*Yaitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu
*Mapendekezo ya Serikali tatu yazua jambo
Tangazo la kuitishwa kwa CC ya CCM, lilitolewa
mjini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana, mbele ya
waandishi wa habari ambaye alieleza kuwa itakutana Jumatatu ya wiki ijayo, kwa
ajenda moja tu ya kupitia kwa undani rasimu ya Katiba mpya. Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya chama hicho,
zimeeleza kuwa mjadala unatarajiwa kuwa mkali wakati wa kujadili suala la
Serikali tatu, ambalo tangu kutangazwa kwa rasimu hiyo ikipendekeza hivyo,
baadhi ya vigogo waliokwishatangaza au kuonyesha nia ya kuwania urais wamekuwa
katika sintofahamu ya nini cha kufanya. Ni sintofahamu hiyo, inayoonekana kukikumba pia CCM
ambacho kupitia kwa Kinana kimeeleza kuwa CC itakayoketi Jumatatu, itaangalia
kwa undani iwapo rasimu ya Katiba mpya, itakidhi matakwa halisi ya wakati huu.
“Siwezi kuzungumzia msimamo wa chama kuhusu rasimu
hiyo kwa sasa hadi Kamati Kuu ya chama, itakapokuwa imekaa Jumatatu ijayo. “Si busara kuharakisha kuzungumzia suala hilo kabla
chama hakijakaa na kuichambua kipengele kwa kipengele, kuona kama inakidhi hali
halisi ya matakwa ya kisiasa tuliyo nayo sasa,” alisema Kinana. Wakati Kinana akieleza hayo, duru za kisiasa kutoka
ndani ya CCM, zinaeleza kuwa Rasimu ya Katiba mpya imeibua hali na wasiwasi kwa
vigogo wa chama hicho wanaohofia chama chao kupoteza nguvu za mamlaka ya dola
kutokana na upepo wa kisiasa unavyovuma sasa nchini.
Wadadisi na wafuatiliaji wa mambo walio ndani ya
CCM, wanaeleza iwapo muundo wa Serikali tatu za Zanzibar, ya Tanzania Bara na
ile ya Jamhuri ya Muungano kama zilizopendekezwa na Tume ya mabadiliko ya
Katiba utaridhiwa, CCM kinaweza kuambulia ukuu wa Serikali ya Muungano pekee. Imani hii ya wadadisi na wafuatiliaji wa mambo,
inajengwa katika msingi wa uungwaji mkono na wananchi kwa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) kwa upande wa Tanzania Bara na Chama cha Wananchi (CUF)
kwa upande wa Zanzibar.
Kwa msingi huo, haina shaka kuwa CUF ambacho kina
nguvu kubwa ya kisiasa kwa upande wa Zanzibar, kinaweza kuibuka kidedea katika
kinyang’anyiro cha urais, huku Chadema kinachoendelea kujipatia umaarufu na
uungwaji mkono mkubwa wa wananchi kikichukua udhibiti wa Serikali ya Tanzania
Bara na kukiacha CCM kikibaki na udhibiti wa Serikali ya Muungano ambayo
kinaweza kushinda kutokana na historia yake ya kusaka ushindi wa jumla. Wakati wadadisi na wafuatiliaji wa mambo wakitoa
tathimini hiyo kwa upande wa vyama, wachambuzi wa siasa za ndani ya CCM
wameeleza kuwa, iwapo chama hicho kitapoteza nguvu ya udhibiti za Serikali za
Tanzania Bara na ile ya Zanzibar na kubaki na Serikali ya Muungano pekee, hilo
linaweza kuwa anguko lake la kiuchumi.
Inaelezwa CCM kikiwa na udhibiti wa Serikali ya
Muungano, hakitakuwa na ardhi ambayo kimekuwa kikiitegemea zaidi kwa ajili ya
kujiendesha kiuchumi jambo ambalo litakifanya kitegemee zaidi misaada ya
wahisani. Baadhi ya wataalamu wa uchumi, waliozungumza na
gazeti hili kwa sharti la majina yao kuhifadhiwa kuhusiana na mwenendo huo wa
mambo, walieleza kuwa CCM kikiwa na udhibiti wa Serikali ya Muungano,
hakitaweza kujiendesha na pia kitashindwa kuwahudumia wananchi kwa sababu
kitakuwa tegemezi kwa wafadhili kama vilivyo vyama vya upinzani hivi sasa.
Vyama vitavyonufaika na mfumo mpya wa uundwaji wa
Serikali kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu, ni kile ambacho kitakuwa na
udhibiti wa dola ya Zanzibar, ambacho kitadhibiti ardhi, rasilimali na uchumi
wa jumla na kile ambacho kitashika dola Tanzania Bara ambacho pia kitakuwa na
ardhi na kumiliki rasilimali za nchi. Mambo haya ndiyo yanayoonekana kuwaumiza vichwa
wanasiasa na vyama ambavyo vimekuwa vikipambana kuwania ukuu wa dola, ambapo
tangu Juni 3, siku ambayo Jaji Joseph Warioba, alitangaza rasimu ya Katiba mpya
iliyokuwa ikipendekeza kuwepo kwa muundo wa Serikali tatu, fukuto la kisiasa
kwa wanasiasa walioonyesha tamaa ya urais na vyama vinavyoiwinda Ikulu,
limepanda.
Ndani ya CCM, kuna vigogo kadhaa ambao wameonyesha
nia ya kugombea urais mwaka 2015, ambao Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa,
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano),
Stephen Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad
Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta. Kwa upande wa Chadema, watu ambao wanatajwa
kuonyesha nia ya kugombea urais ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod
Slaa, Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe. Lakini Chama cha Wananchi (CUF) nacho hakiko nyuma,
kwani Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba amekwisha tangaza nia ya
kugombea urais kwa mara ya nne mwaka 2015.
Source: Peter A.
(June 2013). RASIMU YA KATIBA: Mshtuko CCM . Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment