WANANCHI OMBENI UJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA LAKINI PINGENI ‘MIANYA YA UCHAKACHUAJI’ WA UTEUZI KWENYE KATA ILIYOWEKWA NA MUONGOZO ULIOTOLEWA NA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA BILA KUZINGATIA MAONI YA WADAU
Mwongozo kuhusu
Muundo, Utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka
za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake uliotangazwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba haujazingatia maoni ya msingi yaliyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
CHADEMA inawatahadharisha
wananchi kuhusu ‘mianya ya uchakachuaji’ iliyotolewa na muongozo huo kwa
kuzingatia kuwa ‘uchakachuaji’ wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba, ni
‘uchakachuaji’ wa utoaji maoni kwenye mabaraza ya katiba, ambayo ni hatua ya
awali ya ‘uchakachuaji’ wa rasimu ya katiba.
Kwa mujibu wa Muongozo
huo, ‘mianya ya uchakachuaji’ imeachwa kwenye ngazi ya kamati ya maendeleo ya
kata ambayo wajumbe wake ni madiwani na wenyeviti wa mitaa/vijiji ambao kwa
mujibu wa matokeo ya chaguzi za mwaka 2009 na 2010 kuna hodhi kwenye vikao
hivyo ya chama kimoja (CCM).
Lakini bila kuzingatia
hali hiyo, Tume ya Mabadiliko ya katiba kupitia muongozo huo imewapa mamlaka ya
kuchagua wajumbe wa mabaraza ya katiba katika kila kata kwa upande wa Tanzania
Bara.
Muongozo huo
‘umeminya’ mamlaka ya wananchi wote kupitia mikutano yao ya vijiji na mitaa kwa
upande wa Tanzania Bara kuwa ni ‘kupendekeza’ tu majina badala ya
kuchagua.
Hata hivyo, muongozo
huo umetangaza utaratibu tofauti kwa upande wa Zanzibar ambapo wawakilishi
wakishaguliwa na wananchi kwenye mkutano wa Shehia majina yao yanawasilishwa
moja kwa moja bila kuwa na ‘mianya ya uchakachuaji’ kama ilivyo kwa Tanzania
Bara.
Hivyo, pamoja na
kuwahimiza wananchi wakiwemo wanawake na vijana kuomba kwenye ngazi ya kijiji
na mitaa kuwa wajumbe kwenye mabaraza hayo ya katiba; CHADEMA inawahimiza pia
wananchi na wadau kudai kwamba mara baada ya wananchi kuchagua wawakilishi wao
kupitia mikutano mikuu maalum kwenye vijiji na mitaa, wawakilishi hao waingie
moja kwa moja kwenye mabaraza ya katiba bila kuchujwa na vikao vinavyotawaliwa
na CCM.
Itakumbukwa kwamba
tarehe 14 Februari 2013, CHADEMA kiliwasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
maoni na mapendekezo ya CHADEMA juu ya muongozo uliotolewa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kuhusu muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya
wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake.
Maoni na mapendekezo
yaliyowasilishwa katika nyaraka ya kurasa tisa yalihusu vipengele vyote kumi
vya rasimu ya muongozo iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika maoni na
mapendekezo hayo, CHADEMA pamoja na mambo mengine hakikubaliana na muundo wa
kuwa mabaraza hayo ya wilaya yatakuwa na wawakilishi walioteuliwa na ngazi ya
kata; badala yake CHADEMA kilipendekeza kuwa wajumbe wote waliochaguliwa
kuwakilisha vijiji au mitaa au shehia waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya
wilaya.
Ikumbukwe kuwa
upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi
ilisababisha idadi ndogo ya watu waliotoa maoni ambapo mpaka awamu nne
zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni sawa na asilimia 0.7
ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9.
CHADEMA kilieleza kuwa
muundo na utaratibu huu ni muhimu katika kujenga muafaka wa kitaifa na katika
kurekebisha upungufu katika mchakato uliotangazwa kukamiilika wa ukusanyaji wa
maoni ya wananchi binafsi uliofanyika kwa awamu nne mwaka 2012 ambapo tume
ilifanya mikutano 1776 tu na wananchi wachache kutoa maoni kutokana na sababu
mbalimbali.
Imetolewa tarehe 1
Machi 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi
No comments:
Post a Comment