Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 31, 2013

Serikali yasalimu amri kodi ya simu



 Serikali sasa imekubali kuwa kodi mpya ya laini ya simu ni mgogoro na inakusudia kurejesha muswada wa sheria ulioazisha kodi hiyo bungeni kwa mjadala zaidi. 
Waziri wa Fedha, , Dk. William Mgimwa, alisema jana alipozungumza na NIPASHE ofisini kwake jijini Dar es Salaam na mjadala huo unatarajiwa kufanywa wakati wa mkutano wa bunge unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi ujao. Mgimwa alisema kwa sasa suala hilo linashughulikiwa kwa mapana zaidi na Serikali na linatarajiwa kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi zaidi. Alisema wabunge watapata nafasi ya kujadili suala hilo na kueleza kuwa muafaka utapatikana katika vikao hivyo.

    Wakati Dk. Mgimwa akitoa kauli hiyo, leo utaratibu wa makato ya laini za simu ya Sh. 1,000 unatarajia kuanza kwa kampuni zote za simu nchini. Kodi hizo zilianza kutozwa na serikali mwanzoni mwa Julai, mwaka huu hivyo kuwalazimu wamiliki wa simu nchini kuingia gharama zaidi kwa asilimia 14.5 ili kuongeza mapato yake na kugharamia elimu. Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 bungeni Juni 13 mwaka huu, Waziri Mgimwa alisema kodi hizo zingeanza kutozwa Julai mosi mwaka huu. Dk. Mgimwa alisema kuwa kama chanzo kipya cha mapato ya Serikali, inakusudia kutoza ushuru kwenye huduma zote za simu za mkononi badala ya muda wa maongezi peke yake.

  Alifafanua kuwa asilimia 2.5 ya mapato ya kodi hiyo yatatumika kugharimia elimu nchini kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati Maalumu ya Spika ya Kushauri kuhusu mapato na matumizi ya Serikali. Vilevile alitangaza kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia 10 ya kamisheni ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi ambazo zitakusanywa na kampuni za simu kutoka kwa wakala wanaotoa huduma hizo kupitia simu za mkononi. Kwa mujibu wa Waziri huyo, mapendekezo hayo ni utekelezaji wa ushauri wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itafute vyanzo vipya vya kodi ili kuongeza mapato ya Serikali.  Wakati serikali ikiahidi kuchukua hatua hizo, tayari kodi hiyo imekabiliana na upinzani mkali kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.

     Miongoni mwake ni hatua zinazoratibiwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, za kukusanya majina ya wananchi wasioitaka kodi hiyo pamoja na kuitisha maandamano ya kupinga kodi ya laini za simu. Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnahuye, naye amekuwa aliendesha kampeni ya kuipinga kodi hiyo. Hata hivyo, waliopitisha kodi hiyo ni wabunge wote wa CCM ambao walipitisha bajeti hiyo wakati wenzao wa Chadema wakiombolezwa vifo vya watu wanne waliuawa kwa mlipuko wa bomu katika mkutano wake wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani katika kata nne za Arusha Mjini. Bomu hilo lilirushwa kwenye mkutano wa Chadema eneo la Soweto Juni 15, mwaka huu. Hadi sasa hakuna aliyekamatwa kwa ugaidi huo.



     Wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alikutana na Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Simu (MOAT) Ikulu kusikia pamoja na mambo mengine kodi ya simu itakavyokwaza maendeleao ya sekta ya mawasiliano, wakitaka serikali ifikirie kuondoa. Hata hivyo, Rais Kikwete aliwataka MOAT kutoa mapendekezo ya jinsi serikali itapata kiasi cha Sh. bilioni 178 zilizopangwa kupatikana katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2013/14 kutokana na kodi ya simu.


Source: Ippmedia (July 2013). Serikali yasalimu amri kodi ya simu. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe

No comments: