Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, March 30, 2013

Posho sehemu ya mfumo mpana wa ufisadi nchini


Wiki iliyopita Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alikaririwa akiwananga wabunge wa Afrika Mashariki kwa kushindwa kuhudhuria vikao vinavyoandaliwa na wizara hiyo kwa kutaka kwanza wahakikishiwe kulipwa posho. Kauli ya Sitta ilifuatia ile iliyotolewa na Shyrose Bhanji, Katibu wa wabunge wa Afrika Mashariki, aliyelalamika kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje kuwa wizara inayoongozwa na Sitta imeshindwa kuwapa mwongozo wanapohudhuria vikao vya Bunge la Afrika Mashariki.
Kauli zote mbili za viongozi hawa zinashangaza. Kauli ya Bhanji inashangaza kwa sababu inaonyesha kwamba wabunge wetu wa Afrika Mashariki hawajui majukumu yao, wakati walijinadi siku ya kampeni kwamba wanajua vizuri majukumu yao na kwamba wataiwakilisha vyema nchi yetu katika Bunge la Afrika Mashariki. Hadi leo sijajua akina Bhanji wanataka wapewe mwongozo gani na wizara katika kutuwakilisha wakati kuna nyaraka lundo zinahusu Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hata hivyo, leo sitojadili sana kauli za Shyrose Bhanji. Nitajadili kauli ya Samuel Sitta.

Naijadili kauli ya Samuel Sitta kwa sababu aliitoa kimunkari kana kwamba alikuwa anazungumzia jambo geni katika medani za kisiasa na maisha ya Watanzania kwa ujumla. Siamini kwamba Sitta alikerwa na kauli ya Bhanji. Ninaamini kwamba kilichomkera Sitta ni kitendo cha Bhanji kuyasema aliyoyasema mbele ya kamati ya Edward Lowasa ambaye ni hasimu wake mkubwa kisiasa. Alichofanya Bhanji ni kumwaibisha Sitta na kumpa hoja mpinzani wake kisiasa.
Kwa siasa za kimakundi ndani ya CCM sitoshangaa baadaye nikija kujua kwamba Bhanji yupo katika kundi la Lowassa na pengine ilipangwa aseme aliyoyasema ili kumuonyesha Sitta kwamba hawezi kazi! Samuel Sitta hakuwa na sababu ya kuwashangaa wabunge wa Afrika Mashariki kwa kushupalia posho kwa sababu anajua vizuri kwamba katika nchi hii hakuna kiongozi, mtumishi wala mwananchi wa kawaida anayeweza kuhudhuria kikao cha kazi bila kudai kulipwa posho.
Wabunge wetu wanalipwa posho kwa kukaa bungeni wakifanya kazi zao za kawaida. Viongozi wa taasisi za kiraia (NGOs), wizara mbalimbali na taasisi nyingine za serikali wanajua kwamba hawawezi kuwapata wabunge wetu katika semina yoyote bila kuwadokezea kwamba kutakuwa na posho. Na ikitokea ukaandaa semina isiyo na posho hawaji ama watatoka mara wagunduapo hakuna posho. Yeye mwenyewe Sitta anajua, pamoja na mawaziri wenzake, kwamba hawakubali kufungua semina, kongamano au warsha yoyote bila kupewa bahasha iliyojaa posho baada ya kukamilisha ufunguzi huo, hata kama hotuba wanazotoa wanakuwa wameandaliwa na waandaji wa tukio husika.
Katika taasisi mbalimbali za umma watu wanalipana posho kwa kukaa kwenye vikao vya nusu saa. Utakuta wajumbe wote ni viongozi na tayari wanalipwa posho ya majukumu, lakini bado wanalipana posho ya vikao maelfu na wengine hata mamilioni ya shilingi. Tena basi vikao vyenyewe vinafanyika mita kadhaa kutoka katika ofisi zao. Binafsi niliwahi kuhoji kwenye kikao kimojawapo nilipokuwa kiongozi wa wanafunzi kwa nini tunalipana posho wakati hata dawa za kusafisha vyoo hatuna nikajibiwa kuwa mbona serikalini huko mjini wanalipana! Tunaweza kuamua kufanya jambo la kijinga kwa sababu tu wengine wanafanya ujinga!
Wafanyakazi katika taasisi mbalimbali za serikali hawawezi kuhudhuria semina yoyote bila kudai kulipwa posho, hata pale semina inapohusisha mafunzo kwa ajili ya kuboresha utendaji wao. Mafunzo kwa walimu kazini yameshindikana katika nchi hii kwa sababu walimu hawataki kuhudhuria hadi walipwe posho. Sisi tunaofanya tafiti tumeanza kukwama kwa sababu wananchi wameanza kugoma kushiriki katika utafiti hadi tuwape posho, tena wanapanga na kiwango cha kuwalipa! Hata elimu ya uraia imeshindikana nchi hii kwa sababu wananchi hawakubali kuhudhuria hadi wapatiwe posho. Wanasiasa wanajua adha wanayoipata kutokana na posho. Kila waendapo wanapotembelea majimbo yao ya uchaguzi wanadaiwa posho ya vikao vya ndani na vocha za simu.
Watu hawavutiwi tena na kuchangia mambo ya maendeleo ya kijamii kama vile kuchangia ujenzi wa darasa, kanisa au msikiti, lakini watakufurahia ukiwasaidia wao binafsi. Kuna wengi ambao wamejikuta wanakata tama na kuacha kutembelea majimbo yao kwa sababu hawawezi kukabiliana na adha za posho. Kwa hiyo utaona kwamba suala la posho katika nchi hii ni sehemu pana sana ya ufisadi, na msingi wake ni kutokuamini katika jitihada kama njia ya kupata mafanikio. Tumekuwa taifa la watu wanaopenda maendeleo yetu binafsi, tena kwa njia za haraka haraka bila kutoa jasho. Tumekuwa taifa la watu wanaopenda vitu vya dezo vya kupewa na kufadhiliwa.
Mtu akipata shida kidogo anafikiri namna ya kupata mfadhili na hajishughulishi mwenyewe kuhangaika katika kutatua shida yake. Katika ngazi ya kitaifa utakuta viongozi wetu wanajisifu kwa miradi waliyofadhiliwa na miradi mingi tunayoiita maendeleo haitokani na jasho letu bali ufadhili wa wazungu. Ndiyo maana juzi alipokuja Rais wa China tulikenua meno tukacheka, tukimfurahia sio kwamba tunampenda sana, bali kwa sababu ya ufadhili wake. Na alipoondoka kesho yake magazeti yakaandika ‘Rais wa China aacha neema’; naam, tumepata mjomba, mpya, mchina!
Kwa hiyo, Samuel Sitta alimuonea bure Shyrose Bhanji na wabunge wenzake wa Afrika Mashariki kwa kushupalia posho. Kudai kwao posho walikuwa wanaendeleza tu utamaduni wetu wa kupenda vitu vya dezo vinavyokuja kwa njia ya ufadhili na posho. Zitto Kabwe aliposhupalia suala la posho alizomewa, sio tuna wabunge, bali hata na wananchi wengine akiambiwa anajitafutia umaarufu. Ndiyo maana hadi leo ni mbunge pekee asiyepokea posho ya kukaa huko bungeni, na wenzake wanaendelea kumbeza kwa kujitafutia ‘ujiko’.
Pengine malumbano haya ya akina Sitta na Bhanji yatukumbushe tena tabia hii mbaya ya kulipana posho. Na tuombe Mungu huko mbele tupate kiongozi atakayekuwa na msuli na utashi wa yeye mwenyewe kukataa utamaduni wa kulipwa posho za kukaa na atakayeamua kwa dhati kukomeshau fisadi wa posho.

Source: Mkumbo K. (March, 2013).Posho sehemu ya mfumo mpana wa ufisadi nchini. Raia Mwema

No comments: