WAKATI hali ya Shirika la Ugavi Tanzania (TANESCO) ni mbaya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakimu Maswi, wanatajwa kuwa chanzo cha kulidhoofisha kiuchumi shirika hilo, Tanzania Daima Jumatano, limedokezwa. Vigogo hao wanadaiwa kuingilia shughuli za kiutendaji za shirika hilo kisiasa na kwa maslahi ya watu binafsi. Vyanzo vya habari toka serikalini na TANESCO vinasema Muhongo na Maswi wamekuwa wakiliendesha shirika hilo kama taasisi binafsi kinyume na taratibu, jambo ambalo limesababisha hasara ya mabilioni ya shilingi kwa shirika hilo tangu waingie madarakani. Duru za kisiasa kutoka ndani ya shirika hilo, zinasema kuwa kumekuwa na msigano wa kimaamuzi kati ya shirika hilo na Wizara ya Nishati na Madini. Inaelezwa kuwa wakati Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, Felchesmi Mramba, akianzisha mchakato wa kuomba maoni ya wadau kupandisha bei, Waziri Muhongo aliibuka kupinga mawazo ya kupandisha bei kwa maelezo kuwa shirika lina pesa nyingi na serikali inalipatia ruzuku.
Mramba katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi, alisema kuwa kwa hali ilivyo sasa, hata kama TANESCO ikiamua kutolipa mishahara wala isifanye matengenezo ya mitambo, isinunue vifaa vya kuunganishia wateja, au isiingie gharama nyingine zozote, bado ingepata hasara ya karibu sh bilioni 90 kila mwezi, hivyo lazima bei ya nishati hiyo ipande ili liweze kujiendesha. Taarifa zaidi zinasema, menejimenti ya TANESCO haina mamlaka ya kuendesha kitaalamu shughuli zake isipokuwa Maswi na Muhongo ambao hawana sifa za utaalamu wa kuendesha shirika, huingilia utendaji. “Maswi na Muhongo wamekuwa wakiingilia utendaji wa kila siku wa TANESCO kwa sababu za kisiasa na sasa shirika hilo linaelekea kufilisika kabisa kwani kwa sasa linatumia sh bilioni 5.4 kwa siku huku likikusanya sh bilioni 2.3 tu, hali hiyo imetokana na maamuzi ya kisaiasa yanayofanywa na viongozi hao,” alisema mtoa habari wetu. Habari kutoka ndani ya TANESCO, zinasema kuwa Maswi na Muhongo hawataki bei ya umeme ipande kwani wamekuwa wakisema serikali ndiyo yenye shirika, menejimenti ya TANESCO ni chombo cha kuelekezwa namna ya kuiendesha tu.
Hivi majuzi, baada ya TANESCO kutaka kupandisha bei ya umeme Katibu Mkuu Maswi aliingilia kati kumshauri Mkurugenzi wa Ewura Haruna Masebu kuwa asikubali uamuzi wa TANESCO kwani ungeiaibisha serikali na walipofanikiwa Maswi alinukuliwa katika andiko moja akimwandikia Masebu kumpongeza: “Bwana Masebu, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa uungwana wako na kuamua kazi kwa kuilinda heshima ya serikali yetu. Heshima haina duka. Nakushukuru sana na naomba tuendelee kuisaidia serikali yetu pamoja na matatizo yaliyo mbele yetu. Kwa aina hii ya kushirikiana tutafika tu wala haina gogoro” Wiki hii vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti kuwa nchi iko hatarini kuingia gizani wakati wowote kutokana na hali ya uzalishaji umeme kuwa tete TANESCO. Inaelezwa kuwa hali ya shirika kifedha ni mbaya licha ya serikali kukwepa kukiri uwepo kwa mgawo ikihofia kubanwa kwa ahadi yake kuwa mgawo ungelikuwa historia.
Julai 28 mwaka jana, wakati wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Waziri Muhongo na Naibu wake, George Simbachawene, walilihakikishia Bunge kuwa mgawo wa umeme ungelikuwa historia. Lakini kwa takriban wiki nzima sasa, umeme umekuwa ukikatika hovyo kwa muda mrefu katika maeneo mengi nchini huku TANESCO ikitoa sababu za kawaida kuwa hali hiyo inatokana na matengenezo madogo kwenye miundombinu yake. Habari zaidi za uchunguzi toka ndani ya TANESCO zinasema, hata mikopo ambayo shirika linapata sasa ni kwa ajili ya kulipa madeni tu wala sio kwa ajili ya kusaidia shirika hilo lisifilisike. Ofisa habari wa TANESCO Badra Masudi alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alijibu kwa kifupi kuwa mchanganuo wa pesa za TANESCO uko wazi. Waziri Muhongo alipoulizwa kupitia simu yake ya mkononi kuhusu suala hilo, alijibu kwa kifupi tu kwamba yuko kwenye mkutano. Baadaye alipoandikiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi, hakuweza kujibu.
Ujumbe alioandikiwa na gazeti hili ulisomeka hivi: “Mheshimiwa Waziri, jana Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO amesema shirika linaendeshwa kwa hasara na wewe ulisema wanakusanya pesa nyingi, sana, taarifa ipi ni sahihi? Pia tumepata taarifa kuwa unaiendesha TANESCO kisiasa; hufuati ushauri wa wataalamu nini maoni yako?” Waziri alijibu tena kwa kifupi kwamba yuko kwenye mkutano. Jioni alipopigiwa simu, hakuweza kupokea. Tanzania Daima pia ilimuandikia ujumbe wa simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini: “Mheshimiwa Maswi, unatuhumiwa kuingilia utendaji wa kila siku wa TANESCO, je ni kweli? Au una taarifa zozote kuhusu hili?” Katibu Mkuu hakujibu ujumbe wala kupokea simu.
Source: Isango J. (March 6, 2013). Muhongo, Maswi watajwa kuiua TANESCO. Retrieved from Tanzania daima
No comments:
Post a Comment