Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, January 29, 2013

VURUGU ZASABABISHA HUDUMA KUKWAMA MASASI



HUDUMA zinazotolewa na idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na serikali kuu, zimesimama baada ya watumishi kushindwa kufanya kazi kutokana na kuteketezwa kwa nyaraka na moto kwenye vurugu zilizotokea mwisho mwa wiki iliyopita.
Wakati huduma hizo zikikwama miili ya watu saba waliouwawa kwa kupigwa risasi na polisi wilayani humo imezikwa. Maiti hao ambao wawili wamefahamika, wamezikwa maeneo ya makaburi ya Masasi Mbovu, Nyasa na Upanga katika mji wa Masasi, kati ya saa 4:00 asubuhi na 10:00 alasiri juzi.
Wakati huohuo, watuhumiwa 53 wa vurugu za Masasi wamefikishwa Mahakama ya Wilaya na kusomewa mashtaka mbalimbali, ikiwamo kula njama na kutenda kosa la kuchoma moto majengo na uharibifu wa mali.

Kuhusu kukwama kwa shughuli wilayani humo jana, watumishi walifika kazini kama kawaida lakini walilazimika kukaa katika makundi huku wengine wakichambua mabaki ya nyaraka za ofisi zao zilizoteketezwa kwa moto. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Ofisa Elimu Taaluma wa Wilaya Shule za Msingi Garama Kinderu alisema wafanyakazi hao walishindwa kufanya kazi kutokana na ofisi na nyaraka zote kuteketezwa moto.
Kinderu alisema Idara ya Elimu imeathirika zaidi kutokana na kupoteza kumbukumbu nyingi zikiwamo za walimu, wanafunzi na taarifa za maendeleo ya elimu, baada ya nyaraka zote na kompyuta kuungua.
“Kwa kweli hali ni mbaya sana, kwani hapa kila kitu kimeteketezwa hakuna kumbukumbu iliyobaki,” alisema Kinderu.
Licha ya jengo la elimu, wafanyakazi wa idara ya mahakama ya Mwanzo na ofisi zingine kadhaa za Halmashauri ya Wilaya na Mji wa Masasi, hawakuingia kazini, huku huduma za fedha, ikiwamo benki na zile zinazotolewa na mitandao ya simu za mikononi; Tigo Pesa, M-Pesa, Airtel Money na EzyPesa, zikifungwa.
Wafanyabiashara wa maduka ya vyakula, masoko ya mbogamboga na maduka ya nguo nao walisitisha huduma zao na kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa eneo hilo, kwa kile walichoeleza kuwa ni hofu ya kukamatwa na polisi waliokuwa wamemwagwa kwa ajili ya upelelezi.
Mohamed Rajanu, Aisha Bakari na Joseph Godfrey walisema kwa nyakati tofauti kuwa tukio hilo limewaletea adha ya maisha, hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
“Mchele, sukari, mafuta ya kupikia, ngano na bidhaa zingine za msingi zimekuwa ngumu kabisa kupatikana kwa kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote wilayani humu aliyefungua duka,” alisema Godfrey.
Bakari aliwaomba wafanyabishara kuanza kurejesha huduma hizo ili kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji huduma ambazo kimsingi hakuna njia mbadala wa kuzipata.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Masasi, Beatrice Dominick alisema vurugu hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali, hasa baada ya ofisi za taasisi kadhaa kuteketezwa.
“Bado thamani halisi ya vitu ambavyo vimeteketezwa hatujaipata, lakini kama mnavyoona hapa jinsi uharibifu mkubwa ulivyofanyika... hapa huwezi kufanya kazi kwa mazingira haya,” alisema.

Source: Mwananchi (January 28, 2013)

No comments: