Muda mfupi uliopita hapa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, ametoa tamko la Musoma, likiwataka Watanzania wote wapenda nchi yao, kujiandaa kwa maandamano makubwa na mgomo wa wananchi yatakayofanyika Machi 25, 2013, nchi nzima, kushinikiza uwajibikaji (kujiuzulu au kufukuzwa kazi) kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo, kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne.
"Yatakuwa maandamano makubwa ya kuisimamisha nchi...tunataka siku hiyo mama ntilie wawe barabarani, watoto waliofeli na wazazi wao wawe barabarani, bodaboda wawe barabarani, wamachinga wawe barabarani, walimu wawe barabarani, wanafunzi walioko shuleni na vyuoni wawe barabarani, askari watuunge mkono.
"Wazalendo wote watuunge mkono, Machi 25, 2013, Watanzania wawaoneshe watawala kuwa sauti ya wananchi ni kubwa na muhimu kuliko waziri mmoja na naibu wake...tunataka kitu kidogo tu, waziri na naibu wake wajiuzulu, tunataka wawajibike kwa matokeo mabaya ambayo yametuingiza kwenye kitabu cha maajabu ya dunia..., wanaume na wanawake siku hiyo hakuna mtu kubaki ndani.
"Tutaisimamisha nchi katika majiji manne, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha...nanyi wa Musoma mnataka kulianzisha hapa? Haya Mbunge Nyerere wananchi wako nao wamesema watalianzisha hapa hapa, hawataki kuja Mwanza, kwa hiyo wa Butiama watashuka Musoma, wa Tarime watashuka hapa, wa Serengeti, Bunda na Mwibara, watashuka hapa, yataanzia wapi na kuelekea wapi, mtaambiwa hatua za baadae. Wananchi mjiandae Machi 25, maandamano na mgomo mkubwa," alisema Mbowe.
More updates to come...
No comments:
Post a Comment