioni mbili kuhudumia deni hilo pekee ilhali robo tu ya fedha hizo ilitengwa kwa ajili ya Wizara ya Afya.

     Kamati zinapaswa kukagua kwa kina na kila wakati matumizi ya mikopo ili kuhakikisha inatumika kujenga uwezo wa nchi kuzalisha rasilimali za kuhudumia mikopo hiyo kwa kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuongeza kodi. Pili, makusanyo ya kodi ya serikali. Bunge hupitisha fedha kuwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi. Hivi sasa ni takriban Watanzania milioni moja tu wanalipa kodi (kwa maana ya watu binafsi walio kwenye mfumo rasmi).

     Hivyo tuna wigo mdogo sana wa kodi wakati tunatumia fedha nyingi kukusanya kodi hiyo kidogo. Ni wajibu wa kamati kuona kwamba ufanisi katika kukusanya kodi unafikiwa, sambamba na kuzuia mianya ya ukwepaji wa kodi. Kwa mujibu wa TRA, asilimia 15 ya makusanyo yanayotarajiwa huwa hayakusanywi kwenye idara ya mapato peke yake kutokana na ukwepaji wa kodi. Hii ni sawa na takribani shilingi bilioni 490 kwa kutumia makadirio ya mwaka wa fedha 2012/13.

     Wakati Bandari ya Dar es Salaam inapakua makontena 600 kwa zamu (shift), kuna wakala wa upakuaji (clearing and forwarding agents) wa idadi hiyo hiyo katika Bandari hiyo. Haiwezekani kuwe na wastani wa kontena moja kwa kila wakala. Eneo hili linahitaji jicho pevu kutoka Kamati za Bunge na CAG. Ukwepaji kodi wa kampuni za kimataifa pia ni ajenda kubwa ambayo kila mara kamati inapaswa kuizingatia ili kuzuia. Kamati ya PAC tayari imepitisha mapendekezo ya ukaguzi wa misamaha ya kodi na kuiweka wazi (audit of tax exemptions and transparency).

     Ni matarajio kwamba kwenye ripoti ya CAG kwa mwaka unaoishia Juni 2013, Watanzania wataona taarifa ya ukaguzi wa misamaha ya kodi. Tatu, ukaguzi wa mikataba na taratibu za ununuzi. Hili ni eneo ambalo limekuwa chanzo kikubwa cha ubadhirifu nchini. Ni muhimu kila mara kamati kuzingatia eneo hili katika kazi zake. Eneo hili linaathiri zaidi mamlaka za serikali za mitaa, udokozi umekuwa kama utamaduni na hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

     Ni muhimu kamati kuhitaji mara kwa mara ukaguzi maalumu kwenye masuala ya ununuzi ili kujenga uwajibikaji katika eneo hilo na kuepusha hasara kubwa kwa nchi. Nne, hivi sasa nchi yetu imekuwa kitovu cha biashara ya dawa za kulevya. Vijana wa kitanzania wamekuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali duniani wakihusishwa na biashara ya dawa za kulevya. Moja ya njia ya kupambana na uharamia huu ni uwajibikaji wa mamlaka zenye wajibu wa kupambana na dawa za kulevya.

      Hivyo, Kamati za Bunge zihoji katika hesabu za mamlaka hizo matumizi ya fedha za umma katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya ilhali biashara hiyo inazidi kushamiri. Iwapo tutaiwajibisha Wizara ya Mambo ya Ndani, kitengo cha kupambana na dawa za kulevya tutakuwa tumechangia katika vita hii. Hatuwezi kuendelea kutenga fedha kila mwaka dhidi ya biashara hii haramu lakini bado inazidi kushamiri. Kila mwenye wajibu awajibishwe.

      Jambo jingine ni kuhusu ukaguzi wa mchakato wa ubinafsishaji. Bado sera ya ubinafsishaji inatekelezwa na serikali. Ni wajibu wa CAG kukagua mchakato wa ubinafsishaji na Kamati za Bunge kusimamia uwajibikaji katika mchakato huo. Ubinafsishaji ni uuzaji wa mali ya umma, hivyo ni lazima upate usimamizi kamilifu. Kwa kuhitimisha, nieleze kwamba Kamati za Bunge za Hesabu ni asasi muhimu za demokrasia kwa sababbu husimamia uwajibikaji. Ni vema kamati hizi kupewa uzito stahili kwa kuwa na rasilimali za kutosha katika kufanya kazi zake na kuhakikisha taarifa zake zinapata uzito katika utekelezaji.

     Kimsingi kamati zote za Bunge ni sawa kwa hadhi lakini Kamati za Hesabu ndio Bunge kwa uhalisia.

No comments: