Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick |
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick amekiri ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuna baadhi ya viongozi wanafuata sera ya vyama vya upinzani na kusababisha vurugu kwenye chama. Akitoa siri hiyo kwenye kikao cha Madiwani wa Manispaa ya Temeke juzi, Sadick alisema suala hilo limefikishwa mbele ya viongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ili watu wa aina hiyo washughulikiwe. Akiongea huku akionekana kukerwa na jambo hlo, asema wapo baadhi ya viongozi wa CCM wanaimba sera za vyama vya upinzani kila siku na inafikia hatua ya kuwazuia viongozi wa Serikali wasikanyage kwenye eneo lao kama sio wana-CCM.
"Kuna viongozi wetu wa CCM hivi sasa wamegeuka kama mawakala wa vyama vya upinzani, wanaongea lugha na kufuata sera zao," alisema Sadick. Alisema mradi wa Mji mpya wa Kigamboni umeweza kubainisha viongozi hao baada ya madiwani kuwa kwenye mpasuko mkubwa uliosababisha chama kutetereka. "Nimezungumza hili na Mwenyekiti wa CCM Mkoa ili kutafutia ufumbuzi, leo hii kiongozi wa CCM anadiriki kumzuia Waziri asiende kwenye eneo lake, tusipoangalia hata Rais atazuiwa eti mpaka atimize masharti yao," alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aliongeza, "Kuanzia sasa mikutano na kutumia lugha za upinzani zikome, tuwe wamoja tuondoe tofauti zetu kwa nini tunagombea fito wakati tunajenga nyumba moja?"Hata hivyo, bila kuwataja viongozi hao, alisema kikao maalum cha kutafutia ufumbuzi wa suala hilo kinaandaliwa na kiongozi yeyote aliyeonekana kwenda kinyume na sera za chama hicho atawajibishwa kulingana na kanuni na misingi ya maadili ya chama. Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa, imekuja baada ya madiwani wa halmashauri hiyo kuonyesha mgawanyiko mkubwa baada ya kuwepo na kundi la madiwani wanaopinga mradi wa mji mpya wa Kigamboni kwa madai ya kutoshirikishwa na wengine kukubaliana na mradi huo.
Source: Lusonzo M. (March 2, 2013) CCM yapata kiwewe Dar. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment