Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, August 15, 2013

Mzozo mpya CCM

MWENYEKITI WA MKOA AMVAA NAPE, ASISITIZA KUTOTAMBUA MADIWANI WANANE


      CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeingia katika mzozo mpya wa vikao vya chini kupinga uamuzi wa vikao vya juu, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya chama hicho. Mzozo huo umehusisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Constancia Buhiye, na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambaye kikatiba ndiye msemaji wa chama. Baada ya Nape juzi kusitisha uamuzi wa NEC Mkoa wa Kagera kufukuza madiwani wanane, jana Buhiye aliita waandishi wa habari mjini Bukoba na kuwaeleza kuwa hatambui kauli ya Nape. Alisisitiza kuwa hata kama Nape alitangaza kusitisha uamuzi wa mkoa kuwavua uanachama wa CCM madiwani hao, na kuwataka waendelee na kazi zao hadi vikao vya juu vitakapojadili suala lao na kutoa uamuzi, msimamo wa NEC Kagera ni kwamba waliofukuzwa wamefukuzwa, si madiwani tena.

        Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Nape alisema CCM Taifa imeagiza madiwani hao wanane waendelee na kazi zao za udiwani kama kawaida, huku wakisubiri uamuzi wa Kamati Kuu ambayo imeamua kuweka ajenda yao kwenye kikao hicho kitakachofanyika Dodoma Agosti 23. Nape alifafanua kuwa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola hasa wabunge na madiwani, uamuzi wa NEC mkoa si wa mwisho, kwani unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu ndipo utekelezwe. Hata hivyo, Buhiye alisema kuwa chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa taratibu, miiko, kanuni, katiba na miongozo, hivyo uamuzi uliotolewa na NEC mkoa juzi ulikuwa halali kwa sababu ulitolewa kwenye kikao halali.

      Alipoulizwa kama haoni msimamo wake unapingana na wa chama makao makuu, Buhiye alidai kuwa hakumsikia Nape akitoa kauli hiyo, na kwamba hawezi kuitoa. Alisisitiza kuwa hata kama ni kweli Nape alitoa kauli hiyo, msimamo ni kwamba madiwani wameshafukuzwa. Buhiye alisisitiza kuwa hajapata barua ya Nape kumweleza uamuzi wa taifa na wala hajamsikia kwa masikio yake kupitia kwenye vyombo vya habari akitengua uamuzi wao. “Kwa mujibu wa ibara ya 14 ya katiba ya chama ni kuwafukuza uanachama wanaokihujumu kwa namna yoyote na ibara ya 15 kuwavua uongozi ndani ya chama huku,” alisema. Aliongeza kuwa mkoa unayo haki ya kusimamisha mwanachama yeyote kwa kufuata muongozo wa vikao kuanzia ngazi ya chini kwa wale walioteuliwa na NEC.

       “Anayozungumza Nape ni yake na mimi nazungumza kwa niaba ya kikao cha NEC mkoa wa Kagera,” alitamba na kuongeza kuwa uamuzi wa mkoa hauwezi kutenguliwa na kikao chochote kwa mujibu wa katiba ya chama hicho isipokuwa kutolewa ushauri na uongozi wa juu. Alisema walitarajiwa kuifikisha taarifa ya uamuzi wao makao makuu ya chama jana kutokana wao kuchelewa kuituma. Uamuzi wa kufukuza madiwani ulifikiwa katika kikao cha NEC mkoa kilichoketi Jumanne jioni Agosti 14, lakini ulisitishwa siku moja baadaye kwa kigezo kuwa utaratibu wa kuwafukuza ulikuwa umekiukwa. Madiwani hao wanatuhumiwa kukisaliti chama kwa uamuzi wao wa kuungana na wenzao wa upinzani kusaini hati ya tuhuma za Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, wakitaka ang’olewe kutokana na kuiingiza halmashauri kwenye mikataba mitatu ya kifisadi.

       Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo. Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu. Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake. Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi wa kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.

Nape atoa msimamo

      Alipotafutwa kuzungumzia msimamo wa chama mkoa wa Kagera kupinga maamuzi ya taifa, Nape alisema hili si suala la kubishana kwenye vyombo vya habari sasa. “Nilichosema mimi ndio utaratibu wa chama unaopaswa kufuatwa wala si utaratibu wa Nape. Anayebisha anabishia katiba na kanuni za CCM hambishii Nape, na mimi ndiye msemaji wa chama,” alisema. Alipoulizwa kuhusu uvumi ulionezwa mjini Bukoba kuwa Makamu Mwenyekiti wa sasa, Philip Mangula, na mstaafu Pius Msekwa hawajapendezwa na uamuzi wake wa kubatilisha maamuzi ya NEC Kagera, Nape alisema, “Mangula na Msekwa ni wazee, wao ndio waliotunga kanuni na taratibu ambazo mimi nazitumia kuongoza, hawawezi kuzipinga kanuni walizozitengeneza wao.”

       Kuhusu msimamo upi sasa unapaswa kufuatwa na madiwani hao, Nape alisema kuwa msemaji wa chama ni yeye na kwamba maamuzi ya CCM Taifa yanapaswa yaheshimiwe. Katika hatua nyingine, madiwani hao nane walisema kuwa pamoja na makao makuu kutengua maamuzi ya awali, uongozi wa mkoa juzi jioni uliwakabidhi barua za kuwafukuza uanachama. Chanzo chetu kutoka ndani ya CCM zilidai kuwa mwenyekiti Buhiye amekuwa na visasi dhidi ya uongozi wa chama makao makuu baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ambayo sasa inashikiliwa na Prof. Anna Tibaijuka.

    Hivi karibuni akiwa mjini Bukoba, Rais Jakaya Kikwete alijaribu kuingilia kati mgogoro huo kwa kuwataka meya Amani na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki, kumaliza tofauti zao ili miradi hiyo iendelee kutekelezwa. Hata hivyo, ushauri wake ulipuuzwa na madiwani hao pamoja na wenzao wa CHADEMA na CUF wakisema tatizo si ugomvi kati ya wawili hao bali wanapinga ufisadi wa meya wao kuingia mikataba ya miradi bila kuwashirikisha.

Source: Isango J. (August 2013).Mzozo mpya CCM. Tanzania Daima

No comments: