CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kiko katika hatua za mwisho za kuandaa utaratibu wa kufanya maandamano ya amani kwa ajili ya kumng’oa madarakani Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na Naibu wake, Philipo Mulugo. CHADEMA imeeleza kuwa maandamano hayo ni ya amani na lengo lake hasa ni kuinusuru elimu ambayo iko kaburini. Akizungumza kwa njia ya simu, jana, Ofisa Habari wa Chama hicho, Tumaini Makene, alisema kuwa maandalizi makubwa wameshayakamilisha na wanachomalizia ni taratibu za mwisho na kueleza kuwa yatafanyika katika kanda za chama hicho. Akizitaja kanda hizo kuwa ni Kanda ya Ziwa katika mkoa wa Mwanza na yatahusisha mikoa yote iliyo karibu na mkoa huo, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini itakayohusisha mkoa wa Mbeya na mingine yote iliyo karibu.
Kanda nyingine ni ya Mashariki ambayo itahusisha jiji la Dar es salaam na mikoa iliyo jirani na mkoa huo na Kanda ya Kaskazini itakayohusisha mikoa ya Arusha, Manyara na mingine iliyo ndani ya kanda hiyo. Makene alisema kuwa maandamano hayo yatakuwa ya kwanza na ya kihistoria ambayo serikali haijawahi kuyashuhudia kwani yatahusisha wananchi wote. “Maandamano hayo yatahusisha wananchi wote, madereva wa bodaboda, daladala, bajaji, mama lishe, wanafunzi waliofeli na hata wale ambao hawajafeli, walimu na watu wote yaani kwa ufupi tusiite maandamano bali ni mgomo wa wananchi,” alisema Makene. Alieleza kuwa kufeli mtihani kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa asilimia 94 si jambo dogo na ndiyo maana CHADEMA imepanga kuhakikisha elimu inapanda daraja kwa kuwaondoa watu wanaokwazisha jitihada za elimu. “Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe aliwapa siku 14 wawe wamejiuzulu lakini maadamu wamekataa kufanya hivyo sasa ni mgomo wa wananchi ili kuhakikisha tunawaondoa madarakani,” alisema Makene.
Wameanza maandalizi ya maandamano hayo na watawatangazia wananchi siku husika. “Baada ya kutoa maamuzi ya maana wao wanaanza kuunda tume ya ajabu na wengine kukaa tu maofisini, tuko ‘seriuous’ katika hili na lazima lifanyike,” alieleza Makene. Nayo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imejitetea kuwa haipaswi kushutumiwa yenyewe peke yake katika hilo kwani suala la elimu linasimamiwa na wizara mbili. Chanzo chetu cha ndani ambacho hakikutaka kutajwa jina kilieleza kuwa wadau, wanasiasa na wananchi wamekuwa wakiing’ang’ania wizara hiyo pekee ikiwemo kuwataka mawaziri wake kujiuzulu na kusahau kuwa suala la elimu pia linasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Chanzo hicho kilieleza kuwa mambo ya elimu yanahusisha wizara mbili ndio maana wakati mwingine inakuwa ngumu kutolewa uamuzi na kuishauri serikali kuamua moja katika suala la elimu ili libaki katika wizara moja ili ufumbuzi upatikane. Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP, Charles Kenyela, alikiri kupokea barua ya taarifa ya maandamano ya amani kutoka CHADEMA.
“Nimepokea barua ya CHADEMA kuhusiana na maandamano juzi saa 9: 20 alasiri na tunajiandaa kutoa majibu na kuona namna ya kushughulikia suala lao, lazima kufanya mawasiliano na kuona namna ya kukabiliana na jambo hilo,” alisema Kenyela. Awali Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, aliwapa siku 14 mawaziri hao kuachia nyadhifa zao jambo ambalo wamelikaidi na kubaki madarakani. Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Mbowe alisema hilo ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya wiki mbili, vinginevyo CHADEMA ingeliitisha maandamano makubwa nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.
Source: Mnae H. ( March 6, 2013). Maandamano ya CHADEMA kumng'oa Kawamba. Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment