Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, August 5, 2013

Elimu: Majanga!



 
     Madudu zaidi yamebainika katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, baada ya kuwapanga baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano kwenye shule ambazo hazina masomo ya michepuo yao. Hii ni baada ya wanafunzi 1,189 waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule mbalimbali nchini kubadilishwa na kupangiwa shule nyingine. Kati yao, wanafunzi 865 wamepangiwa shule nyingine na 324 wamebadilishiwa shule kwa sababu walipangwa kwenye shule ambazo hazina michepuo ya masomo yao waliyotakiwa kwenda kusomea. Hayo yamebainika katika tangazo lililotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Mafunzo ya Ufundi kwenye tovuti ya wizara hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita.


    Tangazo hilo lilieleza kuwa baadhi ya wanafunzi hao wamebadilishwa michepuo (combination) na wengine shule, kwa sababu mbalimbali ikiwamo walioomba kubadili ambazo hazipo katika shule walizopangwa awali. “Wizara imepokea maombi ya wanafunzi wanaotaka kubadili shule au combinations, walizopangwa kwa sababu mbalimbali. Wizara imetafakari maombi hayo na kufanya mabadiliko kwa wanafunzi wenye sababu zifuatazo waliopangwa shule za kutwa mahali ambapo hawana pa kuishi; waliopangwa mbali sana kutoka sehemu wanazoishi; walio wagonjwa wanaohitaji kuwa karibu na hospitali; walioomba kuhamia shule za kutwa kwa sababu za kiuchumi na walioomba kubadili ‘combinations’ ambazo hazipo katika shule walizopangwa awali,” lilisema tangazo hilo.




    Tangazo hilo lilifafanua zaidi kwamba baada ya serikali kutangaza matokeo Julai 10, mwaka huu na kuwataka wanafunzi kuripoti kwenye shule walizopangiwa kabla ya Julai 29, mwaka huu, Wizara hiyo imepokea maombi ya wanafunzi kutaka kubadilisha shule au michepuo. “Wakuu wa shule wanaelekezwa kuwapokea wanafunzi hawa katika shule hizo mpya na kuwasiliana na wakuu wa shule walizopangwa awali ili wawatumie ‘Sel form’ za wanafunzi hawa.  Aidha, mnatakiwa kuhakiki uhalali wa kila mwanafunzi mnayempokea kwa kutumia orodha ya majina yaliyomo katika tovuti pamoja na Result Slip za wanafunzi hao.”

   “Wizara inawaagiza wanafunzi wote waliokubaliwa kubadilishiwa shule/combinations ambao taarifa zao zipo kwenye tovuti waripoti mara moja katika shule hizo. Wizara haitatoa barua kwa mwanafunzi yeyote.” Aliongeza  kuwa: “Kuanzia sasa Wizara haitapokea maombi yoyote ya kubadilisha shule/combinations. Endapo yatakuwepo maombi yo yote yafuate utaratibu wa kawaida wa uhamisho kupitia kwa wakuu wa shule.” Julai 10, mwaka huu, Wizara hiyo ilitangaza matokeo ya kupangwa kwa wanafunzi wa kidato cha tano waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na kuwahimiza wanafunzi kuripoti katika shule zao walizopangwa kabla ya Julai, 29, mwaka huu. Hata hivyo, hali ya kuripoti imekuwa ya kusuasua huku katika baadhi ya shule, wakiripoti nusu ya waliopangwa.

     Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano ni waliohitimu kidato cha nne mwaka jana. Matokeo ya kidato cha nne mwaka jana yaliibua mvutano mkali kati ya serikali na wananchi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kufeli vibaya. Wahitimu 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 walipata daraja la nne.
Matokeo hayo yalimlazimu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuunda tume ya kufanya uchunguzi ambayo hata hivyo, ripoti yake bado haijawekwa hadharani. Mbali ya matokeo mabaya ya mwaka jana, Wizara hiyo inakabiliwa pia na kashfa ya kukosekana kwa mitaala; hoja ambayo iliibuliwa na Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, wakati akiwasilisha hoja binafsi Bungeni Februari, mwaka huu.

     Hoja ya Mbatia ilikuwa ikieleza udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini unaosababishwa na kukosekana kwa mitaala rasmi katika shule za msingi na sekondari.  Hoja hiyo iliibua mvutano mkali kati ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali na kiti cha Spika, baada ya kiti kumzuia Waziri asiwasilishe mitaala hiyo bungeni jambo lililolazimu serikali kuja kuichapisha ‘chapchap’ Dar es Salaam. Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na wabunge wa CCM ambao waliikataa kwa kura za ndio huku wabunge wa upinzani wakiiunga mkono.


Source: James R. ( August 2013). Elimu: Aibu, aibu. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments: