John Tendwa alipaswa kuwa ameondoka
kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, tangu mwaka 2008, alipofikisha umri
wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Aliendelea kufanya kazi zake hata baada ya
muda wa mkataba wake alioongezewa kuwa umefikia mwisho, hivyo alikuwa anakalia
ofisi hiyo ya umma, kinyume cha sheria.
Ametumia muda huo wa miezi kadhaa,
aliokuwa anakalia ofisi ya umma kinyume cha sheria, kuropoka, kuharibu
demokrasia, kwa manufaa ya Rais Jakaya Kikwete na CCM. Kutokana na mwenendo
(maneno na matendo) wake mbovu, CHADEMA ilitangaza kutokumpatia ushirikiano
wowote, yeye kama Tendwa. Ikamtangaza kuwa adui wa demokrasia nchini.
Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa
ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta
CHADEMA na kufanikisha dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye.
Kuondoka kwa Tendwa hakuzuii
kutekelezwa kwa mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
iliyomkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Sensa,
hivyo akasababisha kutokea kwa mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi,
Nyololo, Iringa.
Hivyo CHADEMA, kupitia Kurugenzi ya
Habari na Uenezi, inataka kauli ya Rais Jakaya Kikwete juu ya utekelezaji wa
mapendekezo hayo kwa Tendwa watu wengine, akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na wote waliotajwa katika ripoti hiyo ya
chombo cha serikali, kuwa walivunja sheria za nchi na kusababisha mauaji ya
mwandishi, raia asiyekuwa na hatia.
Tunamkaribisha 'with benefit of
doubt', msajili mpya, Jaji Francis Mutungi, kwenye kazi na majukumu yake mapya.
Wapenda demokrasia na maendeleo nchini, wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa
kuzingatia haki, sheria na utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa.
Kupitia mchakato wa Katiba Mpya
unaojadiliwa sasa hivi, CHADEMA tunapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru
zaidi na uteuzi wake, usiwe suala la Rais kuamka tu na kuamua kuteua bila
wahusika kuomba, kuchujwa na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na
iliyoteua.
Tunatambua kuwa msajili mpya aliwahi
kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, kwa muda mfupi, kisha akateuliwa kuwa Jaji
na akateuliwa pia nafasi zingine. Na sasa mwaka mmoja baada ya kutumikia nafasi
hizo, ameteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Jaji Mutungi, anapaswa kuonesha kwa
maneno na vitendo kwamba hatakuwa kama Tendwa, kwa kuanza kushughulikia matendo
ya kiharamia yaliyofanywa na Green Guards wa CCM kwenye chaguzi za madiwani,
zilizomalizika karibuni, ambazo si tu yalikuwa kinyume na Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai, ambayo Jeshi la Polisi wanatakiwa kuchukua hatua, bali pia
yalikuwa kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa. Hivyo yako kwenye mamlaka yake.
Jaji Mutungi, amshauri Rais Jakaya
Kikwete kushughulikia mapendekezo ya Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora, juu ya uvunjifu wa sheria wa wazi uliofanywa na askari polisi na
John Tendwa, hivyo kusababisha mauaji ya Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi,
Septemba 2, 2012, huko Nyololo, Iringa.
Aidha, Jaji Mutungi anapaswa
kumshauri Rais Kikwete kujibu na kufanyia kazi barua mbili alizoandikiwa na
CHADEMA juu ya kuunda Tume Huru ya Kimahakama/Kijaji, kuchunguza mauaji yaliyofanyika
kwenye shughuli halali za kisiasa za CHADEMA.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya
mauaji mfululizo mkoani Morogoro na Iringa, CHADEMA ilimwandikia barua Rais
Kikwete kumtaka aunde Tume ya Kimahakama kuchunguza utata wa vifo hivyo na
vingine kadhaa vilivyotokea kwenye shughuli halali za kisiasa, kwa mujibu wa
Sheria ya Vyama vya Siasa, ili ukweli ujulikane, haki itendeke na wahusika
wachukuliwe hatua, hadi sasa rais hajafanya hivyo.
Itakumbukwa pia kuwa baada ya mlipuko
wa bomu la Arusha, kwenye mkutano wa kampeni, CHADEMA pia ilimtaka Rais Kikwete
kutumia mamlaka yake kuunda Tume Huru ya Kimahakama, ili ushahidi juu ya tukio
hilo uwasilishwe, hadi sasa pia rais yuko kimya. Hivyo kwa nafasi yake, msajili
mpya atoe ushauri kwa rais kuchukua hatua hizo, ili vyama vitimize wajibu wa
kikatiba kufanya kazi zake kwa haki, uhuru na sheria za nchi zinazosimamia
shughuli za vyama vya siasa nchini.
Imetolewa Jumatatu, 5 Agosti, 2013
na;
Tumaini Makene
Ofisa
Mwandamizi wa Habari, CHADEMA
No comments:
Post a Comment