MCHAKATO wa kupata Katiba mpya, umezidi kuiva baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza rasmi uundaji wa mabaraza ya wilaya kwa kufanya uchaguzi maalumu wa wajumbe wa mabaraza hayo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, alisema mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya wilaya utaanza leo kwa watu wenye sifa kuandika barua za maombi za ujumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. Alisema hatua ya kuwapata wajumbe wa mabaraza hayo, inakwenda sambamba na ratiba iliyotolewa na tume yake kwa wananchi kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge.
“Kuanzia kesho (leo), wananchi wote wenye sifa na wanaopenda kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya wataanza kuwasilisha maombi yao kwa maofisa watendaji wa vijiji au Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa Mashehia kwa upande wa Zanzibar. “Mwisho wa kuwasilisha maombi haya ni Machi 20, mwaka huu, ambapo sifa kubwa ya waombaji ni kuwa awe raia wa Tanzania, awe na umri wa miaka 18 au zaidi, awe na uwezo wa kusoma na kuandika, awe mkazi wa kudumu wa Kijiji, Mtaa ya Shehia husika, awe mtu mwenye hekima, busara na uadilifu. “Na mtu mwenye uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo, kwa hali hiyo mwongozo uliotolewa na tume, unaelekeza kila mwombaji anatakiwa kuandika barua mbili ambazo atawaziwasilisha ofisi ya mtendaji wa kijiji au mtaa kwa Tanzania Bara na Sheha kwa Zanzibar.
Alisema uwasilishaji wa barua hizo, utakamilika Machi 20, mwaka huu, ambapo majina ya waombaji yatabandikwa nje ya mbao za matangazo, ili wananchi waweze kuwafahamu walioomba kazi hiyo. Alisema katika mikutano maalumu ya mitaa, vijiji na shehia, tume hiyo imeelekeza wajumbe wote wa mkutano mkuu maalum watapiga kura za siri wakianza kwa kumchagua mtu mzima mmoja, mwanamke mmoja, kijana na mtu yeyote miongoni mwa wananchi walioomba kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya. “Na baada ya Aprili 13 hadi 17, mwaka huu, majina ya wananchi waliochaguliwa yatawasilishwa kwa mkurugenzi wa mamlaka za Serikali za mitaa, mji, ambapo yeye atawasilisha kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kufanya uteuzi wa mwisho,” alisema Warioba.
Source: Kimwanga B. (March 8, 2013). Mchakato wajumbe wa mabaraza ya katiba mpya waanza. Dar es salaam. Retrived from Mtanzania
No comments:
Post a Comment