APOROMOSHA UFAULU KUTOKA ASILIMIA 89 HADI 43
WAKATI Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza majina ya wajumbe wa tume aliyoiunda kuchunguza chanzo cha matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana, serikali imekiri kwamba kiwango cha elimu kimekuwa kikishuka tangu Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete ilipoingia madarakani mwaka 2005. Tofauti na ahadi yake wakati wa kampeni kwamba angepandisha kiwango cha elimu, matokeo ya mitihani ya kidato cha nne tangu mwaka 2005, yameonesha kuwa kiwango cha ufaulu kimekuwa kikishuka kila mwaka. Takwimu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu zilizanikwa jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam. Alitumia pia fursa hiyo kuwatambulisha wajumbe wa tume ya kuchunguza chanzo cha kufeli kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka jana, na kupendekeza hatua za kuchukua. Kwa mujibu wa Pinda, kuanzia mwaka 2005, takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha ufaulu kilikuwa juu kwa asilimia 89.3 na mwaka 2006 kilishuka hadi asilimia 89.1. Mwaka 2007 kiwango cha ufaulu kilipanda kidogo na kufikia 90.6%, lakini kuanzia mwaka 2008 hadi sasa kimekuwa kikishuka kwa kiasi kikubwa.
Mwaka 2008 kiwango cha ufaulu kilishuka hadi 83.6% kutoka asilimia 90.6; na mwaka 2009 kilishuka hadi 72.5%. Mwaka 2010 kiwango cha ufaulu kiliporomoka hadi 51.4%; na mwaka 2011 kulikuwa na nafuu kidogo, kwani kilipanda hadi asilimia 53.6. Mwaka jana 2012 kiwango cha ufaulu kilishuka kwa kasi ya kutisha hadi asilimia 34.5, na kuibua malalamiko kila kona nchini na kusababisha serikali iunde tume. Katika hali ya kushangaza, wakati kiwango cha ufaulu kikishuka kila mwaka kuanzia mwaka 2005, serikali haijawahi kushituka na kuchukua hatua za kunusuru hali hiyo hadi mwaka huu kulipokuwa na mbinyo kutoka sehemu mbalimbali nchini kulalamikia matokeo hayo. “Kutokana na matokeo hayo mabaya ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2012, serikali imeamua kuunda tume kuchunguza tatizo hili kwa madhumuni ya kupata ufumbuzi wa kudumu,” ilisema sehemu ya taarifa ya Waziri Mkuu Pinda. “Katika suala hili itabidi tuanze kuchunguza matokeo ya tangu mwaka 2005 hadi 2012, tutajikita katika kuangalia shule zote, kwa maana ya shule za wananchi, shule za watu binafsi, shule za serikali ambako huwa tunapeleka mkono na shule za seminari, zile ambazo huwa ni washindani wetu,” alisema Waziri Mkuu.
Katika mkutano wake wa jana na waandishi wa habari, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali inafikiria kutoa fursa kwa wanafunzi waliopata daraja la nne na sifuri kurudia mitihani hiyo. Ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliofeli kurudia mitihani yao, Waziri Mkuu ameipa wiki sita tume hiyo kufanya uchunguzi na kuja na majibu yatakayosaidia kupata muundo na mfumo mpya wa elimu nchini. Mbali ya kuwapa fursa wanafunzi hao kurudia mitihani yao, Pinda pia alisema Serikali inakusudia kuwarejesha shuleni walimu wastaafu wa masomo ya Sayansi ili kunusuru hali ya elimu nchini.
Alisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na upungufu wa walimu wa sayansi katika shule nyingi za Serikali ambazo zinakabiliwa sana na tatizo la upungufu wa walimu. Akitangaza wajumbe wa tume hiyo, Waziri Pinda alimtaja Profesa Sifuni Ernest Mchome kutoka tume ya vyuo vikuu kuwa ndiye Mwenyekiti wa tume aliyoiunda kuchunguza kashfa ya matokeo ya kidato cha nne mwaka huu. Makamu mwenyekiti wa tume hiyo ni Bernadeta Kasabango Mshashu (Mbunge). Wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Francis Mbatia (NCCR Mageuzi).
Katika mkutano wa kumi wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Mbatia aliwasilisha hoja binafsi akichambua udhaifu mkubwa wa mfumo wa elimu nchini na kutaka Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza hali hiyo na kuja na majibu ya kuboresha udhaifu huo. Katika hoja hiyo alienda mbali zaidi kwa kusema Serikali haina mitaala ya elimu wala haijawahi kuwa nayo, hali ambayo ilizua mjadala mzito bungeni hadi kusababisha wabunge wa kambi ya upinzani kutoka ukumbini, huku wabunge wa CCM wakiizima kwa kejeli. Wajumbe wengine wa tume hiyo ni Abdul Jabiri Marombwa (Mbunge), Prof. Mwajabu Possi (Profesa Mshiriki wa Elimu toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Honoratha Chitanda (Makamu wa Rais Chama cha Waalimu – CWT), Daina Matemu (Katibu wa TAHOSSA), Juma Mahamoud Mringo (Mwenyekiti TAMONGSCO). Wamo pia Rajan Rakheshi, (Katibu Mtendaji Twaweza), Peter Maduki (Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii), Nurdin Mohamed, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Alharamain, (Mjumbe toka BAKWATA), Suleiman Hemedi Khamis (Mwakilishi-Baraza la Wawakilishi), Abdallah Hemed Mohamedi (Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar), Mbarouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Zanzibar), na Kizito Lawa, Mratibu wa Mitaala (Taasisi ya kukuza Mitaala).
Hadidu za rejea za tume hiyo ni pamoja na kutathimini uwiano wa mitihani iliyotungwa na baraza na uhakiki uliopaswa kufanywa na taasisi ya ukuzaji mitaala ikiwa ni pamoja na kutathmini mihutasari iliyotumika kuwaandaa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Pia kutathimini kiwango na mazingira ya ufundishaji, ikiwemo umahiri wa walimu kumudu maudhui ya masomo, mazingira ya kufundishia, matumizi ya vitabu na zana za kujifunzia, zaidi ya hapo tume inapaswa kuangalia hali ya upatikanaji wa chakula cha mchana na mchango wake katika kuinua elimu, na kuangalia athari za upungufu wa miundombinu kama vile majengo ya shule, madarasa, maabara na maktaba katika ufundishaji. Katika hatua nyingine, wakati Waziri Mkuu Pinda amemtangaza Mbatia kuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa kuchunguza kiini cha kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne, mwenyewe amegomea uteuzi huo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mbatia alisema amegomea uteuzi huo kwa sababu tatu. Mosi ni kwamba hajapata barua rasmi ya uteuzi, lakini pia ana hoja bungeni ambayo haijafika mwisho na tatu haiungi mkono tume hiyo. “Napenda nitoe taarifa kwamba mpaka leo sijapokea taarifa zozote kwa maandishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu zinazothibitisha mimi kuteuliwa huko,” alisema.
Source: Isango J. (March 3, 2013). Kikwete aangusha elimu. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment