Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ameibua tuhuma nzito
dhidi ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), akisema kuwa wamekaidi ushauri wa kitaalam uliowazuia wasitumie mfumo
mpya wa Biometric Voter Registration (BVR) katika uandikishaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura.
Mbowe amedai
kuwa baada ya kuona zoezi la kuandikisha wapiga kura haliendi kama
ilivyotakiwa, NEC walimtafuta mshauri mwelekezi aitwae Darrell Geusz, mtaalam
wa masuala ya BVR kutoka Marekani ambaye baada ya kufanyia utafiti ‘hali’ ya
Tanzania kuhusu mfumo huo mpya, aliwaambia wakilazimisha wanaweza kusababisha
machafuko ya kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa
Mbowe, mtaalam huyo katika ripoti yake aliyoitoa mwezi Januari mwaka huu,
aliiambia NEC kuwa kwa sasa Tanzania haiwezi kuandikisha wapiga kura kwa mfumo
wa BVR kwa sababu ya ukosefu wa fedha, vifaa, utaalam na muda kwani mfumo huo
ili uweze kufanya kazi inayotakiwa unahitaji maandalizi ya takriban mwaka
mmoja.
Mwenyekiti huyo
wa CHADEMA ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ameyasema hayo
jijini Mbeya wakati alipohutubia matukio mawili tofauti, akiwa katika ziara
yake ya siku nne katika mikoa ya Kanda (ya CHADEMA) ya Nyanda za Juu Kusini
yenye mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma na Rukwa.
Mapema asubuhi
Mwenyekiti Mbowe alihutubia wakati akifungua kikao cha Baraza la Uongozi wa
CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kisha baadae jioni akahutubia mkutano wa
hadhara kwenye Uwanja wa Dk. Slaa mjini Mbeya. “Mshauri huyo
mwelekezi ambaye ni mtaalam wa masuala ya BVR kutoka Marekani, amewahi
kuisaidia nchi ya Bangladesh ambako waliandikisha wapiga kura milioni 80,
aliwaambia NEC kuwa Tanzania hatuwezi kuendesha hili zoezi kwa sasa, hatuna
vifaa, hatuna wataalam, hakuna muda wa kutosha, hatuna wataalam, hatuna
maandalizi, akawatahadharisha wakilazimisha wanaweza kusababisha machafuko.
“Lakini katika
hali ambayo haijulikani, wakiendeleza ukaidi kwa ajili ya kutaka kuibeba CCM,
NEC inaonekana kutaka kuendesha zoezi hili bila kuzingatia ushauri wowote wa
kitaalam wala kushirikisha wadau ambao ni vyama vya siasa wala haitaki kutoa
taarifa za kutosha kwa wananchi ambao ndiyo wapiga kura wenyewe. “NEC imekuwa
ikiendesha suala hili kwa usiri usiri sana, taarifa zao wanapoamua kutoa
zimekuwa za kusua sua sana, kwa kushtukiza. Tumekuwa tukidai ushirikishwaji wa
kina wa shughuli na mfumo huu bila mafanikio. Tumeomba sana kupata nyaraka ili
tuelewe, lakini hawataki. Wanafanya siri kubwa.
“Sasa nasi kwa
sababu tunazo njia mbalimbali za kupata taarifa, tumezipata nyaraka ambazo
hawataki wadau kwa maana ya vyama vya siasa tuzione. Kwanza tumepata
nyaraka ambayo inaonesha kuwa wakati walikuwa wanasema hawana kitu cha
kutupatia ili tuelewe mfumo huu wa BVR, wao labda na CCM yao tangu 2013
walikuwa tayari wanajua kitakachofanyika. “Lakini pia
tumefanikiwa kupata nyaraka nyingine hii hapa. Hawa jamaa wa NEC baada ya
kuzidiwa wakaamua kutafuta mshauri mtaalam kutoka Marekani ambaye anasifika
duniani, yaani katika masuala ya BVR ni authority, ameandika ripoti yake yenye
kurasa 16, amewapatia hadi ushauri wa tahadhari ya madhara ya kiusalama jamaa
wa NEC na Serikali ya CCM hawataki kusikia,” amesema Mbowe.
Mbowe ameongeza
kusema kuwa wakati mshauri huyo mtaalam wa BVR akiwatahadharisha NEC kuhusu
muda, tume imeendelea kusema kuwa zoezi hilo litafanyika na kufanikiwa kwa
kipindi cha ndani ya miezi miwili, jambo ambalo Mwenyekiti wa CHADEMA amesema
kuwa serikali inacheza na ‘roho ya amani katika nchi’. Alisema kuwa
mazingira yanayoendelea nchini Tanzania katika suala la mchakato wa hatua
mbalimbali za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, yanatengeneza hali ya kutokuaminiana
miongoni mwa wadau, akisema kuwa hali hii husababisha uchakachuaji na katika
nchi zingine imesababisha machafuko ya kisiasa.
NEC na
ubabaishaji katika ratiba
Mbowe amesema
kuwa tangu mwaka jana NEC imekuwa ikitoa taarifa za kukanganya kuhusu ratiba
kamili ya kuanza kuandikisha upya wapiga kura nchi nzima, ambapo iliwahi kusema
shughuli hiyo ingeanza Septemba 2014, baadae ikaahirisha hadi Desemba, lakini
pia haukufanyika, kisha baadae ikatoa ratiba ya kuanza kazi hiyo Februari 16 mwaka
huu, ikianza na mikoa minne ya Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara. Kiongozi huyo
amesema kuwa baada ya vyama vya siasa kuibana NEC juu ya ratiba na maandalizi
muhimu kuhusu shughuli hiyo huku muda ukikaribia, tume ikawaita wadau na
kuwaambia kuwa zoezi limesogezwa mbele ili kuvipatia vyama vya siasa muda wa
kuandaa mawakala, hivyo litaanza Februari 23, mkoa mmoja pekee wa Njombe badala
ya mikoa minne kama ilivyotangazwa awali.
“Tukawaambia
mnasema tuwaandae mawakala wetu, tuwaandae kuhusu kufanya majukumu yapi hasa na
hamtaki kutupatia nyaraka, bado wakaendelea kutoelewa. Tukawaomba hata ratiba
ya mkoa huo mmoja bado hawakuweza kutupatia. Yaani ni ubabaishaji tu. Sisi
tukaamua kupeleka watu wetu huko mkoa mzima kuanza maandalizi. Tayari
tunavyozungumza tuna watu wako field. “Katika hali ya
kushangaza sana, jana tukapokea ratiba yao, wakaongeza maajabu mengine tena.
Ratiba yao inaonesha kuwa hata mkoa mmoja wa Njombe pekee wameshindwa
kuandikisha mkoa mzima badala yake wataanza na jimbo moja tu la Njombe
Kaskazini. Katika jimbo hilo pia hawawezi kuandikisha kata zote kwa wakati
mmoja badala yake wataanza na kata mji mdogo wa Makambako.
“Yaani
wameshindwa mikoa minne, wakaamua mkoa mmoja, mkoa mmoja hawawezi kuandikisha
wilaya zote, hata wilaya moja wameshindwa, wataanza na jimbo moja na katika
jimbo hilo wataandikisha kata 12, sio zote kwa pamoja wataanza na kata 9 za mji
mdogo wa Makambako, kisha zitafuata kata zingine. Hii ni aibu ya hatari,”
amesema Mbowe na kuongeza;
“Yaani wakati
mamilioni ya Watanzania wanasubiri kuandikishwa nchi nzima, NEC haiwezi hata
kuandikisha wilaya moja kwa wakati mmoja. Halafu eti wameniandikia barua ya
mwaliko kwenda Makambako kushiriki hafla ya uzinduzi utakaofanywa na Waziri
Mkuu Pinda siku ya Jumanne ijayo, nawauliza viongozi wenzangu niende nisiende.
“Kwa sababu
kwenda kwenye uzinduzi huo wa NEC utakaofanywa na Waziri Mkuu ni kubariki uhuni
wote huu wanaoufanya.”
Serikali
kufilisika, ukosefu wa vifaa vya BVR na kuchezea Sheria
Mwenyekiti
Mbowe ameshusha tuhuma nzito kwa Serikali ya CCM akisema kuwa kushindwa
kupatikana kwa vifaa vya BVR kwa muda unaotakiwa ili wananchi waanze
kuandikishwa kunatokana na serikali hiyo kufilisika, kukosa vipaumbele,
kuendekeza ufisadi na matumizi ya anasa huku pia ikilifanya zoezi la uchaguzi
kuwa ni tukio la dharura badala ya mchakato wenye maelekezo ya kikatiba. Alisema kuwa
kugeuza uchaguzi kuwa tukio la dharura badala ya takwa la kidemokrasia lenye
masharti ya kisheria ni kucheza na haki na matumaini ya Watanzania jambo ambalo
linaweza kuhatarisha amani ya nchi. “Ili
kuandikisha wapiga kura nchi nzima, NEC ilihitaji vifaa…wanaviita BVR kits
vipatavyo 15,000 lakini Serikali ya CCM ikawaambia hapana wapunguze,
wakapunguza hadi 8,000, katika hivyo 8,000 hadi sasa vipo 250 pekee tangu
wakati wa uandikishaji wa majaribio. Hadi sasa vingine havijafika kwa sababu
serikali haijalipia, haijalipa kwa sababu imefilisika.
“Pamoja na
mazonge haya yote, juzi nimemsikia Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lubuva akisema
daftari hili hili watakaloandikisha litatumika kwenye Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa, huyu mzee tunamheshimu sana lakini wamempatia kazi
itakayoondoa heshima yake. Huyu ni mwanasheria, Jaji mstaafu. Sitaki kuamini
kuwa hajui kuwa kuhakiki daftari kabla halijaanza kutumika ni hitaji la
kisheria.
“Sheria
inaagiza kwamba baada ya uandikishaji lazima wapiga kura wahakiki daftari lao
kisha sasa ndipo tunapata daftari la kudumu la wapiga kura. Sasa kwa ratiba yao
wanamaliza kuandikisha Aprili 29 na kesho yake Aprili 30 kura ya maoni inapaswa
kupigwa, sasa sijui anataka kutumabia nini. “Pamoja na
kwamba sisi kama CHADEMA pamoja na wanachama wenzetu wa UKAWA tumewaomba
Watanzania kutoshiriki kupiga kura ya maoni ya katiba ili wasitumike
kuhalalisha mchakato haramu, lakini hatutakubali sheria ziendelee kuvunjwa tu
waziwazi na akina Lubuva kwa sababu ya maelekezo ya ikulu huku NEC ikitumika tu
kama kanyaboya,” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa
serikali nyingi duniani hukaribisha machafuko na anguko lake kila zinapoanza
kuchezea chaguzi mbalimbali. Alisema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu
ulijulikana miaka 5 iliyopita kikatiba hivyo maandalizi yake hayawezi kuwa ya
zimamoto au dharura. Alisema sheria
ya uchaguzi inaelekeza wazi kuwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linapaswa
kuboreshwa mara mbili katikati ya uchaguzi mmoja hadi mwingine, lakini hata
takwa hilo la kisheria pia limevunjwa na NEC ambayo imeshindwa kuboresha tangu
ilipoandikisha mwaka 2010.
“Yaani
wakati Watanzania wenye sifa wakisubiri nchi nzima, taifa zima linasubiri,
katika sintofahamu hii, bado viongozi wetu wanathubutu kudanganya kuwa kura ya
maoni itafanyika, huku Waziri Mkuu Pinda akienda kubariki mchezo huu keshokutwa
huko Makambako. Hatujui wanapata wapi ujasiri huu wa kuwadanganya
Watanzania,”amesema Mbowe.
No comments:
Post a Comment