MJI wa Mtwara, sasa unalindwa na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). Wanajeshi hao wamelazimika kuingia mitaani, kutokana na vurugu zilizotokea juzi mjini humo na kusababisha uharibifu wa mali kabla hazijahamia wilayani Masasi ambako watu tisa walipoteza maisha na mali mbalimbali kuharibiwa.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka mjini humo zinasema kwamba, kutwa nzima ya jana magari ya JWTZ yaliyokuwa na askari wenye silaha za moto, yalikuwa yakiranda mitaani ili kuimarisha hali ya usalama.
Pamoja na wanajeshi hao, askari polisi nao walikuwa wakionekana mitaani wakiwa na silaha za moto kwa kazi hiyo hiyo ya kuimarisha ulinzi.
Kutokana na hali hiyo, mji wa Mtwara jana ulikuwa tulivu na shughuli mbalimbali zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Hata hivyo, Msemaji wa JTWZ, Luteni Kanali Masoud Mgawe, alipozungumza na MTANZANIA juu ya uwepo wa askari wa jeshi hilo katika mji wa Mtwara, alisema hana taarifa.
“Sina taarifa zozote na kwa wakati huu siwezi kujua labda uniulize kesho nitakuwa nimepata jibu,” alisema Luteni Kanali Mgawe.
Naye, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Advera Senso, alipopigiwa simu ili kujua hali ilivyo mkoani Mtwara, muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa nyingine zilidai kuwa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, waliwasili mjini Mtwara jana pamoja na mambo mengine, kujionea hali inavyoendelea.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyopo mkoani humo, Pinda na Nchimbi walitanguliwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, aliyewasili mjini humo juzi.
Taarifa hizo zinasema kwamba, baada ya Pinda na Nchimbi kuwasili mjini Mtwara, walikuwa na kikao cha ndani na viongozi wa Mkoa wa Mtwara kilichofanyika katika ukumbi wa VETA mjini humo.
Baadaye jioni, walikutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini katika ukumbi huo huo na waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, eneo hilo lilikuwa na ulinzi mkali uliohusisha askari wa JWTZ pamoja na askari polisi.
Hali ilivyo Masasi
Taarifa kutoka mjini Masasi ambako vurugu kubwa zilitokea juzi kuliko zilizotokea mjini Mtwara, zinasema kutwa nzima ya jana mji wa Masasi ulikuwa tulivu.
Chanzo chetu cha habari kilichoko mjini Masasi kilisema kuwa, katika mji huo, hakukuwa na biashara zozote zilizokuwa zikifanyika.
“Kaka hakuna biashara zozote hapa leo, mji uko tulivu sijawahi kuona, yaani nikikwambia kuko tulivu ujue kuko tulivu.
“Huwezi amini, mimi nilikuwa na shida ya fedha lakini nimeshindwa kwenda kwenye Mpesa kwa kuwa hawafanyi kazi badala yake kuna mtu kaniazima Sh 10,000.
“Hata gari yangu iko nyumbani tu nimeshindwa kutoka nayo kwa sababu hali haitabiriki, kwani hata ukienda pale stendi ambako huwa kuna watu na magari mengi, utakuta kama siyo basi moja utakuta mawili, watu hakuna kwa maana ya hakuna,” kilisema chanzo chetu hicho.
RPC azungumza
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki, aliwaambia waandishi wa habari juzi kwamba, watu 44 wanashikiliwa na polisi wilayani Masasi kutokana na vurugu hizo.
Alisema kwamba, katika vurugu hizo, mali mbalimbali ziliharibiwa ikiwamo ofisi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wilayani humo, Mahakama ya Mwanzo Lisekese, ofisi ya ukaguzi wa shule za msingi, ofisi ya ununuzi na ugavi pamoja na magari sita ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Beatris Dominick, alisema magari 11 yaliharibiwa wakati wa vurugu yakiwamo sita yaliyochomwa moto.
Aliyataja magari hayo kuwa ni yenye namba za usajili SM 960, aina ya Toyota Landcruser, STK 8778 aina ya Landrover, STK 8417 aina ya Prado, SM 2636 aina ya Pajero, ambulance yenye namba SM 3840 na SM 9721 aina ya Tiper.
Mengine yaliyochomwa moto ambayo ni mali ya watumishi wa halmashauri hiyo aliyataja kuwa ni yenye namba T419 BNG T120 AQP, T402 BUC pamoja na pikipiki tano na baiskeli moja.
Pamoja na hayo, alisema baada ya tukio hilo, walifanikiwa kuokoa bunduki kumi na risasi zaidi ya 100 na nyara za Serikali zikiwamo meno ya tembo yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye chumba maalumu cha kuhifadhia nyaraka.
Zitto, Mtikila wazungumza
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amemtaka Rais Jakaya Kikwete, atoe majibu kuhusiana na mgogoro wa gesi na vurugu zinazoendelea mkoani Mtwara.
Zitto alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kwamba, mwenye majibu ya kinachoendelea mkoani Mtwara ni Rais Kikwete kwa kuwa anajua jinsi mradi wa Mnazi Bay ulivyo pamoja na mradi wa gesi.
“Swali kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni tutanufaikaje na jibu la swali hili si ahadi za miradi bali vitendo, hapa ndipo Serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili.
“Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kuwasikiliza wananchi na si kuwahutubia tu, wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa muafaka. Serikali isimamishe mradi huu mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana kwani vurugu hizi zinatokea kwa sababu viongozi hatutaki kuwasikiliza wananchi.
“Wakati juhudi hizo zinaendelea, Serikali nayo iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Jamani nchi inaungua, hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita ya Majimaji,” alisema Zitto.
Mchungaji Mtikila
Naye, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikilia, amezungumzia vurugu hizo na kumtaka Rais Jakaya Kikwete aende haraka mkoani Mtwara kuzungumza na wananchi wa mkoa huo.
Pia, ameitaka Serikali kuacha kutumia nguvu kubwa kupambana na wananchi kwa kuwa wananchi wa mkoa huo wamechoka kuonewa.
Mtikila alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema vurugu hizo zisipozimwa kwa hekima, zinaweza kuenea katika mikoa yote ya kusini na kusababisha vurugu kubwa.
Vurugu za Mtwara zilianza Ijumaa iliyopita, ambapo wananchi walichoma moto jengo la Mahakama ya Mwanzo, nyumba ya Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia na nyumba ya Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mtwara.
Juzi, vurugu nyingine zilitokea wilayani Masasi ambapo nyumba ya mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe (CCM) na ya Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), zilichomwa moto.
Pia wananchi waliharibu kituo kidogo cha polisi, walichoma moto mahakama ya mwanzo mjini humo, walichoma magari mbalimbali na kuharibu mali kadhaa.
Source: Ibadi, M. (January 28, 2013). Masasi na Dar: Mtanzania.
No comments:
Post a Comment