WANAKIJIJI wa Sikonge, Kata ya Misheni, wilayani Sikonge wametishia kuwafikisha polisi viongozi wa serikali ya kijiji chao kwa tuhuma za ubadhirifu na kutoweka bayana mapato na matumizi kwa zaidi ya miaka mitatu. Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi hao walisema uongozi huo unakwepa kuwasomea mapato na matumizi kila wanapoitisha mikutano na wananchi ambapo mara kadhaa mikutano hiyo huvunjika kutokana na vurugu za wananchi kutaka taarifa ya fedha. Elias Kazimoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kata ya Misheni, alisema wameamua kuungana na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kudai haki yao ya msingi.
Alitaja mali zilizopotezwa na uongozi huo ambazo wameshindwa kuzitolea ufafanuzi kuwa ni upotevu wa mashine moja ya kusaga, kompyuta, mashine ya kuchapa maandishi, vichwa vitano vya cherehani, muhuri wa ofisi na mapato yanayotokana na upangishaji nyumba ya kijiji. “Tuliwasilisha malalamiko yetu ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri yetu lakini hadi sasa hatua dhidi ya wahusika hazijachukuliwa… lakini hatutakata tamaa hadi ofisi hiyo iwachukulie hatua,” alisema.
Source: Liumba H. (June 2013).CCM, CHADEMA waungana kudai mali za kijiji. Tabora: Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment