Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, amejitokeza na kubaini athari za kukithiri kwa ufisadi na rushwa ndani ya chama hicho. Makamba alishika wadhifa huo katika kipindi cha kuanzia Juni 2006 hadi Aprili 10, 2011, ambapo yeye na waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CCM) walijiuzulu. Mbali na Makamba, wajumbe wengine walikuwa manaibu makatibu wakuu, George Mkuchika (Bara) na Saleh Ramadhan Feruzi (Zanzibar), Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati. Wengine ni Katibu wa Uchumi na Fedha, Amos Makala, Katibu wa Mipango, Kidawa Saleh na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mambo ya Nje, Bernard Membe.
Hata hivyo, Makamba alikuwa miongoni mwa viongozi waliotajwa kukisababishia chama hicho kupoteza mvuto wake, miongoni mwa sababu zikitajwa kuwa kukithiri kwa tuhuma za rushwa na ufisadi. Lakini katika hafla ya kuitangaza halmashauri mpya ya wilaya ya Bumbuli wiki hii, Makamba, alieleza kukerwa na rushwa na ufisadi ndani ya CCM na serikalini. Alisema CCM na Serikali vinapaswa kuwashughulikia mafisadi na kwamba, ikiwa watashindwa kulitekeleza jukumu hilo, Mwenyezi Mungu atawaadhibu. Makamba alikuwa akizungumza kwa niaba ya wazee wastaafu walioshiriki hafla hiyo.Alisema CCM na Serikali yake vimegubikwa na mafisadi, wala rushwa, wazembe na watu wasiowajibika kwa wananchi.
Makamba alisisitiza kuwa CCM inapaswa kuyatambua matatizo hayo kwa uzito wake na kuchukua hatua kali za kuwashughulikia (washukiwa) kwa vitendo ili chama hicho kisiwe mfano wa kichaka cha wahalifu.Hata hivyo, alisema kama CCM na Serikali vitashindwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuliondoa kundi hilo, hawatakuwa salama kwa kwamba Mungu atachukua hatua dhidi yao, ili kuwaokoa watu wake. “Na ninyi mliopewa uongozi hapa (Bumbuli)…CCM si kichaka cha walafi, mafisadi na wazembe, mtambue kuwa mnawajibika na kuwa waadilifu kwa wananchi, vinginevyo kazi hii itawashinda, mtaondolewa, kama si na CCM basi Mungu atawashughulikia”, alisema. Aliwataka wananchi wa Bumbuli kusherehekea halmashauri hiyo kwa kufanya kazi, na si kucheza ngoma wala majungu.
Source: Said M. (March 2, 2013) Mzee Makamba anena: Mungu ataiadhibu CCM 2015. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment