Mkutano ulifanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Bernard K. Membe (Mb),
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kufunguliwa na mgeni
rasmi, Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mjumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Balozi wa
Tanzania nchini Misri na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mabalozi Wastaafu, Wafanyakazi wa
Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Wizara iliamua kuunda Baraza la Katiba kwa kuzingatia kuwa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni Wizara ya Muungano; Rasimu ya
Katiba imependekeza masuala ya Sera ya Nje kuendelea kuwa miongoni mwa masuala
ya Muungano; na kuwa yako masuala yaliyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba
ikiwemo mipaka, uraia na muundo wa muungano ambayo yanagusa majukumu ya Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
liliazimia mapendekezo yafuatayo katika maeneo ya Mipaka, Muundo wa Jamhuri,
Uraia wa Jamhuri na Sera ya Mambo ya Nje:-
1) Mipaka ya nchi iwekwe wazi mwishoni mwa Ibara ya 2 ili isomeke kama
ifuatavyo: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na
Zanzibar ikijumuisha ardhi, maziwa na sehemu yake ya bahari (Territorial
Waters) pamoja na anga kwa mujibu wa sheria za kimataifa;
2) Baraza pia lilipendekeza mabadiliko katika Muundo wa Jamhuri ya
Muungano kwamba Muundo wa Serikali Mbili uliopo, uendelee na kuboreshwa kwa
kuwekewa mifumo imara ya kisheria itakayoakisi maslahi ya pande zote mbili za
Muungano ili kupunguza changamoto na manung’uniko kutoka kwa wadau wa Muungano.
3) Kuhusu suala la uraia katika Jamhuri ya Muungano; Baraza
lilipendekeza kuwa suala la uraia wa nchi mbili kwa Mtanzania wa kuzaliwa
litamkwe Kikatiba na Raia huyo asipoteze uraia wake wa kuzaliwa kwa sababu ya
kupata uraia wa nchi nyingine. Uraia wa nchi mbili utatoa fursa kwa Taifa letu
kufaidika kimaendeleo kutokana na kutumia rasilimali za Watanzania walioko nje
ya nchi;
4) Kuhusu Uraia, Ibara ya 55(4) inayozungumzia kumpa uraia wa kuzaliwa
mtoto atakayekutwa ndani ya mipaka ya nchi yetu, ambaye wazazi wake
hawajulikani ni raia wa nchi gani, Baraza linapendekeza “….Uraia huo utasitishwa
endapo uraia wa asili (wa nchi nyingine) wa mtoto huyo utagundulika na
kuthibitishwa pasipo na shaka au kama itagundulika kuwa ulifanyika udanganyifu
wa kumtupa kwa makusudi mtoto huyo kwa nia ya kupata uraia wa Jamhuri ya
Muungano.”
5) Kuhusu Uraia wa kuandikishwa, Ibara ya 56(2), mtu aliyefunga ndoa na
raia wa Jamhuri ya Muungano anaweza kutuma maombi ya kuandikishwa kuwa raia wa
Jamhuri ya Muungano baada ya kuomba uraia wa Muda wa kuishi nchini kama
mwanafamilia wa ndoa (dependant) mpaka ndoa iwe imedumu kwa miaka kadhaa (miaka
itamkwe na sheria)”.
6) Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje; Baraza linapendekeza mabadiliko katika
Ibara ya 12 ya rasimu kwamba Misingi (Principles) ya Sera ya Mambo ya Nje
ijumuishwe badala ya majukumu ya Wizara kwa kuwa majukumu hubadilika na
nyakati. Aidha, Katiba ilielekeze Bunge litunge Sheria itakayosimamia
utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
7) Kuhusu Ibara ya 39 (3) inayohusu raia wa Tanzania kutokupelekwa nje
ya nchi kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote bila ya ridhaa
yake, Baraza linapendekeza Kifungu hicho kifutwe, kwa sababu kuna ugumu wa haki
inayotajwa kwenye Kipengele hiki kutekelezeka bila kuathiri wajibu ya kimataifa
wa nchi (international obligations) katika makosa ya jinai, kwa kuwa ni vigumu
sana kupata ridhaa ya mtuhumiwa kuhojiwa kwa makosa aliyoyatenda au
anayotuhumiwa kuyatenda.
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
No comments:
Post a Comment