Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, August 12, 2013

Bakwata yataka RPC ajiuzulu Sheikh Ponda kushambuliwa





Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa na wakili wake, Juma Nassoro katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory

        
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limelaani vikali tukio la polisi kumjeruhi Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu, Sheikh Issa Ponda na limetaka kuundwa kwa tume huru kuchunguza tukio hilo huku likimtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile kujiuzulu. Ponda amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), akitibiwa majeraha yanayoaminika kuwa ya risasi aliyoyapata Ijumaa iliyopita mkoani Morogoro. Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema baraza hilo limesikitishwa na tukio hilo na kusisitiza kwamba, uchunguzi huru unahitajika ili kuhakikisha kuwa wahusika wote wanakamatwa. 
        “Ieleweke kwamba Bakwata na Sheikh Ponda siyo maadui. Tunatofautiana mawazo tu, linapotokea suala lisilo la haki za binadamu lazima tuwe kitu kimoja,”... Sisi Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam, tumesikitishwa na tukio hilo, tunataka tume huru ya kuchunguza kifaa kilichomjeruhi na kuwabaini wahusika ili wachukuliwe hatua za kisheria. Polisi walitakiwa kutumia njia ya weledi katika kumkamata, lakini siyo kumjeruhi kama ilivyotokea.” Alisema Bakwata inamtaka Shilogile kujiuzulu mara moja ili kupisha tume huru itakayoundwa kuchunguza kwa ufasaha juu ya kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda. Alisema: “Hata kama Sheikh Ponda anatafutwa na polisi, ungetumika weledi wa kumkamata siyo kumjeruhi. Tunaamini polisi ina mbinu nyingi za kuwakamata wahalifu na Ponda kazunguka mikoa mingi ikiwemo Zanzibar walishindwaje kumkamata!” alihoji Sheikh Salum.
       Alisema ikithibitika kwamba Sheikh Ponda alijeruhiwa kwa risasi au polisi walihusika, hatua kali zichukuliwe kwa wahusika kwa sababu tukio hilo linahatarisha usalama wa nchi. Kauli ya Sheikh Salum inafanana na ile iliyotolewa na juzi na Amiri wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Yusuf Kundecha ambaye aliitaka Serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo. Hata hivyo, Polisi imeipa jukumu Kamati ya Haki Jinai chini ya Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu kuanza kazi ya kuchunguza tukio hilo. Hatua ya polisi kuanza kuchunguza tukio hilo imepingwa vikali na Sheikh Kundecha ambaye jana alisema haiyumkiniki kushiriki kuchunguza tukio hilo wakati yenyewe inatuhumiwa kuhusika.
       “Umeona wapi mtu anampiga mtu halafu huyohuyo anaunda tume eti kuchunguza kipigo na aliyepiga anakuwa ndani ya tume... hii ni sawa na Tume ya Mwangosi ambayo haikuja na majibu. Kinachotakiwa ni kuundwa tume huru ikiwashirikisha Waislamu,” alisema. Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema jana kuwa Kamati ya Haki Jinai imeshaanza kazi juzi ya kufuatilia tukio hilo kazi kubwa ikiwa ni kuchunguza namna lilivyotokea ikiwa ni pamoja na mazingira yake. Senso alisema timu hiyo imeanza kukusanya taarifa za awali na baadaye itawachukua waliohusika na tukio hilo na kwenda nao eneo la tukio kwa ajili ya kutoa ushahidi.
     “Hapa duniani hakuna kinachoshindikana, wote waliokuwapo kwenye tukio tutawapata na watatueleza namna lilivyokuwa na baadaye tutatoa taarifa.” Kuhusu kama Sheikh Ponda alipigwa risasi, alisema uchunguzi utakapokamilika, taarifa zitatolewa. Hata hivyo, alisema bado wamemweka chini ya ulinzi na atakapopata ruhusa kutoka hospitali, watamkamata na kumfikisha mahakamani kwa makosa ya uchochezi.
Moi yakwepa
      Utata kuhusu madai ya Sheikh Ponda kujeruhiwa kwa risasi umeendelea baada ya jana Msemaji wa Moi, Jumaa Almasi kusema kwamba wanachotibu ni jeraha kwa kuwa alipokewa hospitalini hapo akiwa ameshapatiwa tiba ya awali katika hospitali aliyotoka. “Kutokana na tiba ya awali aliyopatiwa ikiwa ni pamoja na kushonwa jeraha kabla ya kufikishwa Moi imekuwa vigumu kujua kama jeraha alilokuwa nalo lilisababishwa na kitu gani,” alisema Almasi.
 Source: Kiango B., Msuya M., Mhando A., Masoud A., na Hassan R. (August 2013). Bakwata yataka RPC ajiuzulu Sheikh Ponda kushambuliwa. Retrieved from Mwananchi

No comments: