Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, March 30, 2013

Nusu saa ya Lissu balaa kwa Spika



HALI ya mambo si swari kuelekea mkutano ujao wa Bunge na hasa kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda,Raia Mwema likithibitishiwa ya kwamba, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amekwishajichimbia na kuandaa waraka wa unaolenga kumng’oa Spika. Pamoja na vyanzo vingine kadhaa kueleza kuhusu kuwapo kwa mpango huo unaohusisha pia wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tundu Lissu mwenyewe amethibitisha kuandaa waraka huo ambao atausoma rasmi bungeni, katika moja ya vikao vya mkutano ujao wa Bunge. Kisa kikuu cha Spika kuwekwa katika shabaha ya kung’olewa kinatajwa kuwa ni uamuzi wake wa kutumia mabadiliko ya kanuni bila mabadiliko hayo kuridhiwa na Bunge.

Tayari gazeti hili katika toleo lake la wiki iliyopita lilikwisharipoti kuwapo kwa mpango huo ambao huku Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa, Jossey Mwakasyuka, akitetea uamuzi wa Spika kutumia mabadiliko ya kanuni za Bunge kupanga upya kamati za Bunge pamoja na kumteua Mwenyekiti wa Kamati mpya ya Bunge kuhusu Bajeti, Andrew Chenge. Lakini safari hii, Tundu Lissu amezungumza na mwandishi wetu akisema; “Nilishiriki katika kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge kuhusu mabadiliko ya kanuni ambayo Spika ameyatumia kumteua Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.
“Spika alichofanya hakijawahi kufanywa katika miaka 58 ya historia ya Bunge, tangu Bunge kuanzishwa mwaka 1955. Haikuwahi kutokea mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuteuliwa na Spika iwe wakati wa ukoloni, wakati wa chama kimoja na hata tuliporejea Bunge la vyama vingi kuanzia mwaka 1995. “Spika kulazimisha kuwapo kwa kanuni inayompa madaraka ya uteuzi wa mmoja wa wenyeviti wa kamati ya Bunge ni major break (ni jambo kubwa mno), ni tofauti kabisa na utamaduni na mila za Bunge letu, kwa hiyo mabadiliko hayo ya kanuni yalipaswa kuidhinishwa na Bunge.
“Yeye mwenyewe, Naibu Spika, wenyeviti wa Bunge, wenyeviti wa kamati za Bunge na hata wawakilishi wa Bunge katika taasisi za kimataifa hupatikana kwa njia ya kuchaguliwa na si kuteuliwa, na hiyo ni kwa mujibu wa kanuni. Leo hii tunaona mwenyekiti wa kamati ya Bunge anateuliwa, kwa mabadiliko ya kanuni ambayo hayajaidhinishwa na Bunge,” anasema Lissu. Hata hivyo, katika hatua nyingine, Lissu alifichua utetezi wa Spika kuhusu uamuzi wake huo akidai ya kuwa ulilenga kupata mwenyekiti makini wa kamati hiyo mpya ya Bunge, mwenye heshima mbele ya jamii na kwamba kisipokuwapo kipengele cha uteuzi, wabunge wanaweza kuteua mwenyekiti asiye na sifa hizo.
Na kutokana na kauli hiyo ambayo pia Raia Mwema ilidokezwa na vyanzo vyetu vingine vya habari kwamba ndiyo utetezi wa Spika, Lissu anasema; “Spika ametetea uamuzi wake kwamba ulilenga kumpata mbunge mwenye high intergrity ili aongoze kamati hii, hii maana yake wabunge wengine hawana hadhi hiyo isipokuwa Chenge anayehusishwa na kashfa ya rada? “Halafu alijitetea tena akasema afanya uteuzi ili kuepusha wabunge kufanya lobbying ili kushinda uenyekiti wa kamati hii, mimi nilimwambia lobbying ili uchaguliwe bungeni ndiyo siasa za kibunge, ndiyo maana ya demokrasia ya kuchaguliwa.”
Katika hatua nyingine, mbunge mwingine wa Chama cha Mapinduzi amemweleza mwandishi wetu ya kwamba bado hakuna mabadiliko ya kanuni za Bunge yaliyoidhinishwa na Bunge, na kwamba ni kama vile kamati hiyo inayoongozwa na Chenge si halali kwa sasa. Na kuhusu hilo, Lissu pia anazungumza akisema; “Unajua kumbe kamati hii ya bajeti ilikwishaundwa tangu mwaka jana kwa sababu wajumbe wake ndiyo hao wa sasa na ilikuwa ikiongozwa na Andrew Chenge. Kwa hiyo, kwa maana nyingine, Spika alikwishaunda kamati hii na ilianza kazi mwaka jana, sisi awali tulielewa ni Ad hoc commitee (kamati ndogo ya muda) lakini kumbe ndiyo kamati ya kudumu. Sasa hapa, tangu kuwapo kwake kamati hii imetumia fedha za serikali na kwa hiyo, ni matumizi mabaya ya fedha za serikali kwa sababu kuwapo kwake hakutambuliwi.”
Kutokana na hayo, Lissu anasema anakamilisha kuandaa waraka maalumu wa kumng’oa Spika Makinda atakaousoma bungeni kwa madai kwamba uhuru wa Bunge katika mijadala na masuala mengine ya msingi unazidi kuminywa. Alipoulizwa kwa namna gani uhuru wa mijadala bungeni unaminywa, Lissu alisema kuna mapendekezo makubwa ya kutaka muda wa majadiliano bungeni upunguzwe kikanuni kutoka dakika 15 hadi 10 na katika kanuni inayohusu mabadiliko ya muswada bungeni, muda upunguzwe kutoka dakika tano hadi tatu na kwa hiyo, anaamini Bunge linazidi kugeuzwa kuwa muhuri wa kuidhinisha masuala ya watawala.
Spika wa Bunge, Anne Makinda hakuweza kupatikana kuzungumzia lawama hizo dhidi yake, simu zake za mkononi zikiwa zimezimwa kwa takriban siku kadhaa sasa. Namba hizo za simu hata hivyo ziliwekwa wazi katika mkutano wa hadhara wa CHADEMA, eneo la Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam ili wananchi wamtumie ujumbe wa simu kumtaka ajiuzulu, lakini baadhi yao walitumia vibaya namba hizo, wakimtumia ujumbe wenye matusi jambo ambalo ni kinyume cha utamaduni wa Mtanzania. Mbali na mabadiliko hayo yanayozua mvutano bungeni, mabadiliko mengine ni mkutano wa Bunge la Bajeti kuanza Aprili badala ya Juni ya kila mwaka.
Source: Raia Mwema (March, 2013).Nusu saa ya Lissu balaa kwa Spika. Retrieved Raia Mwema

No comments: