KUMEIBUKA
ushindani wa vuta ni kuvute kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo wa
uenyekiti wa mtaa wa Luguruni, kata ya Kwembe, Dar es Salaam. Katika
uchaguzi huo uliofanyika Jumapili katika ofisi ya serikali za mtaa huo
ulionekana kuwa na dalili za upinzani mkali kutokana na vyama hivyo kila kimoja
kutamba kuibuka na ushindi. Tangu asubuhi vituo vya kupigia kura
vilionekana na makundi ya watu mbalimbali na kadiri muda ulivyozidi kwenda idadi
ya makundi hayo iliongezeka. Hali hiyo ilisababisa baadhi ya wakazi wa
mtaa huo kulalamika kuwa kuna baadhi ya watu ambao si wakazi wa mtaa huo
wamekwenda kupiga kura.
Katika uchaguzi
huo uliotawaliwa na vituko vya kila aina, kura zilipoanza kuhesabiwa, baadhi ya
wafuasi wa CCM wakianza kuimba na kushangilia ushindi kabla ya matokeo
kutangazwa huku wengine wakivua nguo hadharani. hali hiyo ilisababisha
ulinzi kuimarishwa kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi unamalizika kwa amani na
ilipofika majira ya saa 1:45 usiku matokeo yalitangazwa huku mgombea wa CCM,
Saidi Mahandula akiibuka mshindi baada ya kupata kura 286 dhidi ya 206 za
mpinzani wake, Mukoba Mukoba wa CHADEMA. Wakizungumza baada ya matokeo
hayo kutangazwa, baadhi ya wananchi walisema uchaguzi huo haukuwa wa haki kwani
watu waliopiga kura si wakazi wa mtaa husika. Uchaguzi huo umefanyika
baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Gilbert Mpanduli (CCM),
kujiuzulu tangu mwaka 2010 kutokana na kuwapo kwa mgogoro wa ardhi kati yake
yeye na madiwani wa Kwembe.
Source:
Tanzania Daima (August 2013).CHADEMA yaitikisa CCM uchaguzi Kwembe. Retrieved
from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment