RIDHIWANI, NAPE WAMTUMIA KUFANYA PROPAGANDA
TUKIO la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Absalom Kibanda usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii, limechukua sura mpya baada ya mtu aliyejitambulisha kama Ridhiwani Kikwete akitumia ukurasa wake wa mtandao wa facebook kutoa maneno ya kejeli, akihoji kama nae ametekwa na Ikulu.Mbali na Ridhiwani, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, naye alitumia mateso ya Kibanda kufanya propaganda chafu, akitoa kauli inayoonesha “anawajua” waliomtesa. Ridhiwani aliandika: “Je, hii nayo ni kazi ya Rama (Afisa Usalama wa Taifa) wa Ikulu?” Rama Ighondu ndiye alitajwa na MwanaHALISI kuhusika na mateso ya Dk. Steven Ulimboka mwaka jana. Kauli hii ilichefua kwa kiwango kikubwa viongozi wa juu wa New Habari, kampuni anayofanyia kazi Kibanda, kiasi cha kumfanya Afisa Mtendaji Mkuu, Hussein Bashe, kuhoji chanzo chake. Bashe ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM, alikwenda mbali zaidi na kuandika maneno makali dhidi ya Ridhiwani:
“Huwezi kuleta kebehi ya namna hii. Inaonyesha namna gani hufahamu nafasi yako katika jamii. Funga mdomo kabisa kwa sababu unajaribu kutukana hisia za watu. “Futa kauli yako ya kijinga ya namna hii, hatuwezi kuvumilia kebehi ya kiwango kikubwa namna hii; umelewa madaraka ya kuwa mtoto wa rais, na kudanganywa na hayo mageti ya ikulu, na kudhani unaweza kuleta kebehi na dharau zako katika kila jambo… “Nakuonya iwe mwanzo na mwisho; usilete kebehi katika jambo hili. Nakuonya, nakuonya, nakuonya usijaribu! Tumekaa kimya…” Tangu Ighondu alipotajwa na MwanaHALISI kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka, serikali haijamkamata wala kumhoji. Kauli ya jana ya Ridhiwani kuuliza kwa kejeli kama Kibanda naye aliteswa na watu wa Ikulu, imeibua upya hisia mchanganyiko kuhusu sakata hilo, huku watu wengine wakisema mtoto huyo wa rais anamponza baba yake kwa kutokujua wapi atoe kauli gani. Baadhi ya waliozungumza na gazeti hili wakionesha kukerwa na kauli ya Ridhiwani, walisema mtoto huyo wa rais anafurahia mateso ya wananchi kwa sababu hajui shida zao, na amelewa madaraka yasiyo yake. Wengine wanaojua kuwa Kibanda alimfundisha Ridhiwani alipokuwa anasoma Shule ya Sekondari Shaaban Robert, Dar es Salaam, walisema hii ni dharau na kejeli iliyopitiliza, inayofanana na ukatili.
Mmoja wao alisema kauli ya Ridhiwani inatokana na kujua udhaifu au upendeleo wa serikali, na kwamba baba yake (rais) hawezi kumchukulia hatua. Wapo pia waliofikia mahali wakasema: “Mtoto huyu kuna kitu anakijua…au kuna kitu anajaribu kuficha.” Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Nape naye alitumia ukurasa wa facebook kulijadili suala hili katika muktadha wa kipropaganda, akitaka kuwahusisha watu kadhaa bila kuwataja majina. Aliandika hivi: “Hili la kutekwa na kupigwa na kuumizwa kiasi hichi (hiki) kaka yangu Kibanda, kila nikilitafakari maneno ya waliosema hakutatawalika na makala za Kibanda mbili au tatu za mwisho kabla ya kuhama chombo cha habari kabla ya anachofanyia kazi sasa vinajirudia kichwani mwangu sana!” Kauli hii inaakisi maoni kadhaa yanayosambazwa tangu juzi katika maeneo na mitandao kadhaa, yakiwanukuu baadhi ya makada na mashabiki wa CCM ambao wanasema wanalenga kuinusuru serikali isihusishwe na tukio la kutekwa kwa Kibanda. Huku wakijua kuwa Kibanda aliacha kazi Free Media na kuhamia New Habari kwa hiari yake, kama mwajiriwa yeyote, kama alivyowahi kuacha kazi New Habari, na Mwananchi kabla hajajiunga na gazeti hili, Nape na wenzake wamediriki kupandikiza propaganda kwamba kuteswa kwake kuna mkono wa mwajiri wake wa zamani.
Gazeti linajua, na Kibanda anajua, kwamba hana uhusiano mbaya na mwajiri wake wa zamani, bali amekuwa akiwindwa na kuandamwa na watu wenye mamlaka makubwa sana katika nchi hii kwa muda mrefu kwa sababu za msimamo wake wa kisiasa katika masuala kadhaa. Amepata kuitwa na kuonywa mara nyingi dhidi ya msimamo wake katika masuala ya kitaifa, na hasa kwa msimamo wake na makala zinazoonekana wazi kumuunga mkono kigogo mmoja anayechuana na wenzie ndani ya CCM katika kinyang’anyiro cha urais 2015. Gazeti hili linajua pia kwamba hata mawasiliano ya simu ya Kibanda na baadhi ya wahariri wenzake (na wa gazeti hili wamo) yanafuatiliwa kinyume na sheria. Kauli yake mwenyewe juzi akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari kabla hajapelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, inadokeza aina ya watu waliomtesa. Kibanda alisema kuwa alimsikia mmoja wa watesi wake aliyekuwa na silaha ya moto akikoki risasi na kisha kumuuliza mwenzake, “afande, tummalize?”
Wananchi waliopiga simu chumba cha habari jana baada ya kusoma kauli za Nape na Ridhiwani walisema nukuu hii ya Kibanda ndiyo inawapa kiwewe watu wanaodhani serikali inaweza kuhusishwa na tukio hili dhalimu. Mmoja wa waliojibu kauli za Nape na Ridhiwani pale pale mtandaoni, aliandika kwa hasira: “Mna dola na all machineries (taasisi zote) mnashindwa nini kuwakamata na kuwachukulia hatua? Lini mtaacha propaganda za kimisukule? “Mwigulu (anadai) anao mkanda, wewe pia unataka kutuaminisha kuwajua wahaini wa Kibanda. Kama kweli acha upuuzi, peleka maelezo polisi. Mmeanzisha propaganda za … mmeigawa nchi kwa kasi ya udini, na bado tu hamtuonei huruma tusio na pa kukimbilia?” Kibanda alivamiwa juzi Jumanne usiku akapigwa, akachomwa jicho, akang’olewa kucha, meno; na akakatwa kidole, akatupwa nje ya lango la nyumba yake iliyoko Mtaa wa Mbezi Beach, Dar es Salaam. Kutoka Dodoma, Danson Kaijage, anaripoti kuwa, Askofu wa Kanisa la Pentekoste Assembless of God (PAG), Jimbo la Dodoma na Morogoro, Charles Kanyika ameishukia serikali kwa kusema imeshindwa kulinda raia na mali zao.
Askofu Kanyika alisema hakuna sababu tena ya kuhoji juu ya nini kinachofanyika kwa waandishi wa habari na wanaharakati, bali hizi ni dalili za kuanguka kwa serikali kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wake. Aliitaka serikali itafakari upya na kuwaleta mara moja wapelelezi kutoka mashirika ya upelelezi ya kimataifa wachunguze matukio na vitendo vya kinyama vinavyoendelea. Alisema: “Mbona matukio haya yanatokea katika kipindi cha awamu ya nne wakati ambapo matukio ya wizi ikiwemo EPA, ufisadi na mauaji, lakini cha kushangazi hakuna juhudi zozote za serikali zaidi ya kuishia na taarifa za mifukoni?” Naye Happiness Mtweve anaripoti kutoka Dodoma kwamba, wananchi wameendelea kulaani matendo ya kinyama yaliyomkuta Kibanda. Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, Dk. Zainabu Chaula alisema kitendo hicho ni cha kinyama.
Dk. Chaula alisema watu hao ambao walithubutu kufanya kitendo hicho wanatakiwa kujishitaki katika nafsi zao na kuona kuwa walichokifanya hakistahili katika jamii ya Kitanzania ukizingatia kuwa tumekuwa tukitawaliwa na amani na utulivu kwa muda wote. “Kwa kweli sisi kwa upande wetu madaktari tumesikitishwa sana na tukio hili na nyie ni ndugu zetu, tunawapa pole sana ila tunaamini Mungu atampa uponyaji wa haraka hivyo tuendelee kumuombea,” alisisitiza Dk. Chaula. Ghisa Abby wa Morogoro anaripoti kuwa, Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo (MOROPC) kimelaani vikali kitendo cha kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya kwa Kibanda. “Waandishi wa habari wa Morogoro tumeshtushwa sana kwa tukio hilo ambalo linaonekana wazi sio la kijambazi, bali ni mwelekeo wa kuwatisha waandishi wa habari wasifanye kazi zao kwa uhuru, kwa kuhofia usalama wao,” alisema Mwenyekiti wa MOROPC, Idda Mushi.
Source: Tanzania Daima.(March 9, 2013). kibanda aibua makubwa. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment