MWENYEKITI wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia, amesema baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana nidhamu ya woga na wamekuwa wakiweka maslahi ya chama mbele badala ya kuweka maslahi ya Taifa. Akizungumza Dar es Salaam jana kuhusu maazimio ya kikao maalumu cha viongozi wakuu wa vyama vya siasa vyenye wabunge na Chama cha UPDP kinachowakilisha vyama visivyo na wabunge, alisema hali hiyo inasababisha hoja nyingi zenye maslahi ya wananchi kutoungwa mkono. Aidha, amevitaka vyama vitoe mafunzo kwa wabunge wake na hatimaye kila mbunge aelewe wajibu wake na kuweka itikadi ya chama pembeni pindi awapo bungeni.
Aliwataka wabunge wote wakae pamoja kukumbushana wajibu kabla ya kuanza kikao cha Bunge kitakachoanza Aprili 9, mwaka huu. Alisema nidhamu hiyo ya woga ambayo ipo miongoni mwa wabunge wa chama tawala, inafanya hoja nyingi kuzimwa kwa kuwa haziungwi mkono pale inapoonekana wabunge wengi wameonekana kutoikubali, huku wachache wa vyama pinzani wakiunga mkono. “Hoja nyingi za msingi haziungwi mkono na wabunge wa CCM, kama vile hoja ya tatizo la maji iliyotolewa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, haikuungwa mkono na wabunge wa CCM, licha ya kuwa katika majimbo yao kuna shida ya maji. “Hata ukiangalia hoja yangu kuhusu suala zima la elimu, hoja ya Hamis Kigwangala kuhusu suala la ajira kwa vijana hoja hizi zote zipo kwa maslahi ya Taifa, lakini bado haziungwi mkono na kwa kuwa wengi wape basi hata kama wachache wataunga spika atasema wengi wameshinda,” alisema Mbatia.
Alisema katika kikao hicho waliazimia mambo mbalimbali, ikiwamo wajibu wa kwanza kwa mbunge lazima uwe kwa Taifa akiwa mahali popote, lakini pia mbunge huyo lazima awe na wajibu katika eneo lake la uchaguzi, awe na wajibu katika chama chake kilichompeleka bungeni na mwisho lazima awe na wajibu kwa dhamira binafsi. “Umefika wakati sasa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ijayo uwezeshe kikamilifu kuwa na Katiba mpya yenye mgawanyo bora wa madaraka, kwa kuwa sasa hivi inaonekana mhimili mmoja ambao ni Serikali unaonekana kuwa na nguvu kuliko mihimili mingine, huku mahakama ikionekana kukosa nguvu na kuwa kama sehemu ndogo,” alisema Mbatia.
Source: Paulinus O. (March 8, 2013). Mbatia: Wabunge CCM waoga. Dar es salaam. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment