MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mabaraza ya Katiba ya Wilaya za Bahi na Dodoma, wamejikuta katika wakati mgumu na kushindwa kutetea hoja ya serikali mbili. Hali hiyo imesababisha kwenda kinyume cha mwongozo wa chama chao unaowataka kupinga serikali tatu. Hayo yalijitokeza jana wakati wa mjadala wa kujadili rasimu ya Katiba mpya, unaoendelea katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini hapa. Tanzania Daima ilishuhudia majadiliano yakiendelea katika ukumbi huo huku baadhi ya makada wa CCM wakionekana kushindwa kutetea hoja ya kuwapo kwa serikali mbili. Baadhi ya makada waliopewa mwongozo wa chama hicho kutaka muundo wa serikali mbili, walishindwa kuwashawishi wajumbe kutetea hoja ya serikali mbili.
Pia katika majadiliano hayo baadhi ya madiwani wa CCM wametaka kuwapo kwa serikali moja huku wengine wakipendekeza uwepo wa mgombea binafsi. Diwani wa Kata ya Ipagala, Charles Mamba (CCM), ni miongoni mwa makada ambao wameonesha kupingana na mwongozo wa chama chake baada ya kutaka uwepo wa serikali moja badala ya mbili. “Mimi napingana na wenzangu, nataka Katiba iweke wazi, kuwe na serikali moja, serikali moja itatuunganisha na itaondoa mtafaruku wa kugombania rasilimali pamoja na madaraka,” alisema. Huku hoja ya kuwepo kwa serikali tatu ikionekana kuchukua nafasi kubwa katika mjadala huo wa siku tatu, wasomi mbalimbali nchini wameunga mkono mapendekezo ya rasimu hiyo ya Katiba.
Wasomi hao walikataa kuwa uwepo wa serikali tatu utaongeza gharama ya uendeshaji wa serikali. Walisema kinachotakiwa ni kusimamia, kujipanga na kuweka mikakati ambayo itakuwa na tija kwa kuzingatia rasilimali zilizopo. Wakati huo huo, Mratibu na Msimamizi wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba wa Wilaya ya Igunga (Tabora), Singida na Dodoma (isipokuwa Wilaya ya Mpwapwa), Fadhila Hassan Abdallah, alisema kuwa Agosti 15 hadi 16 mwaka huu, kutakuwa na Baraza la watu wenye ulemavu. Alisema baraza hilo lenye wajumbe 70 likijumuisha watu wenye ulemavu na wasaidizi wao 20, litafanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini hapa.
Source: Kaijage E. (August 2013).CCM washindwa kutetea serikali mbili. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment